Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KESI YA MJANE WA BILIONEA MSUYA: Mtoto wa Bilionea Msuya alivyomtetea mama yake kesi ya mauaji

Miriam Steven Mrita, mjane marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya; akiwa na Wakili wake Peter Kibatala

Muktasari:

  • Mjane wa Bilionea Msuya ameendelea na utetezi wake dhidi ya kesi ya mauaji ya wifi yake, kupitia kwa mashahidi wake baada ya yeye mwenyewe kuhitimisha utetezi wake na leo.
  • Miongoni mwa mashahidi wake ni mtoto wake ambaye amehitimisha ushahidi wake aliouanza jana jioni, ambaye katika ushahidi wake alijikita katika suala la mirathi ya baba yake ambao linadaiwa na upande wa mashtaka kuwa sababu ya mjane huyo kuhusishwa na mauaji ya wifi yake.

Dar es Salaam. Mtoto wa kwanza wa Marehemu Erasto Msuya maarufu kama Bilionea Msuya; Kelvin Erasto Msuya ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa hakuna ndugu yeyote katika familia na ukoo wao aliyewahi kutamka kuwa wanamtuhum mama yake kuhusika na mauaji ya wifi yake.

Kelvin ametoa maelezo hayo wakati akihojiwa na Wakili Nehemiah Nkoko, kuhusiana na maswali ya dodoso aliyoulizwa na upande wa mashtaka, katika kesi ya mauaji inayomkabili mama yake, Miriam, Steven Mrita.

Miriam ambaye ni mjane  wa aliyekuwa mfanyabiashara wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, Wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, Agosti 7, 2013.

Anakabiliwa na mauaji ya wifi yake, Aneth Elisaria Msuya; yeye na mwenzake Revocatus Everist Muyella, maarufu kama Ray.

Aneth ambaye alikuwa mdogo wa marehemu Bilionea Msuya, aliuawa Mei 26, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam.

Kesi hiyo ya jinai namba 103 ya mwaka 2018, inasikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki.

Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, Miriam anatuhumiwa kuhusika na mauaji ya wifi yake kutokana na mgogoro wa mirathi ya marehemu Bilionea Msuya na kwamba alianza kubadilisha umiliki wa baadhi ya mali za marehemu, wakati alipokuwa msimamizi wa mirathi ya mumewe huyo.

Hata hivyo Miriam mwenyewe aliyakama madai hayo katika utetezi wake akidai kuwa hajawahi kuwa na mgogoro wa mali na wifi yake huyo kwani hata yeye alimgawia sehemu ya urithi.

Katika ushahidi wake aliouanza jana kumtetea mama yake, akiongozwa na wakili wa mshtakiwa huyo, Peter Kibatala na kuhitimisha leo Ijumaa, Novemba 3, 20123, kwa maswali ya dodoso Kelvin ambaye aliteuliwa kuwa mmoja wa wasimamizi wa mirathi hiyo baada ya mama yake, ameelezea namna walivyotekeleza jukumu hiyo mpaka mirathi hiyo ikafungwa.

Shahidi huyo wa tatu upande wa utetezi, ameieleza Mahakama kuwa waliteuliwa yeye na dada yeke wanayechangia baba, Glory Erasto Msuya kuwa  wasimamizi wa mirathi, Oktoba 27, 2021 baada ya mama yao kuondolewa katika jukumu hilo.

Ameeleza kuwa baada ya kuteuliwa walifuatilia katika halmashauri za Arusha, Moshi na Dar es Salaam kujua kama kuna ardhi ambayo baba yao alikuwa anazimiliki au alizowahi kumiliki lakini zikabadilishwa umiliki.

Hata hivyo ameeleza kuwa Dar es Salaam na Moshi hawakupata mali yoyote isipokuwa Arusha ndiko baba yao alikuwa anamiliki viwanja na nyumba kadhaa.

Pia amedai kuwa walikwenda kwa wakala wa Usajili Biashara na Leseni (Brela) kuona kama baba yao alikuwa anamiliki hisa katika kampuni mbili ambazo wanahisa wake ni baba yao, Erasto Elisaria Msuya na mama yao, Miriam Erasto Msuya (jina la ndoa) ambaye jina lake asili mi Miriam Steven Msuya.

