Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KESI YA MJANE WA BILIONEA MSUYA: Simulizi ya ‘House girl’ wa marehemu Aneth kuahidiwa Sh50 bilioni

Muktasari:

  • Shahidi wa 25 wa upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji inayomkabili mjane wa Bilionea Msuya na mwenzake, ameendelea na simulizi ya ushahidi wake, akieleza yale anayodai kuwa yalijiri kabla na baada ya mauaji ya aliyekuwa bosi wake, Aneth Msuya ambaye ni mdogo wa Bilionea Msuya.

Dar es Salaam. Katika mwendelezo wa simulizi ya ushahidi wake, aliyekuwa mfanyakazi wa kazi ndani (house girl) wa marehemu Aneth Elisaria Msuya, ameileza mahakama kuwa aliahidiwa kupewa Sh50 bilioni na watu waliomfuata wakieleza kuwa kuna kazi wanataka kuifanya kwa mwajiri wake huyo.

Mfanyakazi huyo Getruda Peniel Mfuru (38), ametaja dau hilo nono na la kusisimua wakati akitoa ushahidi wake kwa siku ya pili katika kesi ya mauaji ya mwajiri wake huyo, inayosikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki, Mahakama Kuu ya Dar es Salaam.

Maelezo hayo ni mwendelezo wa simulizi ya ushahidi wake aliouanza juzi Jumatano wiki hii, akielezea mfululizo wa matukio ya kabla na baada ya mauaji ya mwajiri wake huyo, katika kesi ya mauaji hayo namba 103 ya mwaka 2018.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Miriam Steven Mrita ambaye ni mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara tajiri maarufu wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya; na mwenzake Revocatus Everist Muyella, maarufu kama Ray.

Aneth ambaye aliuawa Mei 26, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam, alikuwa mdogo wa Bilionea Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro Agosti 7, 2013.

Awali Getruda katika ushahidi wake aliieleza mahakama kuwa Mei 15 2016 muda wa saa nne asubuhi, alitoka kwenda dukani akakutana na gari moja lenye rangi ya bluu ambalo lilishushwa kioo na akaitwa mwanamke, ambaye alikuwa na dereva ndani ya gari hilo.

Alieleza kuwa mwamnake huyo alimuuliza kama anapafahamu kwa Aneth, naye akakubali akawaonesha nyumba kwa na kidole na huku akiwaeleza kuwa Aneth ni dada yake, na kwamba anakaa naye katika nyumba hivyo.

Alidai kuwa mwanamke huyo alimweleza kuwa Aneth ni ndugu yake lakini hawajaonana siku nyingi, hata hivyo waliondoka na wakarudi tena Mei 18 na huyo mwanamke akampatia simu ndogo aina ya Nokia akamsisitiza kuwa ni kwa ajili ya mawasiliano baina yao na asithutubu kuwasiliana na mtu mwingine.

Mahakama ilielezwa kuwa Mei 23 2016, mama huyo alimpigia simu akamtaka waonane nje ya nyumba ya marehemu Aneth, naye akawafuata kwenye gari aina ya Range Rover yenye rangi ya Silver ambayo ndiyo walikuja nayo siku hiyo.

Sasa, katika mwendelezo wa ushahidi wake jana Alhamisi Agosti 14, 2023; na leo Ijumaa Septemba 15, 2023, shahidi huyo amesema kuwa alipolifika katika gari hilo, aliegemea kwenye dirisha baada ya kioo kushushwa na aliangalia ndani, ndipo akamuona yule mama amekaa kwenye kiti pembeni mwa dereva, huku kiti cha dereva akiwa amekaa yule mwanaume.

Kwenye viti vya nyuma walikuwa wamekaa vijana wanne wa kiume waliokuwa wamevaa soksi nyeusi kichwani ambazo walikuwa wamezitoboa macho na pua.

Mwilini walikuwa wamevaa makoti meusi. Mmojawapo wa hao vijana alikuwa amebeba briefcase nyeusi. Alilifungua ndani yake kulikuwa na pesa noti za Sh10, 000 zilizokuwa zimefungwa na (mipira) rubber band.

