KESI YA MJANE WA BILIONEA MSUYA: Utata taarifa za kifo cha Aneth ulivyowapambanisha wakili, shahidi

Muktasari:
- Mahakama imepokea vielelezo viwili kuhusu tukio la mauaji ya Aneth Msuya kupitia mashahidi wawili tofauti wa upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji hayo, ambao wote maafisa wa Polisi.
- Hata hivyo, shahidi mmoja amepinga kielelezo kingine kilichotolewa na shahidi Ofisa wa Polisi mwenzake na mkubwa wake kwa cheo kuwa si sahihi na hapo ndipo shahidi huyo anakumbana na maswali ya Wakili Kibatala. Shahidi huyo amesema nini, kaulizwa maswali gani na kayajibuje? Fuatilia.
Dar es Salaam. Shahidi wa 24 katika kesi ya mauaji ya Aneth Elisaria Msuya, amewasilisha mahakamani Ilani ya Kwanza (taarifa ya awali ya tukio la mauaji ya Aneth), ambayo imepokewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa kielelezo cha 17 cha upande wa mashtaka (prosecution exhibit 17 -PE17).
Shahidi huyo, F832 Sajenti Obadia Joseph kutoka Makao Makuu ya Upelelezi Dodoma, kitengo cha Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya amewasilisha mahakamani taarifa hiyo jana, Ijumaa, Septemba 8, 2023, wakati akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo.
Hii ni kesi namba 103 /2018 inayomkabili Miriam Steven Mrita, ambaye ni mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara tajiri maarufu wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya; na mwenzake Revocatus Everist Muyella maarufu Ray.
Aneth ambaye aliuawa Mei 26, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam, alikuwa mdogo wa Bilionea Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Agosti 7, 2013.
Kupokewa kwa taarifa hiyo iliyowasilishwa na shahidi huyo wa 24, Sajent Obadia na kusajiliwa kama kielelezo cha 17 cha upande wa mashtaka kunafanya Mahakama hiyo kuwa na vielelezo vya aina hiyo viwili ambavyo vyote vinaelezea tukio moja.
Kabla ya Sajenti Obadia, awali taarifa kama hiyo iliwasikisha na shahidi wa nne wa upande wa mashtaka, SSP Richard Mwaisemba, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kigamboni (OC-CID), wakati akitoa ushahidi wake, Machi Mosi, 2022
SSP Mwaisemba alitoa kielelezo hicho ambacho ni nakala kivuli, baada ya kuombwa na Wakili Peter Kibatala anayemwakilisha mshtakiwa wa kwanza, Miriam; wakati akimhoji maswali ya dodoso shahidi huyo kuhusiana na ushahidi wake alioutoa.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za mahakama ambazo zilisomwa jana, kufuatia maombi ya wakili Kibatala, SSP Mwaisemba alipooneshwa fomu hiyo aliitambua akasema kwamba ingawa haikupita mikononi mwake lakini imesainiwa na Inspekta Fredrick Nyudike.
Nyudike ni shahidi wa nane katika kesi hiyo ambaye alichora ramani ya eneo la tukio la mauaji ya Aneth aliyoiwasilisha mahakamani kuwa kielelezo cha upande wa mashtaka wakati akitoa ushahidi wake.
Hivyo Mwaisemba alipoulizwa na Wakili Kibatala kama ana tatizo kuitoa mahakamani hati hiyo kuwa kielelezo alisema kuwa hakuwa na tatizo.
Kwa kuwa upande wa mashtaka haukuwa na pingamizi, mahakama iliipokea hati hiyo, yaani nakala kivuli ya Ilani ya Kwanza (taarifa ya awali ya tukio la kifo cha Aneth) na kuwa kielelezo cha tatu cha upande wa utetezi (deffence exhibit 3 - DE3).
Hata hivyo jana shahidi wa 24 Sajenti Obadia aliwasilisha Ilani ya Kwanza nyingine ambayo alisema ndio nakala halisi pia ilipokewa na kuwa kielelezo cha 17 cha upande wa mashtaka (PE17).