Vilevile Kelvin ambaye ni meneja uzalishaji wa Kampuni ya SG. Premium Resort, inayomiliki Hoteli ya kitalii ya SG Hotel, amedai kuwa walikwenda Mamlaka ya Mapato kujua magari aliyokuwa anamiliki baba yao ambako walipata gari moja na kwamba kwenye akaunti za benki zilikuwa zimefungwa.

Kelvin ameleza kuwa baada ya kukamilisha kukusanya mali walizirodhesha wakawasilisha mahakamani fomu hiyo kisha wakafanya mgawo kwa wanufaika, wao watoto, mama yao pamoja na wazazi wa baba yao na wamepeleka mrejesho mahakamani.

"Tulipopeleka mrejesho mahakamani Jaji Kamuzora alituhoji kama kuna mtu alikuwa na dukuduku au lalamiko lolote baada ya zoezi kukamilika, sisi wanufaika pamoja na bibi. Wote tulisema tunafuraha na tumeridhika," alieleza Kelvin na kuhitimisha.

"Mama ambaye alikuwa jela ili kumhoji kama ameridhika Jaji Kamuzora alitumia mtandao wa zoom. Kwa sasa mirathi imefungwa tangu Agosti 11/2022 ndipo akatamka kuwa mirathi imefungwa rasmi."

Baada ya maelezo hayo shahidi huyo alihojiwa maswali ya dodoso na upande wa mashtaka pamoja na maswali ya kusawazisha hoja za maswali ya dodoso, kutoka kwa wakili Nehemia Nkoko, anayewakilisha mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Muyella.


Mahojiano hayo yalikuwa kama ifuatavyo;

SSA Kimweri: Shahidi kabla hujaondoka kwenda Australia (2013) pale nyumbani kwenu kulikuwa na magari mangapi ambayo ulikuwa unayaona?

Shahidi: Magari mawili

Wakili: Unamfahamu dereva wa familia yenu Karim Mruma?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Ni dereva wa magari yenu yote?

Shahidi: No ni dereva wa familia na kampuni.

Wakili: Uliporudi na ulipofuatilia kama msimamizi wa mirathi ulikuta magari mangapi?

Shahidi: Ni kama nilivyosema jana nilipata gari moja.

Wakili: Ni aina gani ya gari iliyoipata baada ya kufuatilia?

Shahidi: Ni Range Rover Ivogue, ndio ilikuwa katika usajili wa baba.

Wakili: Tazama kielelezo cha 9 cha upande wa utetezi (Hati ya orodha ya mali za marehemu Erasto Msuya) imeonesha magari mangapi?

Shahidi: Mawili.

Wakili: Ni ya aina gani?

Shahidi: Range Rover na Ford Ranger.

Wakili: Dereva wenu alisema mbali na magari ya familia kuna magari mengine mawili aliyoyaacha marehemu yapo magari mawili yanayotoa huduma kwenye mojawapo ya kampuni alizoziacha marehemu, Noah na Landcruiser TDI, unakubaliana nayo?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Sasa hapa kuna tuhuma dhidi ya mshtakiwa wa kwanza mama yako kwamba kuna baadhi ya mali zilibadilishwa umiliki, hayo magari mawili umeyaorodhesha kwenye mirathi?

Shahidi: Hapana, kwa sababu...

Wakili: Hizo sababu sizihitaji utaeleza huko, lakini sasa hili gari Range Rover Ivogue nani alipewa?

Shahidi: Mama yangu, Miriam Steven Mrita au Miriam Erasto Msuya.

Wakili: Hii Range Rover Ivogue ni T429BYY?

Shahidi: Hapana siyo.

Wakili: Mmiliki wa hiyo gari ni nani?

Shahidi: Erasto Elisaria Msuya.

Wakili: Iambie Mahakama kwa sasa hiyo gari iko wapi?

Shahidi: Iko Arusha nyumbani kwetu.

