Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KESI YA MJANE WA BILIONEA MSUYA: Mawakili walivyokabana kwa hoja, Serikali kuwaita mashahidi wengine

Wakili Peter Kibatala (kushoto) akiteta jambo na mjane wa Bilionea Msuya, Miriam Steven Mrita (wa pili kushoto) katika chumba cha Mahakama Kuu. Picha na Sunday George.

Muktasari:

  • Ulikuwa mchuano mkali wa hoja katika kesi ya mauaji inayomkabili mjane wa Bilionea Msuya baada ya  Serikali kuomba kumuita tena shahidi aliyekwishatoa ushahidi wake, kumuongeza shahidi mwingine na kuwasilisha taarifa nyingine ya awali ya tukio la mauaji hayo.

Dar es Salaam. Mawakili wa pande zote katika kesi ya mauaji ya Aneth Elisaria Msuya wamelumbana vikali kwa hoja baada ya kuwasilisha maombi ya kumuita tena shahidi aliyekwishakutoa ushahidi wake na kumuongeza shahidi mwingine ambaye hakuwepo kwenye orodha ya mashahidi wake.

Sambamba na maombi hayo pia Serikali kumuita shahidi kwa mara ya pili na kuongeza shahidi mwingine, na kuwasilisha nakala halisi ya taarifa ya awali ya uhalifu (first crime report) kuhusiana na tukio la mauaji hayo.

Vilevile Serikali imeamua kuachana na shahidi wake mwingine aliyekuwa kwenye orodha ya mashahidi wake waliokuwa wameshatajwa mahakamani.

Maombi hayo yemepingwa vikali na mawakili wa utetezi na hivyo kuibua malumbano makali ya hoja kabla ya Mahakama kutoa uamuzi wake.

Serikali imetoa maombi hayo jana Jumatano, Septemba 6, 2023, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi wa shahidi wa 24 upande wa mashtaka, Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Kagera, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Jumanne Malangahe.

Washtakiwa katika kesi hiyo namba 103 /2018 inayosikilizwa na Jaji Edwin Kakalaki ni Miriam Steven Mrita ambaye ni mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara tajiri maarufu wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya; na mwenzake Revocatus Everist Muyella maarufu Ray.

Aneth alikuwa mdogo wa Bilionea Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Agosti 7, 2013.

Yeye Aneth aliuawa Mei 26, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam, na mwili wake ulikutwa ndani ya nyumba yake.

Leo Mahakama Kanda ya Dar es Salaam ilitarajia kuendelea kupokea ushahidi wa shahidi wa 24, lakini Serikali imesema kuwa imeamua kuachana na shahidi huyo aliyekuwa ameandaliwa ambaye tayari alikuwa mahakamani hapo.

Badala yake ndipo ikawasilisha maombi ya kumuita kwa mara ya pili shahidi wa nane, na kumuongeza shahidi mwingine, huku iliomba kesi hiyo iahirishwe mpaka keshokutwa Ijumaa, kutokana na uamuzi wa kuachana na shahidi huyo aliyekuwa ameandaliwa.

Mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi Yasinta Peter, ameieleza Mahakama kuwa wameamua kuachana na shahidi huyo kwa kuwa ushahidi wake unafafana na ushahidi wa shahidi mwingine aliyetangulia.

"Mheshimiwa jaji shauri hili limepangwa kwa ajili ya kundelea na usikilizwaji. Tutakuwa na shahidi SSP Jumanne Malangahe.", amesema mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Yasinta Peter, baada ya utambulisho na kuongeza:

"Lakini tunatoa taarifa kwamba ushahidi wake unafanana na ushahidi wa shahidi aliyepita.'

Baada ya taarifa hiyo ndipo Wakili Yasinta akawasilisha maombi ya kumuita kwa mara ya pili shahidi wake wa nane,  na kisha akatoa taarifa ya nia ya kumuongeza shahidi mwingine katika orodha ya mashahidi wake.

"Hata hivyo tunaomba kumuita tena PW8 (shahidi wa nane upande wa mashtaka), Fredrick Nyudike, chini kifungu cha 147(4) Sheria ya Ushahidi", amesema Wakili Yasinta na kuongeza:

"Pia tumeandaa notisi ya nyongeza ya shahidi, F832 DC Sajent Obadia na tumeshawapatia wenzetu (upande wa utetezi) nakala. Tumeiwasilisha mahakamani) chini ya kifungu cha 289(1-4) Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Wakili Yasinta amebainisha kuwa nia ya kumuita tena shahidi huyo ni kwa sababu  ndiye aliyeandaa taarifa ya awali ya uhalifu (first crime report) kuhusiana na mauaji hayo na kwamba   kwenye ushahidi wake uliopokewa na Mahakama aliiongelea taarifa hiyo.

