Prime
Kitongoji cha ajabu, hakina huduma hata moja ya kijamii

Mwonekano wa Kitongoji cha Mbuyuni kilichopo kijiji cha Chaumbele Kata ya Magubike wilayani Kilosa mkoani Morogoro. Wakazi wa eneo hilo wanakabiliwa na ukosefu wa shule, huduma za afya na maji.
Muktasari:
- Kitongoji hicho kilichopo umbali wa kilomita 109.6 kutoka Morogoro mjini, ili kukifikia lazima utumie usafiri wa pikipiki ukivuka milima, mabonde, vijito na misitu kinapatikana mpakani mwa Wilaya ya Gairo na Kilosa.
Dar/Morogoro. Zikiwa zimesalia siku 11 shule kufunguliwa, zaidi ya watoto 90 wa Kitongoji cha Mbuyuni hawataanza darasa la kwanza kutokana na kukosekana kwa shule ya msingi katika eneo hilo.
Siyo hao pekee, bali inaelezwa watoto wa umri wa kuwepo shuleni na watu wazima wengi wao hawajafanikiwa kusoma kutokana na wakazi wa eneo hilo kushindwa kuwaandikisha watoto wao. Hiyo ni kutokana na huduma hiyo kuwa mbali na kitongoji kilipo. Pia, inaelezwa kuwa hali hii ilianza miaka 30 iliyopita tangu kitongoji hicho kianzishwe.
Kitongoji cha Mbuyuni chenye wakazi zaidi ya 1,000 kinachotambuliwa kuwa kipo ndani ya Kijiji cha Chaumbele, Kata ya Magubike Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, pia kinakabiliwa na ukosefu wa huduma za afya na maji.
Kitongoji hicho kilicho umbali wa kilomita 109.6 kutoka Morogoro mjini, ili kukifikia lazima utumie usafiri wa pikipiki huku ukivuka milima, mabonde, vijito na misitu minene na kipo mpakani mwa Wilaya ya Gairo na Kilosa, hali inayodaiwa kuonekana kugombewa na wilaya hizo mbili.
Kwa nini kikose huduma
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa mgodi uliopo karibu na eneo hilo ulisababisha mvutano wa wilaya ipi itanufaika na mapato kwa Wilaya za Gairo na Kilosa.
Mvutano huo unadaiwa kudumu kwa muda mrefu kati ya viongozi wa pande hizo mbili, hali ilyosababisha kutofanyika kwa shughuli zozote za maendeleo ikiwamo ujenzi wa shule, zahanati na hata miradi ya maji safi na salama.
Kitongoji hicho kina majina mawili; upande wa Kilosa kinajulikana kama Mbuyuni, wakati upande wa Gairo kinaitwa Mahedu au Mitoji. Hata hivyo, wakazi walioishi kwa muda mrefu kitongojini hapo akiwamo Grace Wilson (84) anasema, "Nimezaliwa hapa na panaitwa Mbuyuni, lakini nilishangaa tulianza kuitwa majina mengine baada ya kuanza kwa mgogoro huo wa kugombea mgodi."
Diwani wa Magubike, Abuu Msofe anasema eneo hilo lina changamoto za muda mrefu ambazo hazijapatiwa ufumbuzi kwa zaidi ya miaka 25 sasa.

Anasema ili kitongoji hicho kipate suluhu ya changamoto zao, kuna haja ya Serikali kutazama upya mipaka kati ya wilaya za Gairo na Kilosa kusudi sasa wananchi waweze kupata huduma za msingi na za haraka zinazohitajika.
Msofe anasema ingawa juhudi za Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka alizoanza kuchukua kuanza kuonesha mwanga, lakini hali bado tete.
Anasema hata wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mtaa uliomalizika Novemba mwaka jana, wananchi waligomea kujiandikisha wakitaka ufafanuzi kuhusu eneo lao.
"Changamoto kubwa ni ukosefu wa miundombinu ya afya, maji, barabara na elimu. Hali hii inasababisha watoto zaidi ya 90 kushindwa kuanza shule kila mwaka na watu wazima wengi katika eneo hili hawajui kusoma wala kuandika," anasema Msofe.
