Prime
Kikokotoo kilivyomtenda mstaafu Jeshi la Magereza

Aliyekuwa mtumishi wa Jeshi la Magereza Tanzania, Salum Shamte.
Muktasari:
- Suala la kikokotoo lilianza kufukuta mwaka 2018 baada ya iliyokuwa Mamlaka ya Kudhibiti Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kuandaa kanuni mpya zilizolenga kukipunguza kwa watumishi wa umma kutoka asilimia 50 hadi asilimia 33 na kupandisha kutoka asilimia 25 hadi 33 kwa watumishi wa sekta binafsi.
Dar es Salaam. Aliyekuwa mtumishi wa Jeshi la Magereza Tanzania, Salum Shamte (56), amesimulia namna kanuni za kukokotoa mafao (kikokotoo) ilivyosababisha apigwe butwaa baada ya kupokea ujumbe (sms) wa kiasi cha fedha za pensheni ya kustaafu alicholipwa.
Anasema alipokea sms ikionyesha malipo ya Sh21 milioni badala ya Sh55 milioni aliyotarajia baada ya kuitumikia Serikali kwa miaka 33.
Alipotafutwa na Mwananchi, Kamishna Jenerali wa Magereza, Mzee Nyamka amesema utaratibu wa malipo ya pensheni haupo kwa Mkuu wa Magereza, Waziri wa Mambo ya Ndani au Katibu Mkuu.
"Mfuko wa pensheni ya kustaafu unalipwa kulingana na michango aliyotoa na kikokotoo kinazingatia utaratibu huo,” amesema.
"Pensheni halipi CGP, Waziri wa Mambo ya Ndani au Katibu Mkuu, ila inategemeana na michango yake aliyoitoa," amesema.
Salum aliyestaafu akiwa na cheo cha Staff Sajenti Kikosi Maalumu cha Kutuliza Ghasi Magerezani (KMKG), Dar es Salaam, anasema aliposoma ujumbe huo alihisi macho yake yana ukungu kiasi cha kutokusoma vizuri tarakimu.
"Niliomba msaada wa mke wangu anisomee, akanitajia vilevile. Miaka 33 napata Sh21 milioni na kiasi hicho nimekatwa Sh10 milioni, nilikuwa nimekopa Chama cha Ushirikia wa Akiba na Mikopo cha Watumishi wa Jeshi la Magereza Tanzania Bara (TPS Saccos)" anasema Salum.
Mstaafu huyo aliyetembelea ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata Relini anasema licha ya kufanya kazi kwa uadilifu, kikokotoo kimeathiri ndoto zake.
Salum anasema alitarajia baada ya kustaafu akanunue maeneo aanzishe shughuli za kilimo.
"Najiona mfungwa mtarajiwa, kwa sababu Sh10 milioni zilizobakia kuna baadhi ya watu niliwakopa muda wote wanazengeazengea nyumbani kwangu wakihitaji niwape chao,” anasema.
"Hata nikitoa hakitatosha, nitaishi katika mazingira magumu. Nashindwa kusimulia, tunafanya kazi katika mazingira magumu ni kama vile Serikali haitambui umuhimu wetu. Kikokotoo sikujua makali yake, sasa najionea," anasema.
Salum anasema mwanzoni wakati watu wanalia kuhusu kikokotoo alikuwa anaona kawaida lakini ameona ukali wake, hivyo kutoa wito kwa watumishi wengine wasijione wako salama.
"Familia yangu hainielewi inahisi nimekula fedha, lakini hata wale niliowakopa nao hawanielewi, wanasema nina fedha niwalipe chao wakafanye shughuli zao. Ninaishi kama digidigi, muda wote nalala ndani," anasimulia.
Anasema hali ilikuwa ngumu, mke wake na baadhi ya majirani wakamtuliza kwa kumtaka awe na subira.
“Nilipofuatilia kwenye uongozi wa Magereza waliniambia Serikali imeshaamua na sisi hatuna namna nyingine ya kukusaidia, kikubwa ridhika.Kuna wengine walikuwa wananishauri nisubiri tamko la Serikali kusitisha kikokotoo,” anasema.