Pia amesema kuwa shahidi Obadia wanayekusudia kumuongeza ndiye aliyekuwa mtunza vielelezo na ndiye aliyepokea taarifa hiyo ya awali ya uhalifu huo.

Taarifa hiyo ilishapokewa mahakamani kama Kielelezo cha Tatu cha upande wa utetezi (ED3), uliotolewa na kupokewa mahakamani na shahidi wa nne wa upande wa mashtaka baada ya kuombwa kufanya hivyo na mawakili wa utetezi wakati wakimhoji maswali ya dodoso.

"Kutokana na kwamba shahidi tuliyemwandaa hatuwezi kuendelea naye tunaiomba Mahakama iahirishe shauri hili mpaka kesho kutwa chini ya kifungu cha 284(1) CPA", amesema Yasinta.

Hata hivyo wakili wa utetezi Peter Kibatala amepinga maombi hayo ya Serikali ya kumuita tena shahidi wa nane, taarifa ya kuongeza shahidi mwingine na maombi ya ahirisho la kesi.

Kuhusu maombi ya kumuita tena shahidi wa nane, Wakili Kibatala amesema kuwa anayapinga kwa kuwa hayana msingi, akibainisha kuwa shahidi wakati anatoa ushahidi wake awali, taarifa hiyo ya awali ya uhalifu ilishapokewa mahakamani

"Sasa wanataka kuleta first crime report ya kwao ili kuja kukinzanisha na ya kwetu na walikuwa wanafahamu. Sasa nini msingi wa kumuita tena?",  amehoji wakili Kibatala na kuongeza:

"Na kwa dhahiri ombi la kumuita tena shahidi wa nane limetokana maswali ya dodoso kwa David Mhanaya (shahidi wa 22) wanataka kuja kuziba mapengo yake."


Wakili Kibatala amesema kuwa pamoja na kwamba kifungu 147 kinaipa Mahakama uhiyari kutu lakini lazima iyatumie mamlaka yake hayo kwa taratibu za kimahakama na kwamba vinginevyo kesi zitakuwa haziishi kama kila shahidi akihojiwa maswali ya dodoso halafu upande wa mashtaka unawaita tena mashahidi waliopita.

"Mheshimiwa jaji toka uanze kikao cha usikilizwaji kesi hii tu wameshatoa notisi nadhani ya tano ikiwemo kuongeza shahidi wa ziada daktari, mahakama ikaruhusu.", Amesema na kuongeza:

"Mazingira yote hayo lazima yaangaliwe. Kwa hiyo tunapinga hatujaona msingi wowote (kumuita tena shahidi wa Nane)".

Akijibu maombi ya taarifa ya kuongeza shahidi mwingine, Wakili Kibatala ameikumbusha Mahakama kwamba Agosti 21 2023 upande wa mashtaka waliwasilisha notisi ya kumuongeza shahidi Dk Chande.

"Majuma mawili baadaye  wanaongeza shahidi mwingine kuja kupambana na maswali ya dodoso waliyomuuliza shahidi aliyepita) na wanaomba kuongeza document", amesema wakili Kibatala na kusisitiza:

"Wanamuita ili kujaliza maelezo ya shahidi wao kwamba hii (taarifa ya awali ya uhalifu) ni nakala kivuli. Kwa hiyo wanataka kuleta ya kwao halisi ili kuja kukinzana  na maswali ya dodoso) yetu."

Wakili Kibatala amesema kuwa kifungu hicho hakikutungwa kwa malengo kama hayo mheshimiwa jaji na akaiomba mahakama ikatae.

Kuhusu taarifa hiyo yenyewe, Wakili Kibatala ameipinga akisema kuwa ina kasoro akibainisha kuwa nakala yake waliyopewa haijawasilishwa mahakamani kwani haijasainiwa wala kugongwa mhuri wa mahakama.

Hivyo amesema kuwa namna yoyote ile mshtakiwa wa kwanza ambaye ndiye mteja wake hajapewa notisi ambayo imewasilishwa mahakamani.