Yule mama alimwambia kuwa hizo pesa ni Sh50 bilioni na kwamba hivi karibuni zinakaribia kuwa za kwake (Getruda), endapo ataondoka pale nyumbani kwa Aneth na kumwachia afanye kazi yake, ambayo hata hivyo hakumweleza kazi hiyo ambayo alitaka kuifanya kwa Aneth.

Awali alipotamka kiwango hicho kikubwa kabisa cha pesa ilidhaniwa kuwa amekosea pangine alimaanisha Sh50 milioni.

Hii ni kwa sababu shahidi wa 22, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), David Paulo Mhanaya, katika Ushahidi wake aliieleza Mahakama kuwa shahidi huyo (Getruda wakati anamhoji alimweleza kuwa watu hao walimuonesha kiasi cha Sh50 milioni kwenye briefcase na kwamba ndizo walizoahidi kumpatia.

SSP Mhanaya ambaya Kwa sasa ni Mkuu wa Upelelelezi Mkoa wa Arusha (RCO), ndiye alikuwa kiongozi wa timu ya wapelelezi wa kesi hiyo iliyoundwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwan Athuman Msuya.

Hata hivyo Getruda alirudia kutamka kiwango hicho mara kwa mara na huku mwendesha mashtaka aliyekuwa akimwongozo, Wakili wa Serikali Mwandamizi Paul Kimweri naye akirejea kutaja kiwango hicho.

Akiendelea na ushahidi wake, alidai kuwa yule kijana aliyekuwa ameshika briefcase alishika bastola na kumwelekezea upande wa kifua, tukio ambalo lilimfanya kuingiwa na hofu kubwa. Wakati wote huo alikuwa amegemea kwenye dirisha la gari.

Yule mwanamke alimwambia kuwa ikifika tarehe 25/5/2016 awe amekwishaondoka pale nyumbani kwa Aneth kwa sababu kuna kazi anakwenda kuifanya.

Kisha alimpatia Sh20, 000 na akamwambia kuwa zile Sh50 bilioni atampatia akifika Arusha. Pia alimwambia hiyo simu atafute mahali popote atakapoiweka au atakapoitupa ili mtu mwingine asiione.

Mei 25, 2016 majira ya saa 5:30 asubuhi aliondoka kwa Aneth akaelekea Feri Kigamboni kuonana na rafiki yake Sabri Kombo. Wakati anaondoka alifunga mlango wa nyumba akaweka ufunguo chini ya zulia, mahali ambapo walikuwa wanaweka. Alifunga geti kubwa la fensi na kuondoka na ufunguo.

Kutoka nyumbani kwa Aneth kwenda Feri alipanda daladala kutoka Kibada mpaka Kigamboni Feri.

Alipanda pantoni kuelekea Magogoni. Akiwa ndani ya Pantoni alikumbuka kwamba aliambiwa na yule mama kwamba ile simu aina ya Nokia aliyopewa na yule Mama aitupe mahali ambapo mtu hatoiona, hivyo aliichukua akaitumbukiza kwenye maji.


Alipofika Magogoni alikutana na rafiki yake Sabri, akamuomba aende alale kwake Chanika na Sabri akamjibu akimuuliza kama dada yake Aneth hataleta shida lakini yeye Getruda akasema kuwa dada yake Aneth hana shida.

Kabla ya kuondoka kwenda kwa Sabri, alikumbuka kuwa alibeba funguo za geti la nyumbani kwa Aneth. Hivyo alimuomba Sabri amsindikize kurudisha zile funguo.

Alipanda tena Pantoni kurudi Kigamboni, walipovuka walichukua usafiri wa pikipiki kwenda kwa Aneth ambayo walipanda wote wawili yeye na Sabri.

Walipofika maeneo ya kwa Aneth walikutana na mwanafunzi wa shule ya msingi ambaye Getruda alimpatia zile funguo amsaidie kuzipeleka mahali pale walipokuwa wanachota maji nyumba ya jirani na mwanafunzi huyo alizipeleka na kisha yeye na Sabri walipanda pikipiki, wakaondoka.

