Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KESI YA MJANE WA BILIONEA MSUYA: Miriam alivyohitimisha ushahidi mahakamani

Miriam Mrita akiwa kizimbani Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Miriam Steven Mrita mjane wa Erasto Msuya amehitimisha ushahidi wa utetezi wake kesi yake inayomkabili na kuahirishwa mpaka kesho ambapo ataita mashahidi wake wa kumtetea.

Dar es Salaam. Hatimaye mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya; Miriam Steven Mrita, amehitimisha ushahidi wa utetezi wake, huku akisisitiza kuwa hakuwa na sababu ya kufanya mauaji ya wifi yake anayotuhumiwa yeye na mwenzake.

Miriam alihitimisha ushahidi wake huo leo Novemba Mosi, 2023 baada ya kusimama kizimbani kwa siku sita, siku nne akitoa ushahidi wake mkuu akiongozwa na wakili wake Peter Kibatala na siku mbili za kujibu maswali ya upande wa mashtaka na maswali ya kusawazisha kutoka kwa wakili wake.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 103 ya mwaka 2018, inasikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Miriam anakabikliwa na shtaka la kumuua wifi yake, Aneth Elisaria Msuya; yeye na mwezake Revocatus Everist Muyella, maarufu kama Ray.

Aneth aliuawa Mei 26, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam. Alikuwa ni mdogo wake Bilionea Msuya aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Agosti 7, 2013.

Baada ya kuhitimisha ushahidi wake huo leo, sasa kesho Novemba 2, 2023 anatarajia kuwaita mashahidi wake kwa ajili ya kuunga mkono ushahidi wake kabla ya kufunga kesi kwa upande wake na kumpisha mshtakiwa wa pili, Muyella kuanza kutoa utetezi wake.


Mahojiano

Wakili wa Serikali: Shahidi, jana nilikuuliza maswali mbalimbali na ukasema usingeweza kumuua Aneth kwa sababu ulimlea kama mtoto wako wa kumzaa, lakini nilipokuuliza kama umeshawahi kusikia mama amemuua mtoto wake au mtoto kamuua mama yake ukajibu kuwa umeshasikia.


Sasa nakuuliza, wewe na Aneth ni mtoto wako wa kumzaa?


Shahidi: Si mtoto wangu wa kumzaa.


Wakili: Kwa hiyo tunakubaliana kwamba kumlea au kumzaa mtoto haiwezi kuwa sababu ya kutokumuua?


Shahidi: Kunakuwa na sababu.


Wakili: Kwa hiyo tunakubaliana kwamba inawezekana kumuua kukiwa na sababu?


Shahidi: Ndio Mheshimiwa (amejibu baada ya jaji kuingilia kati na kumtaka ajibu tu kama alivyoulizwa).


Wakili: Katika ushahidi wako umeeleza kuwa hakukuwa na mgogoro wa mirathi, ni sahihi?


Shahidi: Siyo kweli, nilieleza kuwa sikuwahi kuwa na mgogoro wowote wa mali na Aneth.


Wakili: Wakati unatoa ushahidi wako na nilipoanza kukuhoji ulisema jina lako ni nani?


Shahidi: Miriam Steven Mrita.


Wakili: Ukiacha majina hayo uliiambia Mahakama kuwa pia una majina mengine yaanI aka?


Shahidi: Sikuieleza.


Wakili: Sasa shahidi umeleta vielelezo hapa mahakamani kuishawishi Mahakama kuwa wewe ulikuwa shareholder (mwanahisa) kwenye kampuni ya SG. Hotel. Sasa nitakuuliza kuanzia DE6 ukrasa wa 21. Twambie majina ya shareholder yaliyoandikwa hapa ni nani na nani?


Shahidi: Erasto Elia Msuya na Miriam Erasto Msuya.


Wakili: Sasa jina ulilolitaja mahakamani la Miriam Steven Mrita na lililoko kwenye kielelezo hiki, Miriam Erasto Msuya hayafanani, tunakubaliana ni sahihi?


