Kiama wapigaji fedha za bima ya afya, NHIF kikaangoni
Muktasari:
- Katika kutekeleza bima ya afya kwa wote, Serikali imetenga Sh660 bilioni kwa ajili ya makundi maalumu ya wasio na uwezo, wajawazito, wazee, watoto na wenye ulemavu, na usajili wa ndani umekamilika kwa asilimia 95.
Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, ametoa onyo kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na watoa huduma dhidi ya wizi, ulaghai na ubadhirifu wa fedha za bima ya afya kwa wote.
Aidha, amevipa rungu vyombo vya habari kuibua changamoto za kimfumo kupitia kalamu zao, hatua zitachukuliwa pale ambapo makosa yatabainika.
Amesisitiza kuwa, wakati nchi ikiingia katika mfumo wa bima ya afya kwa wote, ndani ya mfumo wanakabiliwa na maadui wawili, ugonjwa na mifumo, ili kufanikisha mifumo hiyo, vyombo vya habari vinapata nafasi kubwa.
Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa akizungumza wakati wa kikao kazi cha wahariri na waandishi wa vyombo vya habari na redio jamii zilizo kote nchini, kilichofanyika leo Jumatatu, Januari 2, 2026 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Amesema Tanzania imejifunza kutokana na makosa ya nchi zilizotangulia, hivyo watahakikisha wanaweka, wanalinda na kusafisha mifumo kwa maslahi ya Taifa ili huduma ziwe endelevu.
Mchengerwa amesema hayo leo Jumatatu, Februari 2, 2026, wakati wa kikao kazi cha wahariri na waandishi wa vyombo vya habari na redio jamii kutoka kote nchini, kilichofanyika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam.
"Sitakubali chini ya uongozi wangu NHIF ichezewe. Katika hili niko tayari kuchukiwa na watu, na tunaomba waandishi wa habari mtubainishie haya mapungufu kupitia kalamu zenu kwa sababu tumedhamiria kuboresha sekta ya afya," amesema.
Amesema NHIF kuchelewa kulipa madai sababu ya ulaghai, wizi na utapeli kupitia mifumo ni mambo aliyoyataka yakamulikwe akisema hayupo tayari wakati wake kuona mifumo ikiyumba.
Baadhi ya wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya, wakiwa katika kikao kazi kati ya Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, wahariri na waandishi wa vyombo vya habari na redio jamii zilizo kote nchini, kikao hicho kimefanyika leo katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.
"Ulaghai ukiachwa, fedha zinaanza kutoka na kupotea, wahudumu wasiwafanye wananchi wakaikatia tamaa bima, na wagonjwa wanarudi kwenye hofu ya gharama. Mwisho, imani ya wananchi itaondoka.
"Hata sera itakuwa ngumu kutekelezeka, ulaghai si wizi wa fedha pekee, ni wizi wa huduma. Msimamo wa Serikali ni kulinda mifumo na kulinda wanaofichua maovu. Tutaongeza nguvu kwenye malipo ya madai, tutakagua nyayo za miamala ili kudhibiti, na tutagundua mapema kupitia ukaguzi wa ndani, tukishirikiana na vyombo vya uchunguzi," ameongeza.
Amesema hatua hizo zitaambatana na kuchukua hatua za kisheria, kuondoa watoa huduma wasiofaa na mawakala wasio waaminifu.
Aidha, amesema uongozi wa awamu ya sita unajenga mifumo endelevu katika kulinda afya, utu na ubinadamu, kwani Taifa lolote linaweza kusimama iwapo wananchi wake wana afya bora, hivyo afya ni usalama wa Taifa.
Mchengerwa amesema kuelekea uzinduzi wa bima ya afya kwa wote, linaweza kuwa tukio la siku moja, lakini uelewa wa Taifa ni wa siku zote, hivyo amesisitiza kuwa ahadi ya siku 100 za Rais akiwa madarakani linatekelezwa kwa kuweka mazingira bora ya huduma, nidhamu ya kazi, kujenga ubunifu na kuwatia moyo watumishi wa umma.
Rais Samia aliapishwa Novemba 3, 2025, na siku 100 zitakamilika Februari 11, 2026.
Mchengerwa ameagiza vitengo vya habari kuhakikisha vinawajibika katika kufikia elimu kwa umma, na Katibu Mkuu wa Afya kuhakikisha kitengo cha mawasiliano kilichopo wizarani kinawajengea uwezo vitengo vya habari vya hospitali na ngazi za chini ili kufikisha elimu kwa jamii.
Onyo hilo la Mchengerwa kwa NHIF linatolewa huku ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zikibaini ‘madudu’ ndani ya mfuko huo, ikiwemo matibabu hewa ya wagonjwa.
Katika ripoti hiyo ya mwaka 2021/22, ilibainisha wafanyakazi wa NHIF walijikopesha Sh41.42 bilioni na kusuasua kuzilipa. CAG alieleza hadi Juni 30, 2022, NHIF ilikuwa na mikopo ya wafanyakazi ambayo haijalipwa Sh41.42 bilioni, kati yake Sh11.18 bilioni ikiwa mikopo mipya iliyotolewa 2021/22.
CAG alisema mikopo hiyo ilitolewa bila kuzingatia mahitaji ya aya 1.4 ya sera ya mikopo ya wafanyakazi wa mfuko ambayo inahitaji mikopo kutolewa chini ya mfumo wa kukopa na kulipa.
Baadhi ya wahariri kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania, TEF wakifuatilia mkutano kati ya Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa na wadau wa habari nchini.