Alidai kuwa aliamua kuondoka kwa Aneth kwa sababu yule mama aliyempatia simu ya Nokia alimwambia kuwa akimkuta mle ndani atamuwajibisha na yeye. Pia alidai kuwa aliondoka kutokana na vitisho alivyokuwa amekwishapewa kwa kunyooshewa bastola.

Alipofika kwa Sabri hakumwambia chochote kwa sababu yule mama alikwishaambiwa kuwa wakijua amemwambia mtu yeyote, watamfuatilia.

Siku hiyohiyo akiwa nyumbani kwa Sabri, mwajiri wake Aneth Msuya alimtumia ujumbe mfupi wa maneno kutumia simu yake ndogo aina ya Tecno akimtaka arudi nyumbani aondoke kwa usalama.

Hata hivyo baada ya kupata ujumbe huo, hakumjibu chochote, alinyamaza kimya.

Mei 26, 2023 majira ya saa 4 asubuhi alipigiwa simu na mdogo wake Neema kutoka Mererani Cairo kwa Bibi Msuya akamuuliza kama yuko nyumbani kwa Aneth yeye akajibu kuwa hapana, ndipo akamwambia kuwa Aneth ameuawa kinyama nyumbani kwake Kigamboni.

Hivyo alimweleza Sabri taarifa hizo kuwa dada yake amechinjwa kinyama na Sabri alimpa ushauri kwamba aende kituo cha Polisi lakini yeye Getruda alikataa kuwa hapana, anaogopa.

Badala yake alimuomba Sabri ampatie nauli ya kwenda nyumbani kwao Masama Sonu na Sabri alimtafutia na kumpatia nauli Sh50, 000.

Mei 28, 2016 asubuhi aliondoka kwa Sabri akaelekea kwao Masama Sonu.

Julai 20, 2016 akiwa nyumbani kwao Masama, alipigiwa simu na Bibi Msuya akamuuliza alikuwa wapi, naye akamjibu kuwa yuko nyumbani kwao Moshi.

Julai 23, 2016 jioni alipigiwa simu na askari aliyemtaka waongee hivyo akamuuliza kuwa alikuwa wapi na yeye akamjibu kuwa yuko nyumbani kwao Masama Sonu.

Huyo askari alikwenda akiwa na mwenzake wa kike wakiwa na gari dogo na walimchukua na kumpeleka katika kituo ha Polisi Moshi na alikwenda kulala na askari wa kike kuwa katika nyumba iliyokuwa karibu na kituo.

Julai 24, 2016 asubuhi walipanda gari kwenda Dar es Salaam yeye na wale askari  na walifika siku hiyo hiyo saa 11 jioni, na walipofika Ubungo walichukuliwa na gari dogo wakaelekea kituo cha Polisi Chang'ombe saa 12 jioni.


Usiku huo alikwenda kulala na yule askari wa kike nyumbani kwake karibu na kituo cha Polisi Chang'ombe.

Julai 25, 2016 waliamka kwa yule askari wa kike kurudi kituo Cha Polisi Chang'ombe, ambako Afande David alimchukua na kumpeleka kwenye chumba cha mahojiano kituoni hapo akamkabidhi kwa kwa yule askari wa kike amuandike maelezo kuhusiana na tukio la mauaji ya Aneth.

Kisha alikwenda kwa dada yake Gongo la Mboto na baadaye akaenda kwa Bibi yake Masama Sonu.

Agosti 6, 2016 alipigiwa simu na askari Polisi kutoka Chang'ombe Dar es Salaam ambaye alimwambia kuwa anamhitaji kituoni hapo. Hivyo alifanya jukumu la kupanda gari kwenda Gongolamboto kwa dada yake.

Agosti 7, 2016 huyo askari alimpigia tena simu, yeye akamweleza kuwa alikuwa Gongo la Mboto na askari wa kike akaenda kumchukua mpaka kituo cha   Polisi.

