Kijana amuua baba yake akimtuhumu mchawi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, ACP Theopista Mallya.
Songwe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limemtia hatiani kijana mmoja (32) ambaye jina lake limehifadhiwa mkazi wa Kijiji cha Hantesya Wilaya ya Mbozi kwa madai ya kumuua baba yake mzazi akimtuhumu kumloga.
Kijana huyo anadaiwa kutoroka mara baada ya kumuua baba yake kwa kipigo usiku wa Oktoba 13 kuamkia Oktoba 14, 2023 katika Kijiji cha Hantesya Kata ya Nyimbili wilayani Mbozi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, ACP Theopista Mallya amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa usiku wa kuamkia Oktoba 17 katika Kijiji jirani cha Hantesya na kwamba kwa sasa anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
"Kijana huyo anadaiwa kumuua baba yake Menard Msongole (80) maarufu kwa jina la Gaga kwa tuhuma za ushirikina kwa kumpiga na kitu kizito kichwani," amesema RPC Mallya
Naye Ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Sekela Tuya amesema kijana huyo amekamatwa katika kijiji cha Msamba 1 alikokuwa amekimbilia baada ya kutekeleza mauaji ya baba yake mzazi usiku wa kuamkia Oktoba 14 mwaka huu.
Endelea kufuztilia Mwananchi na mitandao yetu kwa habari zaidi.