Pia wakili Kibatala amepinga maelezo ya Wakili Yasinta kwamba watawapatia kesho nakala ya taarifa ya awali ya uhalifu wanayokusudia kuuwasilisha mahakamani kupitia kwa shahidi huyo wanayeomba kumuongeza.

Hata hivyo amewakumbusha upande wa mashtaka kuwa taarifa ya awali ya uhalifu iliyoko mahakamani ilitolewa na shahidi wao tangu mwaka jana 2022, baada ya wao upande wa utetezi kumuomba lakini anashangaa kuwa leo wanataka kuleta nyingine ili kukinzanisha na hiyo ya kwanza iliyoko mahamamani

"Kwa hiyo Mahakama inapotafsiri vifungu lazima pia izingatie kuwa haki inapaswa ionekane inatendeka vinginevyo tuna risk proceeings simply because (tunahatarisha mwenendo wa kesi Kwa sababu tu) kuna watu hawajafanya majukumu yao" amesema Kibatala.

Kuhusu hoja ya kuahirisha kesi mpaka Ijumaa, Wakili Kibatala amepinga akidai kuwa itakuwa ni muda mrefu huku akibainisha kuwa ikijumlishwa siku ambazo imekua iliahirishwa inafika wiki nzima (siku 7) kwa kikao hiki tu kilichoanza Agosti 14 mwaka huu.

"Kwa hiyo tunapinga kukubaliwa lakini hata kama wakikubaliwa leo basi angalau tuendelee kesho badala ya Ijumaa. Siyo kwamba sisi tuna kesi hii moja vinginevyo tarehe 13 (Septemba mwisho wa siku zilizopangwa kusikiliza kesi hiyo)  itatukuta hatujafanya chochote maana mara wamekosa shahidi mara hili." amelalamika Kibatala.

Kwa upande wake Wakili Nehemiah Nkoko anayemtetea mshtakiwa wa pili (Muyella) amesema anaunga mkono yote yaliyoelezwa na Wakili Kibatala.

Akijibu hoja za Wakili Kibatala Wakili Yasinta amesema kuwa kifungu cha Sheria walichokitumia kuomba kumuita tena shahidi wa nane hakiwakatazi kufanya hivyo.

Amesema kwamba  na kwamba madai kuwa shahidi huyo anaitwa ili kuziba mapengo yaliyotokana na ushahidi wa shahidi wa 22 hayana miguu ya kusimamia kwa sababu sheria Iko wazi na kwamba sababu zimesema wazi.

Pia amesema kuwa kielelezo hicho (taarifa ya awali ya uhalifu iliyokwishapokewa mahakamani hapo kwa kuombwa na upande wa utetezi) hakikuwa sehemu ya mwenendo wa hatua ya uhamishwaji kesi hiyo kutoka mahakama ya chini yaani Kisutu

Hivyo Wakili Yasinta amesema kwamba kwa hali hiyo upande wa mashtaka pia una haki kupata nafasi hiyo kuizungumzia zaidi.

"Mbali na kwamba si kielelezo cha committal kilitolewa na shahidi wa upande wa mashtaka shahidi wa nne. Aliulizwa kama anaitambua na kama ana tatizo kielelezo hicho kutolewa akasema hana tatizo." amesema Yasinta na kuongeza:

Ndio maana tunaona upande wa Jamhuri aletwe huyo shahidi aje sasa kwa ufafanuzi zaidi kwa maslahi ya haki.

Kuhusu hoja za Wakili Kibatala kupinga taarifa mara kwa mara zikiwemo za kuongeza shahidi, wakili Yasinta amesema kuwa Wakili Kibatala hajataja sheria yoyote waliyoikiuka kwa kufanya hivyo.

"Tunasisitiza sheria haikatazi ni kwa sababu ya nature (asili) ya kesi yenyewe", amesisitiza Wakili Yasinta.

Kuhusu suala la taarifa ya awali ya uhalifu (kuhusiana na mauaji hayo) amesema kwa kuwa wao utetezi ndio waliibua hoja hiyo (wakati wakimhoji shahidi wa 22) basi lazima na wao ufafanuzi utolewe ili mahakama ipate kupima.

Kuhusu madai ya Wakili Kibatala kuwa notisi waliyopewa haijawasilishwa mahakamani, Wakili Yasinta ameomba ruhusa kuwa amuoneshe waliyonayo wao kama haijasainiwa na hainana tarehe ya kuwasilishwa mahakamani na mhuri lakini Wakili Kibatala hakuwa tayari kumuangalia hiyo alisisitiza kuwa waliyopewa ina kasoro hizo.