Katika ushahidi wake jana akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi Paul Kimweri, amesema kuwa mwaka 2016 wakati tukio la mauaji ya Aneth linatokea alikuwa akifanya kazi Polisi makao makuu Dar es Salaam, kitengo cha kumbukumbu ya makosa ya jinai dhidi ya binadamu.
Majukumu yake yalikuwa ni kupokea taarifa zote za maosa ya jinai kutoka mikoa maalumu ya Kipolisi Dar es Salaam, yaani Kinondoni, Ilala na Temeke, kuzichambua na kuzitenganisha kulingana na aina ya makosa, na kuzitunza kuhakikisha kuwa hizo kumbukumbu zinakuwa salama.
Amezichanganua taarifa hizo alizokuwa anazipokea, alizitaja kuwa ni pamoja na taarifa za makosa yanayofunguliwa katika vituo vya Polisi ambayo alisema kuwa wanayaita IR
Nyingine amesema ni makosa yanayotolewa na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO) ambayo wanayaita SCR yaani Serious Crime Report (taarifa ya makosa makubwa); FCR (first crime report - Ilani ya kwanza), progressive report (maendeleo ya kesi) na Final report (taarifa ya mwisho).
Amefafanua kuwa Ilani ya Kwanza (FCR) ni fomu maalumu ambayo inajazwa kituoni mara tu tukio linapotokea na kutumwa kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kupitia kwa RCO.
Amefafanua zaidi kuwa fomu hiyo hujazwa na askari wa mpelelezi wa zamu wa siku husika na husainiwa na Mkaguzi wa zamu wa siku husika.
Kwa mujibu wa ushahidi wake, Mei 30, 2016 akiwa ofisini akiendelea na majukumu mengine alipokea nyaraka kutoka mkoa wa Temeke za kesi za jinai za aina tofauti miongoni mwake zikiwemo za makosa ya kijinai ya mauaji zikiwemo Ilani ya Kwanza tatu za mauaji.
Amezitaja Ilani hizo kuwa ya kwanza ilihusu tukio la mauaji ya mlinzi wa ghala aliyenyongwa maeneo ya Keko, ya pili ilikuwa ya mauaji ya vibaka watatu waliouliwa na wananchi wenye hasira kali maeneo ya Keko na ya tatu ilikuwa inahusu mauaji ya Aneth Elisaria Msuya lililotokea maeneo ya Kigamboni.
Baada ya kupokea ilani hizo aliziweka kwenye jalada la makosa ya mauaji lililoko ofisini, akazitunza ili kuhakikisha kwamba zinakuwa salama kabla ya kumpelekea DCI au afisa yeyote akizihitaji na baada ya kuifanyia kazi huichukua na kuirudisha tena kwenye jalada husika.
Akiielezea Ilani ya Kwanza ya mauaji ya Aneth amesema kwamba ilikuwa na namba ya IR iliyosomeka KGB/ IR/ 2849/2016 na namba ya RCO yaani SCR ni DSM/TMK/SCR/262/2016.
Baada ya ilani hiyo kupokewa na kusajiliwa kuwa kielelezo cha 17 cha upande wa mashtaka (PE17) shahidi huyo aliisoma taarifa zilizomo katika ilani hiyo:
Pamoja na mambo mengine inaeleza kuwa iliripotiwa na Richard. Mwaisemba Mei 26, 2016 saa 12 asubuhi na inaeleza kuwa Aneth Elisaria Msuya alichinjwa shingoni na kukatwa koromeo kwa kitu chenye ncha kali nyumbani kwake Kigamboni Kibada Mei 26, 2016 usiku.
Pia inaeleza kuwa hakuna mtuhumiwa aliyekuwa amekamatwa wala kujulikana.
Kisha Wakili Kimweri alimpa vielelezo hivyo vyote viwili yaani kile cha k kisha akamuongoza kutoa ufafanuzi wa maelezo yaliyomo katika kila kielelezo.