Kituoni hapo alikuta wanawake tisa ambao walikuwa wamepangwa pamoja na askari mmoja wa kiume, ambaye alimwambia kama anaweza kumtambua yule mama ambaye alikuwa anakwenda Kigamboni mara kwa mara naye akaijibu kuwa ndio anaweza.

Yule askari alimwambia awatazame nyuso zao wale wanawake kisha amshike bega. Aliwatizama nyuso zao kisha akamshika bega yule mama ambaye ambaye alikuwa amesimama nafasi nne kutoka kulia kwenda kushoto.

Agosti 28, 2016 akiwa bado kwa dada yake Gongo la Mboto, alipigiwa simu ya askari wa Chang'ombe ambaye alimuuliza mahali alikokuwa na alimweleza kuwa alikuwa Gongo la Mboto kwa dada yake, askari huyo alimtuma tena askari wa kike akaenda kumchukua na kwenda naye mpaka kituo cha Polisi ambacho hata hivyo hakukitaja.

Kituoni hapo alikuta wanaume tisa waliokuwa wamepangwa sehemu moja kwa mstari. Pia alikuwepo askari Polisi mmoja wa kiume, ambaye alimuuliza kama anamkumbuka yule mwanaume aliyekuwa anakwenda Kigamboni mara kwa mara na yule mama, naye akajibu kuwa ndio akimuona.

Yule askari alimwambia awatazame wanaume wale nyuso zao kisha amshike bega.

Baada ya kuwatizama nyuso zao alimtambua kuwa alikuwa ni mtu wa pili kutoka kulia.

Mahakamani aliwatambua watu hao kwa kuwagusa ambao ni mshtakiwa wa kwanza (Miriam) na wa pili Muyella.

Baada ya ushahidi wake huo, akiongozwa na mwendesha mashtaka alihojiwa na mawakili wa utetezi maswali mbalimbali kuhusiana na yale aliyoyaeleza katika ushahidi wake huo, akianza Wakili wa mshtakiwa wa kwanza (Miriam); Peter Kibatala.

Ifuatayo ni sehemu ya kwanza ya mahojiano hayo baina ya Wakili Kibatala na shahidi huyo:

Kibatala: Shahidi, umejitambulisha kama nani?

Shahidi: Nimejitambulisha kama Getruda Peniel Mfuru

Kibatala: Una kitambulisho chochote kuthibitisha kwamba wewe ndio Getruda Peniel Mfuru? 

Shahidi: Hapana.

Kibatala: Kwa hiyo hakuna namna ya kujiridhisha kwamba wewe ni Getruda Peniel Mfuru?

Shahidi: Kwa hapa sijakibeba.

Kibatala: Unafahamu kwamba watu huwa wanaigiza hata majina?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Ukitoa wewe kuna mtu mwingine ambaye aliona hilo gari lililokuja Kibada (nyumbani kwa marehemu Aneth)?

Shahidi: Watu walikuwa ni wengi waliokuwa wanapita barabarani

Kibatala: David (Paulo Mhanaya, shahidi wa 22, aliyekuwa mpelelezi mkuu wa kesi hiyo) alikuwepo siku hiyo?

Shahidi: Kwa kweli sikumbuki kama alikuwepo.

Kibatala: Nini kitakukumbusha kama alikuwepo?

Shahidi: Hakuna kitakacho nikumbusha.

Kibatala: Huyo David yuko hapa mahakamani?

Shahidi: Ndio yupo (anasema kisha anakwenda kumgusa)

Kibatala: Hilo gari aina ya Range Rover uliloliona (huko Kibada), umeoneshwa leo ulitambue na umuoneshe Mheshimiwa Jaji kwamba ni hili hapa?

Shahidi: Hapana, sikuoneshwa nilitambue nililitambua mwenyewe

Kibatala: Kwa hiyo jaji hana haki ya kulitambua.

Kibatala: Umetaja gari lingine la rangi ya bluu lililokuja tarehe 15/5/2016, umelionesha mahakamani Jaji na wazee wa baraza walitambue?