Anaeleza aliposikia kauli ya Serikali siku ya Mei mosi kupitia kwa Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango haoni mwanga.
Katika Sherehe za Mei mosi zilizofanyika kitaifa mkoani Arusha, Dk Mpango alisema uamuzi wa kukibadilisha kikokotoo utatokana na tathmini ya kina ya kisayansi ya watakwimu bima.
Salum anasema,“nimeona nipaze sauti yangu kupitia vyombo vya habari ili familia na wale wanaonidai wajue maana kila nikiwaeleza hawanielewi kabisa. Na Serikali ijue shida tunazozipitia, na sisi tuna mahitaji na mipango mingi.”
“Rais inawezekana halifahamu hili kama sisi wastaafu tunapitia shida hizi, atusaidie vinginevyo tutakufa tuna majukumu mazito ikiwamo kusimamia familia,” anasema.
Salum anasema hata wakati wanaanza kutoa elimu ya kikokotoo hicho walielezwa watakatwa kidogo sehemu ya mshahara wao baada ya kustaafu na utakaribiana na waliokuwa wanapokea walipokuwa wakifanya kazi.
Anasema baada ya kustaafu kwa mwezi anapokea Sh290,000 wakati kipindi anafanya kazi mshahara kwa mwezi ulikuwa Sh745,000.
Historia yake
Salum mzaliwa wa Rufiji mkoani Pwani anasena alianza kazi Jeshi la Magereza mwaka 1990 Kiwira mkoani Mbeya akiwa Kuruta.
Anasema alijiunga rasmi na Jeshi hilo mwaka 1991 katika Gereza la Maweni mkoani Tanga.
“Mwaka 1992 nilihamishiwa Gereza la Chumbageni, lakini mwaka 1993 nilirudi tena Maweni, baadaye mwaka 1994 nilihamishiwa Kikosi Maalumu cha Kutuliza Ghasi Magerezani (KMKG), Dar es Salaam,” anasema.
Mwaka 1996 hadi 2006 alihamishiwa Kisongo katika Gereza la Umoja wa Mataifa Arusha walikokuwa waanzilishi kabla ya kuhamishiwa Dar es Salaam kuendelea na kazi KMKG hadi alipostaafu mwaka 2023.
Msimamo wa Serikali
Hoja ya kikokotoo iliibuliwa katika risala ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), iliyosomwa Mei mosi 2024.
Dk Mpango aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan alisema uamuzi wa mabadiliko ya kanuni hiyo, utatokana na tathmini ya kina ya kisayansi ya watakwimu-bima na Serikali inaamini Tucta itawasilisha maoni yake.
“Tunawategemea wataalamu wetu watushauri kuhusu suala hili la uhimilivu na uendelevu wa mifuko ya hifadhi ya jamii, tunawahakikishia wafanyakazi hakuna mtu angependa kuona watu waliotumikia nchi hii wanaathirika kwa kukosa kiinua mgongo stahiki au pensheni zao,” alisema.
Kwa mara kadhaa suala la kikokotoo limekuwa likiibuliwa bungeni na wabunge wakitaka Serikali kufanya marekebisho.
Suala la kikokotoo lilianza kufukuta mwaka 2018 baada ya iliyokuwa Mamlaka ya Kudhibiti Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kuandaa kanuni mpya zilizolenga kukipunguza kwa watumishi wa umma kutoka asilimia 50 hadi asilimia 33 na kupandisha kutoka asilimia 25 hadi 33 kwa watumishi wa sekta binafsi.
Hatua hiyo ilipigiwa kelele na watumishi wa umma, ndipo hayati Rais John Magufuli alipoivunja SSRA na kuahirisha matumizi ya kanuni hizo, akitaka zianze kujadiliwa mwaka 2023.
Julai 1, 2022, Serikali ilipeleka suala hilo bungeni, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako alisema kikokotoo kipya kinafanya wafanyakazi wote wa Tanzania wa sekta ya binafsi na umma, kutumia viwango sawa vya ukokotozi wa mafao.
Kanuni hizo zimeendelea kulalamikiwa na wafanyakazi, huku baadhi ya wabunge wakikishikia bango katika mijadala yao.