Akilinganisha vielelezo hivyo viwili shahidi huyo ameanza kwa kubainisha zile alizoziona kama kasoro katika kielelezo DE3, kwanza akisema kuwa alisema kuwa ni nakala kivuli lakini kielelezo PE17 ni nakala halisi.
Pia amesema kuwa nakala hizo hazifanani katika taarifa zilizomo, akibainisha kuwa kielelezo PE17 namba ya SCR imeandikwa chini ya neno confidential (siri) ambako ndiko inapaswa iandikwe na kwamba inasomeka DSM/TMK/SCR/262/2016.
Lakini akasema kwenye DE3 SCR imeandikwa chini ya maneno copied to DCI, halafu na kwamba inasomeka DSM/TEMEKE/SCR/262/2016.
"Kwa mfumo wa utendaji wa kipolisi tunatumia kufupisha maneno mfano Temeke tunaandika TMK, hatuandiki neno lote kamili," amesema shahidi huyo.
Alisema kuwa kwenye kielelezo DE3 mbele ya neno to DCI pameandikwa maneno bado sijapata kumbukumbu lakini kwenye PE17 mbele ya neno to DCI hakuna kilichojazwa.
Shahidi huyo amesema kuwa katika utendaji wa Polisi, aliyeijaza kielelezo DE3 kama alikuwa anamaanisha kumbukumbu namba haiandikwi kwenye fomu hiyo.
Badala yake amesema kuwa kumbukumbu namba inaandikwa kwenye fomu ya maendeleo ya kesi ambayo ni fomu maalumu, yaani Polisi Fomu namba 5 (PF5).
"Sehemu ya mwisho ya iliyoandikwa maneno hearing date kwenye kielelezo DE3 imeandikwa tarehe 11/7/2016 na kwenye PE17 pako wazi hakuna tarehe iliyojazwa kwa kuwa hii ni ilani ya Kwanza ambayo inajazwa mara tu tukio linapotokea.
"Kwa hiyo haiwezekani tukio limetokea siku hiyohiyo na upelelezi haujafanyika halafu kesi ikapewa tarehe ya kusikilizwa."
Kuhusu eneo lililoandikwa accused (jina la mshtakiwa amesema kuwa kwenye PE17 pamejazwa maneno "bado hajapatikana" na kwenye DE3 imejazwa Getruda Peniel Mfuru. Getruda alikuwa mfanyakazi wa ndani wa marehemu Aneth.
Kuhusu eneo lililoandikwa "arrest" (kama amekamatwa), amesema kuwa katika kielelezo DE3 imejazwa YES na kwenye PE17 imejazwa NO.
"Kielelezo DE3 kwenye eneo la particulars (maelezo) inaonesha kuwa marehemu aliuliwa kwa kuchinjwa shingoni na kukatwa koromeo lake na kitu chenye ncha kali na watu wasiofahamika, kwenye accused name limejazwa jina Geteuda Peniel Mfuru," amesema na kusisitiza:
"Kwa kuwa hii kesi( ya Aneth) ilikuwa na maslahi kwa jamii huu Waraka (Ilani ya Kwanza) naikumbuka maana ilikuwa inatembea sana ndani ya ofisi kwa mabosi zangu.Kulingana na taarifa hizo zilizomo ndani ya nyaraka hizo, nakala kivuli ya DE3 haikuzalishwa kutoka kielelezo PE17."
Hivyo amesema kuwa kati ya hizo nyaraka mbili aliyoipokea yeye na kuitunza ni PE17 na kwamba ndio nyaraka halisi ya Polisi na ni siri ambayo inatakiwa itembee ndani ya Jeshi la Polisi tu.
Baada ya kumaliza maelezo hayo ndipo Wakili Kibatala akaanza kumhoji maswali ya dodoso na sehemu ya mahojiano hayo ilikuwa kama ifuatavyo:
Kibatala: Kwa hisani yako Mheshimiwa jaji kabla hatujaendelea naomba mahakama yako itusomee mwenendo wa Machi Mosi 2022 shahidi wa nne Richard Mwaisemba ambaye ndo alitoa kielelezo cha tatu cha upande wa utetezi (DE3).