Shahidi: Sijamuonesha

Kibatala: Umeonesha hata picha zake tu gari yawezekana ni kubwa kulileta

Shahidi: Hapana.

Kibatala: Unasema mara ya kwanza walikuja tarehe ngapi?

Shahidi: tareh 15/5/2016.

Kibatala: Na Aneth alikuwa wapi?

Shahidi: Kazini

Kibatala: Ilikuwa siku gani?

Shahidi: Sikumbuki

Kibatala: Nikisema siku hiyo ilikuwa Jumapili ambayo watumishi hawaendi kazini una lolote la kusema?

Shahidi: Ndio nina la kusema siku hiyo dada yangu haendi kanisani

Kibatala: Kuna swali la kanisani hapa?

Shahidi: Samahani.

Kibatala: Uwe unasikiliza swali. Nimekuuliza kiwa nikikwambia siku hiyo ilikuwa Jumapili watumishi wa umma huwa hawaendi kazini una lipi la kusema?

Hata hivyo shashidi huyo alirudia jibu lake lilelile la awali.

Kibatala: Ulimwambia Jaji kuwa hicho kituo cha polisi ambacho ulikwenda kufanya utambuzi mara ya kwanza ni kituo gani?

Shahidi: Sijamwambia kwa sababu sikukijua.

Kibatala: Ulimfafanulia Jaji iwapo yule asakari wa kike aliyekufuata Gongo la Mboto kuwa si mmojawapo wa waliokufuata (kijijini kwao) Sonu Masama?

Shahidi:  Nimesema askari aliyenifuata ni mwanamke

Kibatala: Kwa hiyo huo ufafanuzi hukuutoa? Mimi nakuuliza kwa sababu magwaride ya utambuzi yana utaratibu wake

Kibatala: Ulimfafanulia iwapo yule Afisa aliyekufuata Gongo la Mboto aliondoka eneo la gwaride?

Shahidi: Sikujua kwa sababu aliyenifuata Gongolamboto sio aliyekuwepo kwenye gwaride

Kibatala: Huo ufafanuzi umeutoa?

Shahidi: Ndio niliufafanua vizuri kabisa

Kibatala: Ulimfafanulia Jaji kuwa katika wale kina mama (walioshiriki katika gwaride la utambuzi) hakuna yeyote ambaye alikuwa na pingu au alama yoyote inayoweza kumtofautisha na wengine?

Shahidi: Sikufafanua sababu sikuulizwa.

Kibatala:  Ulimfafanulia Jaji kuwa wale kina mama wote walikuwa wanafanana maumbo na rangi?

Shahidi: Sijamwabia kwa sababu sikuulizwa.

Kibatala: Ulimwambia Jaji kuwa walivaa mavazi yanayofanana?

Shahidi: Sijamwambia sababu sikuulizwa.

Kibatala: Ulimwambia Jaji mwanga pale eneo la gwaride la utambuzi ulikuwaje?

Shahidi: Sijamwambia kwa sababu sijaulizwa.

Kibatala: Ulimwambia Jaji yule askari mwanaume alijitambulisha kwako jina na cheo chake?

Shahidi: Sijamwambia sababu sijaulizwa.

Kibatala: Ulimwambia Jaji ulishuhudia majina yako yakiandikwa baada ya utambuzi

Shahidi: Sikumwambia

Kibatala: Katika kielelezo hiki PE9 (kielelezo cha 9 cha upande wa mashtaka, ambacho ni fomu ya gwaride la utambuzi wa mshtakiwa wa pili - Muyella), kuna mahali pamerekebishwa 8 na 9 umemwambia Jaji kuhusu marekebisho haya?

Shahidi: Sikumwambia.

Kibatala: Kielelezo hiki pia wameandika Miriam halafu wakafuta wakaandika Getruda, ulimwambia Jaji kuwa ulishirikishwa katika marekebisho haya?

Shahidi: Sijamwambia sababu siyajui.

Kibatala: Mawakili walikwambia utambue (katika kielelezo hicho) majina yako?