Ripoti ya CAG ya 2019/20 ilionesha Serikali ilipata hasara baada ya kukataliwa madai ya Sh4.48 bilioni kutokana na makosa ya ujazaji wa taarifa za wagonjwa, ikiwemo idhini batili, kutozingatia miongozo ya matibabu, kutoonesha vipimo vya utambuzi na kuingizwa kwa huduma zisizo rasmi.
Aidha, CAG alibaini NHIF kulipa vituo vya afya madai yasiyo ya kweli kiasi cha Sh14.46 bilioni kwa kipindi cha 2019/20 hadi 2021/22, wakiwemo baadhi ya watumishi wa mfuko.
Mada ya NHIF
Akitoa mada, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk Irene Isaka, amesema hatua zilizofikiwa ni kutekeleza maagizo ya Waziri wa Afya. Mpaka sasa, wameshasajili kwa mifumo ya ndani asilimia 95 ya kaya, ikijumuisha kaya zaidi ya 200,000.
"Tumefanya usajili wa ndani kwa namba za kaya na kadi, imebaki kwenda katika kaya kuchukua alama za vidole na picha. Tumeshasajili wazee, wasiojiweza na wanawake 490 na sasa tunaendelea na usajili," amesema.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe, amesema baada ya nchi kupata Uhuru, wananchi walipata matibabu bure kwa muda, lakini kutokana na mabadiliko ya nchi na uchumi mwaka 1990, Serikali ilianza kuchangia huduma na wananchi kuchangia.
Amesema hilo lilianza hospitali za juu, na mfumo wa bima ya afya ukaanza kwa sekta rasmi. Serikali iliruhusu wasio na uwezo wapewe matibabu bure.
"Serikali sasa inapanua huduma kutoka vituo 8,549 kufikia 12,846, kulikuwa na haja kuhakikisha kila kijiji kina zahanati na kila kata ina kituo cha afya. Ongezeko hili limeenda sambamba na kusimika vifaa tiba vya X-Ray, CT Scan, MRI, na sasa PET Scan," amesema Dk Shekalaghe.
Awali, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema vyombo vya habari vina uwezo wa kuwafikia watu milioni 30 hadi 40 kwa wakati mmoja, hivyo lazima vitumike kufikia wananchi wengi.
"Tunafahamu bima ya afya kwa wote inakwenda kuleta mabadiliko na inaondoa wasiwasi kwamba nikipata changamoto yoyote nitatibiwa. Tukihamasisha Watanzania milioni 12 kulipa Sh150,000 tu, nchi itakusanya trilioni 1.8, na Watanzania hawawezi kuwa na hatari kubwa ya matibabu," amesema Balile.
PET Scan yaanza kazi
Waziri Mchengerwa amezindua Mashine ya PET CT Scan katika Hospitali ya Ocean Road, Dar es Salaam, ni ya kwanza kununuliwa tangu uhuru.
Mashine hiyo ameizindua ikiwa ni wiki chache tangu alipotoa maagizo yake Desemba 8, 2025 wakati alipofanya ziara yake Hospitali ya Taifa Muhimbili.
"Mashine hii imenunuliwa mwaka 2022 kwa gharama ya karibu Sh20 bilioni, ina uwezo wa kuzalisha dawa tiba ikilinganishwa na mashine zingine za Afrika Mashariki,” amesema.
Kutokana na uwepo wa mashine hiyo nchini, Mchengerwa ametoa maagizo kwamba: “Kuanzia sasa, safari zote za wagonjwa kwenda nje ya nchi zimetamatika na Serikali imeokoa mabilioni ya fedha, gharama zilizotumika kupeleka wagonjwa nje."
Amesema kipimo hicho kiliigharimu Serikali kati ya Sh6 mpaka Sh8 milioni kila mgonjwa anapopimwa nje ya nchi, nje ya gharama za usafiri, malazi na huduma nyingine mtu anapokuwa nje ya nchi, lakini sasa kipimo hicho kitawagharimu wagonjwa Sh1.2 milioni pekee.
Kuhusu kiwanda cha kuzalisha dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa sasa kimechukuliwa na Serikali na ina hisa ya zaidi ya asilimia 70.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk Diwani Msemo amesema PET CT Scan ni uchunguzi wa kimatibabu unaounganisha teknolojia ya PET inayoonesha utendaji wa seli/metaboliki na CT inayoonesha muundo wa viungo ili kutoa picha za 3D zenye maelezo ya kina.
Amesema mashine hiyo hutumika kugundua saratani, kuangalia ukubwa wake, na kufuatilia matibabu, pamoja na matatizo ya moyo na ubongo.
Ameyataja mambo muhimu kuhusu mashine hiyo kwamba kiutaratibu dawa maalumu ya mionzi (tracer) hudungwa mwilini ikufuatiwa na kusubiri kwa dakika 60-90 ili isambae, kisha mgonjwa hupita kwenye mashine kwa dakika 15-60.
“PET Scan hugundua saratani mapema, kubaini maeneo ya biopsy, kupanga radiotherapy, na kutathmini magonjwa ya moyo. Usalama wake uchunguzi hauna maumivu, ingawa unahusisha mionzi kidogo, na tracer haidumu mwilini kwa muda mrefu.
“Kwenye maandalizi wagonjwa wanashauriwa kufunga kula kwa saa kadhaa kabla ya kipimo.
Ni teknolojia muhimu inayoonesha mabadiliko ya kimetaboliki kwenye seli kabla hata ya muundo wa kiungo kubadilika, jambo linalosaidia ugunduzi wa mapema,” amebainisha.