Kwa maombi hayo Jaji Edwin Kakolaki anayesikiliza kesi hiyo akasoma sehemu hiyo kisha Wakili Kibatala akaanza kumhoji shahidi huyo.
Kibatala: Shahidi, wewe ni askari makini ambaye unafahamu majukumu yako na sheria?
Shahidi: Nafahamu majukumu, sheria siwezi kusema nafahamu sana.
Kibatala: Unaifahamu Katiba ya Nchi hii, una uhalali wewe kumuita mtu aliyeuawa kumuita kibaka?
Shahidi: Mheshimiwa Jaji ndio maana nimeomba msamaha kwamba ninatumia maneno tuliyozoea.
Kibatala: Kwa maneno yako nimekusikia ukisema waliouawa ni vibaka, ni sawa?
Shahidi: Kwa mujibu wa nyaraka nilizozipokea.
Kibatala: Kwa hiyo Jeshi la Polisi au mwandishi wa Ilani ya kwanza ana mamlaka ya kumuita mtu aliyeuawa kuwa mwizi?
Shahidi: Kama nyaraka zimeandikwa hivyo, lakini pia Mheshimiwa Jaji mimi sijaja hapa kuwakilisha Jeshi la Polisi bali kama askari.
Kibatala: Wale waliiba nini?
Shahidi: Nyaraka hazikusema.
Kibatala: Shahidi hebu tusaidie majina ya wale waliouawa?
Shahidi: Siwafahamu/ siwakumbuki maana ni muda mrefu.
Kibatala: Kwani Aneth (tukio) ilikuwa ni muda mfupi mpaka umemkumbuka?
Shahidi: Kama nilivyosema huu waraka ulikuwa inatembea sana ofisi.
Kibatala: Cheo chako ni nini vile?
Shahidi: Sajenti.
Kibatala: Ni cha ngapi kutoka chini?
Shahidi: Cha tatu.
Kibatala: Wewe (sajenti) na SSP nani mkubwa?
Shahidi: SSP
Kibatala: Unafahamu kwamba kielelezo DE3 kilitolewa na SSP Richard Mwaisemba bila pingamizi?
Shahidi: Sifahamu.
Kibatala: Nyaraka zote DE3 na PE17 ulizijaza wewe? Maana naona umezitolea maoni meengi?
Shahidi: Sikujaza mimi.
Kibatala:Unafahamu kuwa Mwaisemba ndiye alikuwa OC-CID (Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya) wa eneo lilikotokea tukio?
Shahidi: Ndio nafahamu.
Kibatala: Unafahamu utaratibu wa kuripoti makosa makubwa umejengwa kwenye PGO (Mwongozo wa Utendaji wa Jeshi la Polisi) 311?
Shahidi: Sikumbuki.
Kibatala: Utaratibu wa kupokea taarifa za makosa makubwa ukoje? zinaletwa hivi hivi tu hakuna mahali pa kusaini?
Shahidi: Hakuna mahala pa kusaini.
Kibatala: Kwa hiyo tukitaka kufahamu Ilani ya Kwanza imeletwa tarehe fulani namna ya kujua ni kutegemea ushahidi kama wako huu tu?
Shahidi: Yes
Kibatala: Na kama ikipotea sasa tunaitafuta vipi?
Shahidi: Haiwezi kupotea kwanza ni confidencial
Kibatala: Kwa hiyo ikiwa confidencial haiwezi kupotea?
Shahidi: Hapana, sijasema hivyo, inategemea na umakini wa mtunzaji
Kibatala: Hata unapompelekea DCI pia unampelekea tu hivi au kuna hati ya kusaini?
Shahidi: Hakuna hati akihitaji tu nampelekea.
Kibatala: Kuna mahali ambapo kwenye nyaraka hiyo (PE17) kuna mhuri wa DCI kuipokea?
Shahidi: Haupo.
Kibatala: Sasa shahidi hebu nenda kwenye sehemu iliyoandikwa commission of offence (kutendeka kwa kosa) tarehe iliyoandikwa hapo ni tarehe ngapi?