Shahidi: Hapana

Kibatala: Aneth alikuwa anamfahamu Kombo (Sabri) Haji? (Mpenzi wake Getruda, ambaye alikwenda kulala kwake Chanika baada ya kuondoka kwa marehemu Aneth)

Shahidi: Alikuwa hamfahamu

Kibatala: Alikuwa (Sabri Kombo Haji) mpenzi wako?

Shahidi: Alikuwa rafiki yangu.

Kibatala: Hakuwa mpenzi wako?

Shahidi: Alikuwa rafiki yangu.

Kibatala: Mlifahamiana Machi miezi miwili kabla Aneth kufariki, ni sahihi?

Shahidi: Siyo kweli

Kibatala: Mlifahamiana lini?

Shahidi: Tarehe 4/4/2016

Kibatala: Mlifahamiana wapi?

Shahidi: Huko huko Kigamboni.

Kibatala: Jirani na kwa marehemu alikokuwa anafanya kazi?

Shahidi: Hapana, alikuwa ni mkazi wa huko.

Kibatala: Unakumbuka alihamia huko lini?

Shahidi: Sifahamu nilimkuta.

Kibatala: Alikuwa anafahamu ulikokuwa unaishi?

Shahidi: Sikumtambulisha

Kibatala: Wakati unaondoka kwa Aneth ilikuwa majira ya saa 5:30 asubuhi, ni sahihi?

Shahidi: Ndio

Kibatala: Mlirudi saa ngapi (kwa marehemu Aneth) kurudisha funguo?

Shahidi: Saa 10 jioni.

Kibatala: Wakati unarudisha funguo hukuona gari ya Aneth?

Shahidi: Sikuona sababu alikuwa hajarudi.

Kibatala: Unafahamu ripoti ya daktari inasema Aneth alifariki muda wa saa 4 asubuhi (Mei 25, 2017) saa moja kabla ya wewe kuondoka?

Shahidi: Hapana dada alikuwa kazini.

Kibatala: Kutoka kwenye nyumba ya Aneth mpaka dukani ulikokuwa unakwenda (siku anayodai ndio alikutana na washtakiwa kwenye gari Kwa mara ya kwanza), ni umbali gani?

Shahidi: Si mbali ni nyumba ya pili tu.

Kibatala: Wakati afande David anakuhoji ulimwambia kuhusu huo umbali?

Shahidi: Sikumwambia afande David, huo ni ushahidi wa afande David na huu ni ushahidi wangu

Kibatala: Nitakuwa sahihi kuwa siku ya kwanza washtakjiwa walipokuja ilikuwa rahisi mtu wa dukani kuwaona?

Shahidi: Haikuwa rahisi, walisimama kwenye kona ya kueleza barabara kubwa.

Kibatala: Hiyo kona iko upande gani?

Shahidi: Kwenye ubavu wa nyumba ya duka.

Kibatala: Hapo ilikuwa ni kati ya nyumba ya Aneth na ya Duka?

Shahidi: Kwa kweli hayo masuala sikuweza kuyafahamu

Kibatala: Hukuweza kuyafahamu na ndio maana ya cross examination (maswali ya dodoso)

Kibatala: Ulimtajia Mheshimiwa Jaji hilo gari lililokuja Kibada (Kigamboni) siku ya kwanza lilikuwa aina gani?

Shahidi: Mimi nikishika rangi tu sukumtajia aina ya gari.

Kibatala: Haya mambo kwamba ulishika rangi ya gari tu hukumtajia aina ya gari ulimwambia afande David? (Wakati alipomhoji)

Shahidi: Nilimtajia rangi si aina ya gari.

Kibatala: Ulimtajiia afande David namba za gari hilo?

Shahidi: Sikumtajia namba sababu sikushika namba za gari

Kibatala: Ulimtajia Mheshimiwa Jaji muundo wa hiyo gari ya terehe 15/5/2016 au ulimwambia gari muundo wake ukoje?

Shahidi: Sikumwambia kwa sababu sijaulizwa

Kibatala: Ulimwambia Jaji baada ya kutolewa Moshi ulipoifika Chang'ombe (Kituo cha Polisi), kwa muda uliokaa hapo Polisi uliwahi kuoneshwa ile gari ili uitambue?

