Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kinana ajiuzulu CCM, Samia aridhia

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana (katikati) akiwa na waliokuwa mawaziri January Makamba (kushoto) na Nape Nnauye (kulia) ambao uteuzi wao ulitenguliwa hivi karibuni. Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Taarifa ya kuomba kujiuzulu imetolewa leo kwenye taarifa ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla.

Dar es Salaam. Mwanasiasa mkongwe nchini,  Abdulrahman Kinana ameomba kujiuzulu wadhifa wa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM)-Bara.

Kinana mwenye miaka 71, alirejea ndani ya chama hicho kwa nafasi hiyo Aprili 1, 2022 alipochaguliwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM kwa kura za ndiyo 1875 sawa na asilimia 100.

Alichaguliwa akichukua nafasi ya Philip Mangula ambaye aliandika barua ya kung’atuka kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia ambaye aliliridhia.

Kurejea kwa Kinana kulielezwa na wadau wa siasa ndani na nje ya CCM, kuwa kulilenga kukipa nguvu chama hicho  kutokana na weledi na uzoefu  wake.

Awali Kinana alikuwa  Katibu Mkuu wa CCM na  alisifika zaidi kwa uchapaji kazi wake kwa kufanya ziara mikoani hadi ngazi za mashina, huku  akiikosoa vilivyo Serikali na watendaji wake walioonekana kutokwenda na kasi wakiwemo mawaziri aliowaita ‘mawaziri mizigo.’

Baada ya kukaa kwa siku 850 sawa miaka miwili na miezi mitatu, Kinana ameomba kupumzika na ombi lake limeridhiwa.

Leo Jumatatu, Julai 29, 2024, taarifa ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla imeeleza Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia ombi la Kinana aliyeomba kupumzika.

Makalla amemnukuu Rais Samia akisema: “Ni kweli nilipokuomba utusaidie kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti nilikuahidi utakaa muda mfupi kama ulivyoomba, na kwa kweli nilipenda uendelee kutusaidia, lakini kwa kuwa umeomba sana na ahadi ni deni nalazimika kwa moyo mzito kuridhia kujizulu kwako.”

Pia, Makalla amesema mwenyekiti wa CCM amesisitiza chama kitaendelea kutumia uzoefu na maarifa ya Kinana kila vitakapohitajika na chama kinamshukuru kwa mchango wake mkubwa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk George Kahangwa amesema umri unaweza kuwa sababu za kuamua kuomba kujiuzulu, kwa sababu amefanya kazi kubwa ndani ya chama hicho.

“Mchango wa Kinana ulikuwa ni mkubwa sana akiwa katibu mkuu kwa kukisaidia chama kwa kuzunguka mikoani na wakati huu wa makamu mwenyekiti, alikuwa anatumia uzoefu wake kuwashauri kiutu uzima,” amesema Dk Kahangwa na kuongeza:

“Hana mchango tu ndani ya chama lakini hata ndani ya nchi. Akiwa makamu mwenyekiti hakuonekana sana, lakini uzoefu wake umekisaidia sana CCM.”