Hivyo Wakili Yasinta ameomba wampatie nyingine lakini Wakili Kibatala akapinga kuwa hawezi kumpatia katika hatua ambayo yeye Wakili Yasinta anajibu pingamizi dhidi ya notisi hiyo na Jaji Kakolaki akakubaliana naye kuwa katika hatua hiyo hawezi kumpatia.

Wakili Yasinta ameomba Mahakama ione kuwa kwa waliyonayo imesainiwa kuonesha kuwa imewasilishwa mahakamani basi hata waliyowapatia upande wa utetezi haina tatizo


Kuhusu kuwapatia nakala ya kielelezo wanachokusudia kukiwasilisha mahakamani amesema kuwa kama upande wa utetezi wanaona kuwapatia nakala hiyo kesho halafu kesi iendelee kesho watakuwa wamechelewa basi kesi hiyo iahirishwe mpaka Jumatatu ili wapate muda wa kutosha kujiandaa.

Amesema kuwa hata hivyo kifungu 289(4) CPA kinataka waeleze msingi wa ushahidi wa shahidi husika tu na si lazima kuambatanisha na kielelezo hicho, japo wao waliona tu kuwa ni vema pia wawapatie nakala hiyo upande wa utetezi.

"Haki iko kwa pande zote kwa washtakiwa lakini pia kwa mtu ambaye amepoteza uhai ndio maana Jamhuri inapambana kuhakikisha kila kitu kimefanyika kiusahihi. Pamoja na kwamba kielelezo kikishatolewa tumeona aje tena ahojiwe", amesema Yasinta na kuongeza:

"Yeyote ambaye Jamhuri inaona anaweza kuisaidia mahakama wakati wowote inaweza kufanya hivyo ili kutenda haki."

Hata hivyo Wakili Kibatala amesisitiza kuwa wakati shahidi wa nane anatoa ushahidi kielelezo hicho cha 3 cha utetezi (taarifa ya awali ya tukio la uhalifu) Walikuwa nayo ilishaingia kwenye kumbukumbu ilishapokewa kupitia shahidi wa nne.

Amesema kuwa shahidi wa nane alitoa ushahidi mwaka 2022 na akahojiwa maswali ya dodoso na shahidi wa 22 pia mhojiwa  kwenye hii kielelezo hicho ED3 baada kilichotolewa na shahidi wa kwao wenyewe.

"Mheshimiwa Jaji kama unakumbuka madai ya Mhanaya (shahidi wa 22 alipohojiwa maswali ya dodoso) alihoji kwamba hii (kielelezo hicho yaani taarifa ya awali ya tukio la uhalifu) ni ya siri nyie mmeitoa wapi? Nikamwambia tumeiomba mahakamani wewe hujaona",amesema Kibatala na kuongeza.

"Ndio maana tunasema hakuna uhalali wa kisheria kumuita tena (shahidi wa nane) wakati nyaraka iko mahakamani."

Amesema kuwasilishwa kwa notisi hiyo kutaathiri maswali yao ya dodoso waliyomuuliza shahidi wa 22 David Mhanaya, na akamuelekeza Mahakama katika kifungu 289(3) kinasema katika kuamua maombi hayo ya Serikali Mahakama inapaswa kuangalia maana kuwasilisha maombi hayo.

Wakili Kibatala amesisitiza  kuwa mahamama inatakiwa kuangalia muktadha wa maombi hayo, kwamba ni lini upande wa mashtaka walijua kuwa shahidi wa nane anatakiwa kurudi kutoa ushahidi.

'Wenzetu (upande wa mashtaka) wamesema si takwa la kisheria kutupa nakala (ya hiyo taarifa wanayokusudia kuuwasilisha mahakamani)  bali kueleza tu msingi (wa ushahidi ulioko) na kwamba ili tu wasitu-shtukize. Hata kama Iko  hivyo lakini unapoamua kufanya jambo ambalo hulazimishwi ukilifanya mahakamani lazima upitie taratibu zote."amesisitiza Kibatala.


Uamuzi wa Mahakama

Hata hivyo mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote katika uamuzi wake imeikataa hoja zote za mapingamizi ya upande wa utetezi na ikakubaliana na maombi yote ya Serikali.