Shahidi: Ndio


Wakili: Sasa kwa mujibu wa share (hisa) zilizogawanywa humu Miriam Steven Mrita hana share, maana kuna share 600 kwa  Erasto Elia Msuya na share 200 kwa Miriam Erasto Msuya kwa hiyo Miriam Steven Mrita hana share hapo.


Shahidi: Hana mheshimiwa (anajibu baada ya jaji Kakolaki kuingilia kati kumuuliza tena swali la wakili kama Miriam Steven Msuya ana share).


Wakili: Unakubaliana nami kwamba mojawapo ya taarifa ambazo Polisi wanazipata ni kutoka kwa raia, ni sahihi?


Shahidi: Ndio


Wakili: Huyu Ndeshukurwa Elisaria Elia Msuya (mama wa marehemu Aneth, aliyewajulisha mahali alikokuwa Getruda) ni raia wa Tanzania?


Shahidi: Ndio.


Wakili: Pia umeelezea kushangaa Getruda (shahidi wa 25 upande wa mashtaka) kusema alitishwa na akakaa muda woote huo bila kutoa taarifa (kuhusiana na madai ya washtakiwa kwenda kwa marehemu Aneth na kukutana naye), unakumbuka?


Shahidi: Ndio


Wakili: Sasa hebu tusaidie wewe kwa uelewa wako kuna muda maalumu wa mtu kukaa na kitisho kwenye nafsi yake?


Shahidi: Sijui Mheshimiwa.


Wakili: Na utakubaliana nami kwamba hata hivyo vitisho vyenyewe vinatofautiana, haviko sawa?


Shahidi: Mimi ninachojua mheshimiwa jaji vitisho ni vitisho tu.


Wakili: Kwa hiyo anayetishiwa kuchapwa fimbo na anayetishiwa kuuawa vyote vinalingana?


Shahidi: Vitisho ni vitisho tu.


Wakili: Umeieleza Mahakama sababu za kutaka Getruda asiaminike ni kutokumbuka hata sare (za shule) alizokuwa anamvalisha Allan (mtoro wa marehemu Aneth)?


Shahidi: Ndio.


Wakili: Sasa shahidi hebu ieleze Mahakama tangu tukio hilo lilipotokea Aneth alipouawa mwaka 2016 mpaka mwaka huu Getruda alipokuja kusimama mahakamani ni miaka mingapi imepita?


Shahidi: Miaka Saba.


Wakili: Utakubaliana nami kuwa katika kipindi hichohicho kwa tukio hili hili hata wewe mwenyewe kuna vitu huvikumbuki kama namba za magari (ya familia yake) ni sahihi?


Shahidi: Ndio.


Wakili: Ukisema kwamba katika mgawo wa mirathi ulioufanya japokuwa hakuna uthibitisho, kwamba Aneth alishukuru na akasema atajenga nyumba kuweka kumbukumbu, hiyo nyumba umewahi kuiona ?


Shahidi: Bado.


Wakili Nehemiah Nkoko (utetezi): Shahidi mimi nitakuuliza maswali machache tu ya ufafanuzi. Utakubaliana na mimi kwamba hakuna shahidi aliyekuja hapa kusema kwamba wewe hukuhudhuria mazishi ya Aneth?


Shahidi: Ni kweli hakuna shahidi aliyesema hivyo.


Wakili: Pia utakubaliana na mimi kuwa hakuna ndugu yeyote wa Aneth aliyekuja akasema kuwa wewe unahusika na mauaji ya Aneth?


Shahidi: Ndio hakuna yeyote aliyekuja kusema hivyo.


Wakili: Pia utakubaliana nami kuwa hakuna ndugu yeyote aliyekuja kusema wewe na mshtakiwa wa pili (Muyella) mlipanga mauaji ya Aneth?


Shahidi: Kweli hakuna ndugu yeyote aliyekuja kusema hivyo.


Wakili: Utakubaliana na mimi kuwa hakuna ndugu wa Aneth au shahidi yeyote aliyekuja kusema kuwa kuna ndugu wa Aneth aliyekwenda kulalamika Polisi kuwa wewe na mshtakiwa pili ndio mlimuua Aneth?


Shahidi: Ndio hakuna shahidi huyo.