Shahidi: Tarehe 26/5/2016
Kibatala: Muda gani?
Shahidi: Usiku
Kibatala: Eneo gani?
Shahidi: Kibada Kigamboni
Kibatala: Kwa jinsi fomu hiyo ilivyo nini kilitokea muda huo?
Shahidi: Kwa mujibu wa document hii ni muda ambao tukio lilitokea.
Kibatala: Unafahamu hii PE17 mmeileta ili kuonesha kwamba kielelezo DE3 kina mapungufu ndio maana Umeulizwa maswali mengi ya kuvilinganisha?
Shahidi: Hapana, sifahamu.
Kibatala: Unafahamu kwamba kwa mujibu kielelezo cha upande wa mashtaka PE1 (taarifa ya kitabu ya uchunguzi wa sababu za kifo) mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi tarehe 26/5/2016 saa nne asubuhi?
Shahidi: Sifahamu.
Kibatala: Kwa mujibu wa PE 17 (Ilani ya Kwanza aliyoiwasilisha yeye shahidi huyo) marehemu ameuawa tarehe 26 usiku wewe kama askari Polisi makini, katika hali ya kawaida inawezekana mtu ambaye amefanyiwa uchunguzi wa chanzo cha kifo tarehe 26 asubuhi akauawa tarehe 26 usiku?
Shahidi: Siwezi kuelezea hiyo.
Kibatala: Sasa Shahidi, nakuoneaha kielelezo DE3 (Ilani hiyo ya kwanza, kielelezo cha upande wa mashtaka ambayo pia ilitolewa na shahidi wa upande wa mashtaka Mkuu wa upelelelezi Wilaya ya Kigamboni) kwanza msomee Jaji eneo la muda wa kutendeka uhalifu.
Shahidi: Tarehe 26/5/2016
Kibatala: Muda gani?
Shahidi: 0610 saa 12 Asubuhi
Kibatala: Unafahamu kuwa muda huo ndio unaendana na ushahidi mwingine kuwa ndio mwili uligundulika?
Shahidi: Sifahamu.
Kibatala: Sasa shahidi nenda sehemu iliyoandikwa date of hearing (tarehe ya usikilizwaji), ambayo wewe umesema ni moja ya mambo unaona hayako sawa, sasa hiyo tarehe 11/7/2016 imewekwa mbele ya maneno tarehe ya usikilizwaji au sehemu ya tarehe ya kuandaa huo waraka?
Shahidi: Kwa mujibu wa waraka huu iko chini ambako imeandikwa date of hearing?
Kibatala: Bado unasisitiza kuwa hiyo (1/7/2016) ni tarehe ya mtu kupelekwa mahakamani?
Shahidi: Ndio.
Kibatala: Sasa mwambie Mheshimiwa Jaji kielelezo PE17 tarehe ya kujazwa fomu imewekwa wapi?
Shahidi: Hii fomu hakuna kipengele kwamba mjazaji anaijaza tarehe ya kujaza tukio.
Kibatala: Kwa hiyo hakuna mahali pa tarehe ya mjazaji?
Shahidi: Ipo.
Kibatala: Imeandikwa ameijaza tarehe ngapi?
Shahidi: Hii fomu imeeleza maelezo ya jumla ya tarehe ya tukio lakini si kumwelezea mjazaji kuwa alijaza tarehe ngapi.
Kibatala: Angalia nyaraka zote mbili DE3 na PE17, halafu mwambie Jaji IR namba zinafanana au hazifanani?
Shahidi: Zinafanana
Kibatala: Msomee Jaji
Shahidi: Kwenye DE3 ni KGB/IR/2849/2016 na kwenye PE17 ni KGB/IR/2849/2016.
Kibatala: Twende kwenye iliyoandikwa "method" (namna ya tukio au uhalifu ulivyotendeka), ni kweli vielelezo vyote vinaeleza marehemu aliuawa kwa kuchinjwa na kukatwa koromeo kwa kitu chenye ncha kali, zinafanana (DE3 na PE17) au zinatofautiana?
Shahidi: Zote zinafanana.