Mwananchi ilizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka ambaye amekiri kuwepo kwa changamoto hizo huku akitaja chanzo kikuu ni mgogoro wa mipaka.
Hata hivyo, anasema tayari hatua zimeshaanza kuchukuliwa kutafuta suluhisho la kudumu.
"Nilipofika kitongojini mwaka 2024, niliwaagiza wakazi kutenga maeneo kwa ajili ya shule na zahanati. Tayari suala la upatikanaji maji linaendelea kushughulikiwa. Mgogoro wa mipaka umeshughulikiwa na tulikuwa tunasubiri tu ukamilike mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili Kamishna wa Ardhi aje na timu yake kufanya tathmini ya mipaka," anasema Shaka.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima anasema: "Mkuu wa Wilaya ya Kilosa ameeleza kila kitu kinachotakiwa kusemwa, na amenifahamisha kuwa tayari walifika eneo la tukio, kwa hiyo tayari tatizo limeanza kushughulikiwa."
Walia kukosa elimu
Hakika, ukistaajabu ya Musa, utayaona ya firauni. Hali hii inajidhihirisha wazi katika kitongoji hiki ambacho shule zipo mbali na watoto wanalazimika kuvuka mito mitatu mikubwa mvua zinaponyesha.
Alfred Mganga (48) anasema ingawa alipata nafasi ya kusoma alipokuwa mdogo, hakufanikiwa kusoma kwa bidii kutokana na umbali wa Shule ya Msingi Chaumbele, iliyopo zaidi ya kilomita nane kutoka kilipo kitongoji chao.
“Hatuna shule hapa. Nililazimika kusoma katika Kijiji cha Chaumbele, lakini sikuhudhuria masomo mara kwa mara kwa sababu ya umbali. Tulijitahidi kama wanakijiji, tukafyatua tofali 20,000 na tukapata bati 50 kutoka kwa mwekezaji wa machimbo ya madini. Hata hivyo, uongozi wa wakati huo ulitumia vifaa hivyo vibaya,” anasema Mganga.
Mganga anaongeza kuwa changamoto nyingine ni ukosefu wa barabara na majisafi, hali inayowalazimu kunywa maji kutoka kwenye visima vya kienyeji.
Mkazi mwingine, Daudi Mchae (50) anasema wazazi wake walimzuia kwenda shule wakihofia asije akaliwa na wanyama wakali msituni.
“Watoto hawapati elimu. Mimi mwenyewe sikusoma kwa sababu ya umbali wa shule. Zaidi ya miaka 30 imepita sasa, kila mtoto anayezaliwa hapa ananyimwa haki ya kupata elimu,” anasema.
Samson Mwendi, mkazi mwingine anasema hali ya kitongoji hicho ni mbaya kutokana na kukosa huduma ya maji safi, shule na barabara.
“Watoto wangu sita hawajasoma kwa sababu ya umbali wa shule ilipo,” anasema Mwendi.
Inaelezwa tatizo la ukosefu wa elimu imekuwa kikwazo kikubwa kwa vijana wa Mbuyuni, kiasi cha kushindwa hata kutumia simu za mkononi kutokana na kutojua kusoma na kuandika.
Daudi Asheri (26) anasema tatizo hilo linawanyima fursa nyingi za kiuchumi, hasa biashara.
Ezekia Mhina (25) anasema wanapigania watoto wao wapate elimu ili waweze kuzisaidia familia zao siku zijazo.
Huduma za afya, maji
Wakazi wa eneo hilo wanasema changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni pale wanapopata mgonjwa, iwe mchana au usiku, ni vigumu kumpakiza kwenye usafiri wa pikipiki. Hivyo hutumia machela kumbeba mgonjwa.
Changamoto hiyo ni kubwa zaidi kwa wajawazito ambao wanalazimika kutumia usafiri wa bodaboda kupita kwenye milima na mabonde, hali inayosababisha wengi wao kujifungulia njiani kutokana na mtikisiko.