Wakili: Pia utakubaliana na mimi kwamba kwenye jalada hakuna maelezo ya mlalamikaji na hamjawahi kupewa maelezo ya mlalamikaji?


Shahidi: Ni kweli hatujawahi kupewa maelezo ya mlalamikaji.


Wakili: Nitakuwa sahihi kwamba hakuna shahidi yeyote aliyekuja hapa akatoa ushahidi kwamba wewe na marehemu Aneth mlikuwa na mgogoro wa mali?


Shahidi: Hakuna mheshimiwa.


Wakili: Utakubaliana na mimi kwamba hakuna shahidi yeyote au ndugu wa karibu akiwemo baba mama au mtoto akasema kuwa wewe hukuwahi kuwapa pesa zilizotokana na mirathi ya Erasto Msuya?


Shahidi: Hakuna mheshimiwa.


Wakili: Na vilevile hakuna shahidi yeyote kutoka katika ukoo wa Msuya aliyekuja kusema wewe ulijimilikisha mali za marehemu mume wako mara tu alipokufa?


Shahidi: Hakuna mheshimiwa.


Wakili: Sasa kuna maswali uliulizwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi kuwa kuna siri imejificha lakini hukuisema, nitakuwa sahihi kwamba hakuna ndugu hata mmoja wa Aneth aliyekuja hapa mahakamani kusema kwamba wewe na mshtakiwa wa pili ndio mlimuua ndugu yao na kwamba hiyo ndio siri yenyewe, nitakuwa sahihi?


Shahidi: Ndio mheshimiwa.


Wakili: Sasa shahidi utakubaliana nami kuwa mashahidi wengi waliokuja wakasema kuhusu gwaride la utambuzi, utakubaliana nami Getruda alishindwa kutambua ni kituo kipi alipelekwa kufanya utambuzi?


Shahidi: Ni kweli mheshimiwa.


Wakili: Uliulizwa kuhusu kilelezo DE3 na PE17 (taarifa za awali za tukio la uhalifu yaani mauaji ya Aneth, ya kwanza inayosema Getruda alikamatwa na kuhojiwa kama mtuhumiwa na nyingine ikisema kuwa hakuwahi kukamatwa) kuhusu kukamatwa kwa Getruda,  mashahidi wa Jamhuri  wanapingana katika hili, ni kweli?


Shahidi: Ni kweli mheshimiwa.


Wakili Kibatala: Shahidi nitakuuliza maswali machache kuhusiana na maswali aliyokuuliza wakili (mwendesha mashtaka) akitumia nyaraka ambayo niliitumia kumuuliza maswali shahidi wa 22, (Mhanaya), kuwa ulibadilisha umiliki wa gari T800 CKF, tarehe 12/12/2013, kuja kwenye majina yako, unaiambia nini mahakama kuhusiana na gari hilo kwa kutumia nyaraka hii?


Shahidi: Mheshimiwa jaji hii gari inatoka kwenye kampuni Goldlisten Mwanga kwenda kwa Miriam Steven Mrita.


Wakili: Pia shahidi wakili alikuuliza kama ulileta mahakamani ushahidi wa kimaandishi kuwa ulipelekwa hospitalini kutibiwa baada ya kupigwa ukasema hujaleta unaiambia nini Mahakama kuhusu hilo?


Shahidi: Mheshimiwa jaji nilisema kuwa sikuleta nyaraka lakini walikuja madaktari wa Magereza na wa hospitali ya Temeke kutoa ushahidi.


Wakili: Shahidi uliulizwa pia kuhusu vielelezo vya kampuni na iwapo majina yaliyoko kule (Miriam Erasto Msuya) yanakuhsu wewe, unaiambiaje Mahakama kuhusu majina yaliyoko kwenye vielelezo hivyo na haya uliyoyataja hapa mahakamani (Miriam Steven Mrita)?


Shahidi: Miriam Steven Mrita ni la baba yangu mzazi.


Baada ya kuhitimisha mahojiano hayo kesi hiyo imeahirishwa mpaka kesho ambapo mshtakiwa wa kwanza Miriam ataita mashahidi wake wa kumtetea.