Kibatala: Sasa nenda sehemu iliyoandikwa maneno brief particulars (maelezo mafupi) mpaka mahali ambako mwili wa marehemu ulikutwa zinafanana?
Shahidi: Si kweli.
Kibatala: Kwenye DE3 Ulikutqa wapi?
Shahidi: chumba cha watoto
Kibatala: Kwenye PE17?
Shahidi: Chumba cha watoto.
Kibatala: Kwenye umri (wa marehemu) nyaraka zote zinafanana au hazifanani?
Shahidi: Zinafanana.
Kibatala: Kwamba marehemu alikuwa mfanyakazi Wizara ya Fedha zinafanana?
Shahidi: Zinafanana.
Kibatala: Kwamba mwili ulikutwa sakafuni damu.ikiwa imeganda zinafanana?
Shahidi: Zinafanana
Kibatala: Kwenye ile SCR (namba za Mkuu wa Upelelezi Mkoa -RCO) namba zinafanana au hazifanani ukitoa TMK na Temeke vingine vyote vinafanana, ni kweli au si kweli?
Shahidi: Kweli vinafanana.
Kibatalà: Sasa nenda DE3 sehemu iliyoandikwa complainant (mlalamikaji ni nani majina na cheo chake?
Shahidi: Linasomeka jina la Richard D. SP (SP ni Mrakibu wa Polisi, yaani cheo alichokuwa nacho wakati huo shahidi Mwaisemba)
Kibatala: Na kwenye PE 17?
Shahidi; Linasomeka Richard Mwaisemba SP cheo chake.
Kibatala: Nenda mahali yaliyoandikwa maneno 'discovered by whom' kwenye DE3 ni nani?
Shahidi: Richard D. SP
Kibatala: PE17?
Shahidi: Imeandikwa Richard Mwaisemba.
Kibatala: Kwenye DE3 nenda eneo la afisa wa Polisi anayepokea ripoti ni nani?
Shahidi: Ni mpelelezi
Kibatala: Sasa nenda PW17 hayo majina ni sawa na yale ya kwenye DE3?
Shahidi: Ndio
Kibatala: Kwa mujibu wa nyaraka zote mbili ofisa aliyetoa ripoti kwenye kielelezo PE17 anatoka wapi?
Shahidi: Kigamboni
Kibatala: Kuna tofauti na afisa aliyetoa ripoti mwenye DE3?
Shahidi: Kwa mujibu wa fomu hii inaonesha anatokea Kigamboni
Kibatala: Wewe umejitambulisha unatoka Kigamboni?
Shahidi: Hapana.
Kibatala: Fomu zote kuna mahala kuna majina yako?
Shahidi: Hakuna mahala kuna majina yangu.
Kibatala: IR namba huwa inapatikana kwenye jalada la kesi, ni kweli?
Shahidi: Ni kweli
Kibatala: Na huyu anayejaza Ilani ya Kwanza (FCR) anaipata kwenye jalada la kesi, ni sahihi?
Shahidi: Hapana ni kwenye kitabu cha kesi, lakini si lazima kwenye tu kama kesi imefunguliwa hata kwenye jalada la kesi.
Kibatala: Nani mtunzaji wa kitabu cha ripoti za matukio kati ya Wakili na Polisi?
Shahidi: Ni Polisi.
Kibatala: Aliye sehemu gani?
Shahidi: Charge room (chumba cha mashtaka)
Kibatala: Anayejaza fomu PF4 (FCR - Ilani ya Kwanza) anapata wapi SCR namba (namba ya RCO - Mkuu wa Upelelezi Mkoa)?
Shahidi: Anatoa RCO
Kibatala: Sasa wewe ni RCO wa Tekeme 2016? maana umesema huwa hamuandiki kwa kirefu.
Shahidi: Hapana sikuwa RCO
Kibatala: Katika DE3 mshtakiwa anaitwa nani?
Shahidi: Anaitwa Getruda Peniel Mfuru.
Kibatala: Kazi yake?