Hivyo imeiruhusu upande wa mashtaka kumuita tena shahidi wa nne kutoa ushahidi tena, Seeikaku kuongeza shahidi mwingine ambaye hakuwepo kwenye orodha ya mashahidi, kuwasilisha nakala halisi ya taarifa ya awali ya tukio la uhalifu ( mauaji ya Aneth) na imekubali maombi ya Serikali kuahirisha kesi hiyo mpaka kesho.

Alichokisema Jaji Kakolaki

Mahakama imealikwa na upande wa mashtaka kwa maombi manne

Mosi, Kuachana na shahidi wake SSP Jumanne Malangahe.

Mbili, kumuita tena shahidi wa nane Inspekta Fredrick Nyudike

Tatu, kuwasilisha taarifa halisi ya awali ya tukio la uhalifu.

Nne, kumuongeza shahidi Obadiah aliyekuwa mtunza vielelezo na aliyepokea taarifa hiyo.

Tano, ahirisho mpaka Ijumaa ili kuleta mashahidi wengine kupitia hayo maombi waliyoyafanya.

Mahakama imepitia maelezo ya pande zote na kuyapa uzito na kupitia sheria zinazohusu maombi haya.

Ombi la kwanza la upande wa mashtaka kuachana na shahidi halikupingwa, hivyo hilo limekubaliwa.

Ombi la pili, baada ya kupitia kumbukumbu za mahakama hakuna ubishi kuwa nakala kivuli ya taarifa hiyo ya awali ya tukio la uhalifu  ilitolewa na kupokewa kama kielelezo cha tatu cha upande wa utetezi na shahidi namba nne ambaye alikataa kufahamu kilichomo na pia hakuulizwa lolote.

Shahidi namba nane alipoitwa hakuulizwa swali lolote la dodoso kujua walichokuwa wanakitafuta upande wa utetezi mpaka alipoitwa shahidi wa 22 na kuulizwa maswali ya dodoso kuhusu kielelezo hicho (taarifa hiyo ya awali ya tukio la uhalifu)

Nakubaliana na Wakili Yasinta (Wakili wa Serikali ) kuwa kifungu cha 147 hakikatazi kuita tena shahidi. Lakini Mahakama inaona kuwa upande wa utetezi utakuwa na nafasi ya kumuuliza ili kujua walichotaka kukifahamu katika kielelezo hicho. Hivyo pingamizi hili linakataliwa.

Ombi la kuongeza shahidi; hakuna ubishi taarifa hiyo ( ya nia ya kumuongeza shahidi) iko katika maandishi, hivyo imekidhi kigezo cha kwanza. Pia  kuna majina ya shahidi, kielelezo kitakacholetwa na maelezo ya ushahidi unaotakiwa kuletwa kama kifungu cha 289(4) CPA kinavyoeleza.

Mahakama imechunguza notisi hii maelezo yaliyotolewa ambayo ni taarifa halisi ya awali ya tukio la uhalifu iliyotolewa kwa RCO Temeke na kwa DCI.

Kuhusu maelezo ya shahidi Obadia yameelezwa kuwa ndiye aliyepokea taarifa hiyo na mtunza nyaraka na kumbukumbu ofisi ya DCI.

Kuambatanisha kielelezo kwenye notisi si sharti la lazima lakini kwa ajili ya haki utetezi wapewe nakala hiyo mapema wajue maudhui yake na wajiandae mapema.

Hivyo upande wa mashtaka wawapatie upande wa utetezi nakala hiyo tarehe 7/9/2023 na wasipofanya hivyo hawataruhusiwa kutumia ushahidi huo.

Kuhusu hoja ya notisi kutokusainiwa mahakama imeona halina mashiko kwa kuwa Mahakama inaongozwa na nyaraka iliyowasilishwa mahakamani ambayo Imekidhi matakwa ya kisheria

Kuhusu kuahirishwa kwa minajili ya haki ni bora Mahakama hii ikaruhusu ahirisho ili kuwapa nafasi upande wa mashtaka ya kuandaa na kuleta mashahidi hivyo kwa. Kwa kesho haitawezekana. Hivyo ombi la kuahirishwa mpaka tarehe 8/9/2023 lonakubaliwa.

Hivyo Mahakama inaruhusu ombi la ahirisho na kwa sababu hiyo mahakama imeyakataa mapingamizi yote.