Ajili Justine (22) anasimulia jinsi alivyojifungulia njiani mtoto wake wa kwanza miaka mitatu iliyopita. Anasema uchungu ulimuanza jioni na alipanda bodaboda kwenda hospitali lakini akajikuta akijifungulia njiani akisaidiwa na mama yake mzazi.
"Walinichukua na mtoto nikaenda hospitali, nikapata tiba kidogo na kuruhusiwa kurudi nyumbani. Hata hivyo, kichwa cha mtoto wangu kimebaki kimebonyea mpaka leo," anasema Ajili.
Rosa Jackson anasema wanatumia Sh12,000 kwa usafiri wa pikipiki kutafuta huduma za afya.
Pamoja na changamoto hizo, Rosa anasimulia jinsi alivyojifungua kwa upasuaji baada ya kubebwa kwa machela hadi hospitali.
"Mwaka 2010 nilibebwa kwenye kitanda nikiwa nimelala chali mpaka Belega. Safari hiyo ilichukua saa nne na nusu nikiwa na uchungu wa siku mbili. Tulipofika hospitali, nilifanyiwa upasuaji na kupata watoto wawili. Wakati huo hakukuwa na usafiri wa pikipiki," anasema Rosa.
Grace Wilson (84), anakumbuka miaka 60 iliyopita wanawake walijifungulia nyumbani. Iwapo matatizo yalitokea, walibebwa kwa machela hadi kituo cha afya cha Belega, safari iliyochukua saa nne hadi tano.
Serikali yafafanua
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Peter Julius anasema hakuna watoto wanaosoma kutokana na ukosefu wa shule ya karibu.
Anasema zamani watoto walilazimika kutembea kilomita nane kwenda Shule ya Chaumbele, jambo ambalo liliwafanya wazazi kukosa amani. Hali imezidi kuwa mbaya kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamesababisha mafuriko na kuongeza changamoto kwa jamii hiyo.
“Nina kundi la watu wenye umri wa miaka mitano hadi 30 ambao hawajasoma na hatuna uhakika lini shule itapatikana. Zamani, watoto walilazimika kutembea kilomita nane kwenda na kurudi, lakini sasa hakuna anayesoma,” anasema Julius.
Hata hivyo, anasema uongozi wa wilaya ulitembelea eneo hilo mapema mwaka jana na kuahidi kujenga shule, zahanati na kuboresha upatikanaji wa maji safi.
“Licha ya ahadi hizo lakini bado hakuna kilichofanyika mpaka sasa,” amesema.
Diwani wa Magubike, Msofe anasema wauguzi kutoka Magubike hufika mara kwa mara kutoa chanjo, lakini hali ya miundombinu mibovu na mvua nyingi hujikuta wakikwama.
Anasema barabara iliyopo ni mbovu haipitiki hasa eneo ulipo mto mkubwa unaotoka Berega kupitia Ibindo kuelekea Dumila unapokuwa na maji mengi.
“Miundombinu ni mibovu, na mjamzito anapopata uchungu analazimika kusafiri kilomita 20 hadi Magubike, jambo ambalo ni mateso makubwa. Tunatamani tupate hata kisima, eneo hili halijawahi kupata maji safi na salama tangu kianzishwe,” anaeleza Msofe.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Morogoro (Moruwasa), Tamim Katakweba amesema suala hilo limewasilishwa kwao linaendelea kushughulikiwa.
Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Sospeter Lutonja amesema tayari wamechimba kisima kimoja cha mkono kwenye Kitongoji cha Shuleni na wanatarajia kuchimba visima zaidi katika Wilaya ya Kilosa, ikiwemo eneo hilo, Januari hii.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka amesema wakurugenzi wa wilaya za Gairo na Kilosa, pamoja na Kamishna wa Ardhi, watafanya kazi ya kutafsiri mipaka ili kuondoa mvutano wa kisiasa uliopo.
Kuhusu upatikanaji wa umeme, Shaka amesema mkandarasi amethibitisha kuwa kuanzia mwezi huu, kitongoji hicho kitakuwa na umeme kufuatia agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha umeme unafika hadi ngazi za vitongoji.