Shahidi: Sijamwambia jaii, sababu afande Mchomvu ( shahidi wa 10, Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Mjini Magharibi Zanzibar, Richard Mchomvu, ambaye wakati wa mauaji hayo alikuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Temeke(RCO), akiwa na cheo cha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP) wala David hawakuniuliza.

Kibatala: Ulimwambia Jaji mikufu ya dhahabu uliyodai alikuwa ameivaa mshtakiwa wa kwanza, muda wote wakati unahojiwa na kina Mchomvu na David waliwahi kuonesha uitambue?

Shahidi: Sijamwambia kwa sababu sijaulizwa hilo swali.

Kibatala: Leo hapa mahakamani hiyo mikufu mkubwa na midogo umemuonesha Jaji?

Shahidi: Sijamuonesha sababu haipo hapa.

Kibatala: Unasema pia tarehe 15 alivaa suti na viatu fulani na singlend, ni sahihi?

Shahidi: Ndio.

Kibatala: Uliwahi kuoneshwa uzitambue hizo nguo ulipokuwa kule Chang'ombe Polisi?

Shahidi: Sijawahi kukaa Chang'ombe maana sikuwa mshtakiwa.

Kibatala: Shahidi umesema baada ya kutoka Moshi na askari waliokufuata ulipelekwa kituo cha Polisi Chang’ombe, ambako ulihojiwa na Afande Mchomvu na kisha Afande David, Sasa nakuuliza wakati huo waliwahi kuonesha hizo nguo na viatu?

Shahidi: Hapana, hakuna aliyenionesha.

Kibatala: Hapa mahakamani hizo nguo umemuonesha Jaji na wazee wa baraza?

Shahidi: Sijaionesha sababu sijaulizwa.

Kibatala: Sasa twende kwenye gari ya Range Rover tarehe 18/5/2023, Unafahamu namba za ile gari?

Shahidi: Sizifahaku sababu sijazisoma.

Kibatala: Hizo nguo alizovaa huyo mama ulizozitaja, ullipokuwa Chang'ombe walikuonesha?

Shahidi: Ndio walinionesha

Kibatala: Umevitoa hapa mahakamani kama kielelezo?

Shahidi: Sijazionesha sababu sijaulizwa.

Kibatala: Nguo alizovaa tarehe 23/5/2016 zilikuwa nguo ngani?

Shahidi: Kwa kweli Sikumbuki

Kibatala: Yawezekana umesahau kwa sababu sasa ni muda mrefu, wakati Mchomvu na David wanakuhoji uliwasimulia hizo nguo?

Shahidi: Nimesema sizikumbuki sababu sikukariri nguo nilikariri matukio yaliyokuwa yanaendelea.

Kibatala: Sasa nakurudisha tena tarehe 15/5/2016 ulisema yule mama alijitambulisha kuwa ni ndugu wa Aneth, ni sahihi?

Shahidi: Ndio alijitambulisha hivyo.

Kibatala: Siku hiyo huyo mama alikutishia kwa chochote?

Shahidi: Hakunitishia kwa chochote

Kibatala: Na unasema ulikuwa na uhusiano mzuri na Aneth, ni sahihi?

Shahidi: Tena wa amani na furaha tele.

Kibatala: Baada ya kuachana na hao watu baadaye ulimwambia Aneth kuwa kuna ndugu yako nimekutana naye?

Shahidi: Sikumwambia sababu sikuwa na fikra mbaya, sikukumbuka

Kibatala: Ulikuwa na umri gani 2016?

Shahidi: Sikumbuki

Kibatala: Lakini ulikuwa mama. wa watoto watatu?

Shahidi: Ndio

Kibatala: Tarehe 18/5/2016, waliporidi tena walikutishia nini?

Shahidi: Siku hiyo waliniwekea bastola shingoni upande wa kushoto.

Kibatala: Ndio siku uliingia kwenye gari wakakuweka kati?