Wakili: Sasa soma hii nyaraka (taarifa ya uchunguzi wa namba za magari kutoka Mamlaka ya Mapato-TRA), iambie Mahakama ina namba zipi za usajili na mmiliki ni nani?

Shahidi: Hapa imeandikwa T429 BYY, Range Rover Ivogue, mmiliki ni Erasto Erisalia Msuya.

Wakili: Iambie Mahakama kwa mujibu wa hiyo kielelezo PE6 (kielelezo cha sita cha upande wa mashtaka) hati ya ukamataji mali wakati gari hiyo inakamatwa na Polisi iwapo huyu dereva wenu naye ni shuhuda na alisaini?

Shahidi: Naona jina Karim Mruma.

Wakili: Umesema hii mali inaonekana imekamatwa, lakini wewe umeiorodhesha, wakati unatafuta mali za marehemu ulikwenda Jeshi la Polisi kupata taarifa?

Shahidi: Sikuona umuhimu.

Wakili: Kwa sababu wakati huo ilikuwa nyumbani.

Wakili: Kwa hiyo unaiambia Mahakama kuwa gari hiyo haiko mikononi mwa Polisi?

Shahidi: Nimesema kwamba wakati huo ilikuwa nyumbani.

Wakili: Unakubaliana na mimi kwamba hakuna sababu yoyote uliyoitoa hapa mahakamani kwa nini hayo magari mawili Noah na Landcruiser TDI hukuyaorodhesha?

Shahidi: Haipo.

Wakili: Kama msimamizi wa mirathi kutokuorodhesha mali zilizoachwa na marehemu ni sahihi?

Shahidi: Siyo sahihi.

Wakili: Wakati Erasto Msuya anafariki ulikuwepo?

Shahidi: No sikuwepo.

Wakili: Baada ya kurudi na kufuatilia mali za marehemu uliwahi kufuatilia mali za marehemu ambazo zilikuwa bado kwenye transfer (uhamishwaji) lakini ulikuwa haijakamilika wakati anafariki?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji mirathi ni ya baba yangu, mimi niliorodhesha mali alizokuwa anamiliki baba.

Wakili: Kwenye hii orodha ya mali za marehemu twambie namba 8 ni kitu gani na mmiliki wake ni nani?

Shahidi: Ni gari na mmiliki wake ni Miriam Steven Mrita.

Wakili: Miriam Steven Mrita ni marehemu?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Umesema majina mengine ya Miriam Steven Mrita ni Miriam Erasto Msuya, wakati ulipiteuliwa kuwa msimamizi na kufuatilia mali. Angalia kielelezo DE8: Ruling ya Jaji Kamuzora kumuondoa Miriam katika usimamizi wa mirathi kuwa ni Kelvin na Glory kuwa wasimamizi, soma majina ya wadaawa.

Shahidi: Ndeshukurwa Elisaria Msuya na Miram Steven Mrita.

Wakili: Soma uamuzi huo mpaka mwisho kama kuna jina la Miriam Erasto Msuya?

Shahidi: Hakuna.

Wakili: Mshtakiwa wa kwanza kila anapoitwa hapa mahakamani anatajwa kwa jina gani?

Shahidi: Miriam Steven Mrita.

Wakili: Kati ya wewe shahidi na mama yako ambaye ni mshtakiwa nani mwenye haki ya kuieleza mahakama jina lake sahihi?

Shahidi: Ni mshtakiwa.

Wakili: Kwa kufanya ulinganisho, jina Miriam Steven Mrita na Miriam Erasto Msuya ni jina moja yanafanana?

Shahidi: Kiherufi hayafanani, lakini nimesema yote mawili ni ya mama yangu.

Wakili: Katika orodha ya wanufaika wa mirathi wakati unamtaja mshtakiwa wa kwanza hilo jina la Miriam Erasto Msuya uliandika?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Lililopo ni jina gani?

Shahidi: Miriam Steven Mrita.

Wakili: Kwa hiyo tangu umekuja kutoa ushahidi wako hapa hoja zako zote ni masuala ya mirathi tu, ni kweli?