Shahidi: Msichana wa kazi
Kibatala: Mwambie Jaji alikamatwa tarehe ngapi (kwa mujibu wa kielelezo DE3)? Au tarehe iliyoandikwa hapo 27/5/2016 ni ya Nini?
Shahidi: Inasema ndio tarehe aliyokamatwa.
Kibatala: Progressive report kazi yake nini?
Shahidi: Maendeleo ya kesi inampa taarifa DCI (Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai) kesi inavyoendelea mahakamani.
Kibatala: Kwa mujibu wa PGO (Mwongozo wa Utendaji wa Jeshi la Polisi) namba 170 ndio inaitwa first progressive report in case of serious crime?
Shahidi: Hapana, hapa hakuna hiyo hapa kuna final
Kibatala: Soma hii PGO170
Shahidi: Anasoma
Kibatala: Kuna neno final hapo?
Shahidi: Hapa siwezi kujua.
Kibatala: Kwenye hiyo PGO Kuna fom imekuwa imeainishwa kama final progressive report?
Shahidi: Hapa hakuna.
Kibatala: Ni kweli PGO ndio Mwongozo Mkuu wa Matendo ya Polisi?
Shahidi: Ni mojawapo tu.
Kibatala: Nyingine ni zipi?
Shahidi: Zipo nyingi tu.
Kibatala: Nitajie tatu tu
Shshidi: Nidhamu...
Kibatala: Nidhamu haiko kwenye PGO? maana inazungumzia mpaka fimbo filimbi, viatu na hata namna ya kupiga pasi.
Shahidi: Ipo (nidhamu kwenye PGO).
Kibatala: Ni kweli kwamba mchakato wote wa hizo ripoti unaongozwa na PGO 311 tangu ripoti inapopokelewa kituoni mpaka.inapofika mahakamani?
Shahidi: Sikumbuki.
Kibatala: Nikikuonesha PGO?
Shahidi: Nikisoma labda naweza kujifunza
Kibatala: Soma hii PGO311 (anamkabidhi shahidi Kitabu hicho akimuonesha mahali pa kusoma).
Shahidi: Siwezi kukumbuka.
Kibatala: Ahaa , hata baada ya kuonesha PGO na kusoma bado huwezi kukumbuka tu, sasa ngoja nikuulize hivi, Unafahamu kwamba kwa POG 311(4)(a) FCR (Ilani ya Kwanza inapelekwa chargeroom (chumba cha mashtaka)?
Shahidi: Anasoma PGO hiyo ambayo inaeleza kuwa afisa katika chumba cha mashtaka ndio anawajibika kupokea na kuandika (kwenye kitabu cha kila taarifa inayopokewa kwenye vituo vya Polisi na kumpelekea afisa mhusika kwa hatua za haraka.
Kibatala: Baada ya kusoma hapo sasa ni hiyohiyo (PGO 311 inayohusika na Ilani ya Kwanza) au?
Shahidi: Mheshimiwa Wakili nimesema siwezi kukumbuka.
Kibatala: Hata baada ya kusoma bado huwezi kukumbuka?
Shahidi: Siwezi kukumbuka
Kibatala: Sawa mimi nauliza maswali tu wenye kupima na kuamua ni Wengine (Mahakama/Jaji).
Kibatala: Ni kweli kwa PGO 311(10) Ripoti kwenda kwa DCI inapitia kwa OC-CID (Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya) kwenda kwa RCO (Mkuu wa Upelelezi Mkoa) kisha kwa DCI ?
Shahidi: Najua si kwa PGO hiyo bali kwa taratibu za Polisi.
Kibatala: Ambazo zikoje inaanzia wapi?
Shahidi: Kwa OC- CID , RCO kisha kwa DCI.
Kibatala: Kwa hiyo ni kama nilivyosema.
Kibatala: Kwa mujibu wa PGO 311 (10) (a) OC-CID linapotokea tukio katika eneo lake anapaswa kwenda eneo la tukio?
Shahidi: Ndio, anapaswa kwenda yeye au subordinate (ofisa mdogo kwa cheo) wake.
Kesi hiyo itaendelea Jumatatu.