Shahidi: Ndio

Kibatala: Mwenye bastola alikaa upande gani?

Shahidi: Kushoto

Kibatala: Na yule Mama?

Shahidi: Upande wa kulia

Kibatala: Aliyekuwekea bastola alivaa chochote usoni?

Shahidi: Alivaa miwani.

Kibatala: Ulimwambia Jaji hiyo bastola ni ya rangi gani?

Shahidi: Sijamwambia sababu sijaulizwa.

Kibatala: Aliyekuwekea bastola ulishawahi kumuona tena?

Shahidi: Sikuwahi kumuona tena

Kibatala: Simu hiyo waliyokupatia ndo uliitupa ukiwa kwenye kivuko

Shahidi: Ndio

Kibatala: Ambapo hakukupa maelezo maalumu kuwa uitupe baharini ila ulijiongeza tu kuitupa baharini?

Shahidi: Ndio alishaniambia niitupe mahali ambako mtu mwingine hataiona.

Kibatala: Na baada ya kuondoka ukaingia nayo ukaificha na hukumwambia mtu yeyote?

Shahidi: Ndio sikumwambia mtu sababu ya vitisho walivyonitishia.

Kibatala: Na ukiwa peke yako ukaizima na kuificha si ndio?

Shahidi: Ndio

Kibatala: Kwa sababu uliitupa baharini kwa utashi wako namba za simu za huyu mama alizokupigia hatuwezi kuzipata, ni kweli?

Shahidi: Ndio

Kibatala: Shahidi, Wakili wa Serikali anakuongoza kuhusu Cairo Mererani ulikofanya kazi miezi sita, Babu Msuya ni kabila gani na Bibi Msuya?

Shahidi: Babu Msuya ni Mpare na Bibi Msuya sijui ni kabila gani

Kibatala: Umewahi kusikia mtu anaongea Kipare?

Shahidi: Hapana

Kibatala: Mtu akiongea Kipare unajua?

Shahidi: Siwezi kujua wanaongea lugha gani

Kibatala: Umesema baadaye ulivuta kumbukumbu kuwa ulimuona kwa Bibi Msuya na Baba mkwe wake akamtambulisha mkwe wake ilikuwa mwaka gani?

Shahidi: 2015.

Kibatala: Ulifahamu Erasto alifariki mwaka gani?

Shahidi: Sikujua

Kibatala: Lakini ulijua kuwa akifariki?

Shahidi: Nilijua lakini sikujua kama ni mtoto wa familia hiyo.

Kibatala: Huyo mama Mshtakiwa, alikaa muda gani

Shahidi: Alikaa muda mfupi akaondoka

Kibatala: Uliona dalili zozote za ugomvi?

Shahidi: Sikuona dalili za ugomvi

Kibatala: Ulimwambia Jaji kuwa gari alilokwenda nalo (hapo nyumbani kwa wakwe zake) ni moja ya magari uliyoyaona Kibada?

Shahidi: Mimi sikuona gari alilokuja nalo

Kibatala: Unamfahamu jirani yenu (wakati akiwa kwa marehemu Aneth), anaitwa Aziza?

Shahidi: Hapana simkumbuki

Kibatala: Mtu anaitwa Ahlam?

Shahidi: Simkumbuki

Kibatala: Ulisema hukuwahi kumuona baba Allan (aliyekuwa mume wa Aneth), wala mwanaume mwingine kwa Aneth, ni sahihi?

Shahidi: Ndio Sikuwahi kumuona baba Allan wala mwanaume mwingine yeyote.

Kibatala: Uliwahi kujua kama alifika nyuma (siku za nyuma) kabla hujafika?

Shahidi: Sikujua.

Kibatala: Aneth alikwambia baba Allan aliondoka kwa sabau gani

Shahidi: Hakuniambia

Kibatala: Wala huwezi kujua kama marehemu alikuwa anakaa na Allan kwa amri ya Mahakama?

Shahidi: Siwezi kujua

Kibatala: Ile nyumba ilikuwa kwa jina la nani?

Shahidi: Siwezi kujua