Shahidi: Eeh, naizungumzia mirathi.

Wakili: Lakini unafahamu kesi inayomkabili mama yako mshtakiwa wa kwanza Miriam Steven Mrita hapa mahakamani ni ya mauaji ya Aneth Elisaria Msuya?

Shahidi: Ni ya mauaji siyo kesi ya mirathi.

Wakili: Katika ushahidi wako hakuna chochote ambacho umekizungumza kuhusiana na kesi ya mauaji kama mama yako anahusika au hahusiki, ni sahihi?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Mwisho

Wakili Nehamia Nkoko: Shahidi Utakubaliana na mimi kwamba wewe bado hujamaliza kutoa ushahidi wako mpaka mimi nitakapomaliza kukudodosa maswali na Wakili wako aliyekuongoza atakapomaliza kukuuliza maswali?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Utakubaliana nami kesi ya mauaji hapa mahakamani imeletwa na upande wa mashtaka?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Utakubaliana nami kwamba mojawapo ya hoja ambazo wamezileta hapa mahamani ni kwamba sababu ya mama yako kuhusika na mauaji walikuwa na mgogoro wa mirathi?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Utakubaliana na mimi katika maswali yoyote ya dodoso hakuna mahali ambapo dada yako au bibi yako wamekuja hapa mahakamani au kule Arusha wakalalamika kuwa katika mgawo ule walidhulumiwa?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Utakubaliana na mimi nyote kwa pamoja ninyi mnaamini kwamba Miriam Steven Mrita hizi tuhuma si za kweli?

Shahidi: Tunaamini.

Wakili: Na Utakubaliana na mimi kwamba mwaka huu wewe ulikuwa na babu yako hospitalini na bado mna mahusiano mazuri?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Babu yako alikuwa amelazwa Hospitali gani?

Shahidi: Rabininsia, Dar.

Wakili: Utakubaliana nami aliyefanya mipango ya wewe kwenda kusoma Australia ni shangazi yako?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Anaitwa nani?

Shahidi: Ester.

Wakili: Utakubaliana na mimi hadi unarudi Tanzania yeye ndio alikuwa anakuhudumia nauli, kula na mambo mengine yote?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Utakubaliana na mimi ni ukweli usiopingika kwamba mpaka unarudi Tanzania mwaka 2018 mahali ulikokuwa unaishi Australia ni nyumba ambayo shangazi yako alikuwa anailipia (hata baada ya yeye kuondoka 2015).

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Nitakuwa sahihi kuwa hata baada ya kuondoka shangazi yako huduma alizokuwa anakupatia aliendelea kukupatia hata baada ya shangazi yako Aneth kuuawa?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Utakubaliana na mimi hakuna yeyote katika ndugu zako shangazi, babu bibi au yeyote aliyewahi kukutamkia kwa mdomo wewe kuwa mama yako ndiye alimuua Aneth?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Utakubaliana nami kwamba jina maarufu mama yako Arusha alikuwa ni Mama Msuya?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Utakubaliana nami kuwa kumbukumbu kuwa mama yako anatumia pia jina la Miriam Erasto Msuya ulilipata kwenye kumbukumbu wakati unafuatilia mirathi ya baba yako?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Nini sababu hukuorodhesha yale magari mawili kwenye mirathi?

Shahidi: Hayakuwa na umiliki wa jina la baba.

Wakili: Hebu iambie Mahakama kwa nini tangu kesi hii ianze upande wa mashtaka hawakumleta ndugu zako akiwemo bibi yako kuja kutoa ushahidi kuwa wanamtuhumi mama yako?

Shahidi: Hawaamini kwamba mama alihusika.

Wakili Peter Kibatala, ameileza Mahakama kuwa baada ya kutathmini (maswali ya dodoso aliyoulizwa shahidi huyo na jinsi alivyoyajibu) hakuwa na swali lolote la ufafanuzi, alimaanisha kuwa ameridhika na majibu yake.

Kesi hiyo imeahirishwa kwa muda kabla ya kuendelea na shahidi wa nne wa utetezi baadaye.