Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kinana: Watanzania changamkieni fursa kituo cha biashara Ubungo

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Abdulrahman Kinana (kulia) akiwa na aliyewahi kuwa Balozi wa China nchini Tanzania, Lu Yuoqing walipokuwa wakikagua ujenzi wa kituo Cha biashara cha EACLC leo Februari mosi, 2024 jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Kituo hicho cha biashara Ubungo kinatarajia kuzinduliwa rasmi kwenye maadhimisho ya Sikukuu ya Sabasaba Julai 7, 2024.

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amewataka Watanzania kuchangamkia fursa zinazopatikana kwenye kituo cha biashara cha Ubungo (EACLC) kinachojengwa jijini Dar es Salaam.

Kinana ametoa wito huo leo Februari mosi, 2024 alipotembelea kituo hicho kinachoendelea kujengwa, huku akisisitiza haitakuwa na maana kama kituo hicho kitakamilika na kutumiwa na watu kutoka nje ya nchi.

“Nitoe wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa hii na ningependa kuona asilimia 100 ya wafanyabiashara wa kituo hiki wawe ni Watanzania, tusije tukafungua halafu tukakuta watu kutoka nchi jirani ndio wamekuja kuchukua fursa hii,” amesema.

Kinana amesema ni dhahiri Watanzania na wafanyabiashara wa nchi za jirani hawana sababu ya kusafiri kwenda nchi za nje kufuata bidhaa, kwani zitakuwa zikipatikana katika kituo hicho.

“Nawahakikishia kuwa Serikali yetu inatoa msukumo katika uwekezaji kwenye sekta binafsi kama sehemu ya kukuza biashara, ajira na mapato ya Serikali,” amesema kiongozi huyo wa chama tawala.

Kwa upande wake, Balozi Lu Yuoqing ambaye aliwahi kuwa Balozi wa China nchini Tanzania kati ya mwaka 2012 hadi 2017, amesema Serikali ya China itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali ili kuleta maendeleo hapa nchini.

Amesema ushirikiano wa nchi hizo mbili ni wa kihistoria tangu enzi za waasisi wa mataifa hayo, Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Mao Tse Tung wa China.

“Nakumbuka hata mipaka ilipofunguliwa baada ya mlipuko wa ugonjwa wa Uviko 19, Rais wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan ndiye alikuwa Rais wa kwanza kutembelea China,” amesema Yuoqing.

Kinana pamoja na Yuoqing wamekagua ujenzi unavyoendelea katika kituo hicho cha biashara cha kimataifa kinachotarajiwa kuwa na takriban maduka 1,800 na ofisi 200.

Kituo hicho kinatarajia kuzinduliwa rasmi kwenye maadhimisho ya Sikukuu ya Sabasaba inayofanyika Julai 7, 2024.