Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kesi ya Mjane wa Bilionea Msuya: Korti yapokea nyaraka kutoka CMC 

Miriam Mrita, mke wa aliyekuwa mfanyabiashara wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya

Muktasari:

  • Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imepokea nyaraka iliyozalishwa kutoka kwenye mfumo iliyotolewa na kampuni ya CMC Automobiles Limited kama kielezo.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imepokea nyaraka iliyozalishwa kutoka kwenye mfumo iliyotolewa na kampuni ya CMC Automobiles Limited kama kielezo.
Nyaraka hiyo imetolewa leo Novemba 8 katika kesi ya mauaji inayomkabi Miriam Mrita, mke wa aliyekuwa mfanyabiashara wa madini mkoani Arusha, Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya.

Mshitakiwa mwingine ni Revocatus Muyella.
Mahakama pia imevikataa  viambatanisho viwili ikieleza vipo kinyume cha utaratibu kwa kuwa ni nakala za majibu.

Viambatanisho hivyo ni barua ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) iliyoandakiwa kwenda CMC na nakala ya taarifa ya nyaraka inayoonyesha uingiajia na utokaji wa gari gereji.
Katika kesi ya jinai namba 103 ya mwaka 2018, Miriam na Muyella wanakabiliwa na shtaka la mauaji, wakidaiwa kumuua Aneth Msuya, aliyekuwa wifi wa Miriam.

Aneth aliuawa Mei 26, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam.

Alikuwa mdogo wa Bilionea Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, Agosti 7, 2013. 
Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki, iko katika hatua ya utetezi. Jana iliendelea kwa maswali ya dodoso kwa shahidi wa nne wa upande wa utetezi.
Shahidi huyo Ernest Msuya, ni meneja utawala na matengenezo (ya magari ya wateja) wa kampuni ya uuzaji magari ya CMC Automobiles Limited, maarufu kama CMC Motors, makao makuu Dar es Salaam.
Awali, wakili wa utetezi, Peter Kibatala aliweka pingamizi wakati Wakili wa Serikali, Paul Kimweri akimuongoza shahidi huyo kutoa nyaraka hiyo kutoka kwenye mfumo ikionyesha mtiririkio wa matengenezo ya gari.
"Mheshimiwa jaji tunapinga kwa sababu hatujamsikia shahidi akisema kuna viambatanisho vyovyote, lakini kwa upande wa barua hatuna pingamizi kwa sababu utaratibu umefuatwa," amedai wakili Kibatala.
Wakili Kimweri alieleza katika msingi wa swali lake alimuuliza shahidi kuhusu mfumo wa kutunza kumbukumbu na akasema zote zinazofanywa kwenye mfumo ni za uhakika. 

 "Baada ya kumuuliza hizo kumbukumbu za kwenye mfumo ni za uhakika na zinaweza kuonekana ndiyo tukaja kwenye barua, ambayo amesema ni majibu kwenda kwa DPP na kuhusu kumbukumbu za historia ya hicho ambacho amekuja kukitolewa ushahidi, shahidi amesema hana shida na kumbukumbu za kwenye mfumo," alieleza Wakili Kimweri na kuongeza:
“Pia shahidi nimemuuliza kama hana tatizo ya barua na viambatanisho vyake ili Mahakama ione, akasema hana tatizo, kwa hiyo Jaji namna ambavyo tumeweka msingi kwamba barua hiyo ndiyo inajibu kuhusu mfumo, huwezi pokea barua ukaacha viambatanisho kwa sababu ni sehemu moja.” 
"Sisi tunafikiri tumeweka msingi kwamba hakuna tatizo la kuzuia kielelezo kisipokelewe kwa sababu kimsingi si pingamizi la kisheria ni pingamizi la content na si hoja ya kisheria," amedai.
Akitoa uamuzi wa pingamizi hilo, Jaji Kakolaki alisema pingamizi lilitokana na viambatanisho, shahidi hakuwezeshwa kuelezea uhusika wake kabla ya kutolewa, hivyo ni kweli hoja ya Kibatala kwamba shahidi hakuelekezwa kuhusu viambatanisho. 
"Katika viambatanisho hivi ni kweli kuna baadhi ya nyaraka mbili ni nakala, kwa hiyo haviwezi kuwa sehemu ya hiyo barua husika kwa sababu ziliambatanishwa kinyume. Pingamizi la Kibatala sehemu linakubalika kwa kutokupokea nakala, lakini kuhusu vielelezo viwili vinaweza kupokewa kama ushahidi," alisema Jaji Kakolaki. 
Baada ya uamuzi huo, Wakili Kimweri aliendelea na maswali ya dodoso kwa shahidi huyo wa mshtakiwa wa kwanza, Miriam, ambaye anafanya idadi ya mashahidi wa utetezi kuwa wanne akiwemo mshtakiwa mwenyewe.
Ifuatayo ni sehemu ya maswali na majibu baina ya Wakili wa Serikali Kimweri na shahidi wa mshtakiwa wa kwanza Miriam.
Kimweri: Ulisema taarifa zote zipo kwenye mfumo na pia mfumo unatunza kumbukumbu sahihi hata kama zimetoka kwenye matawi mengine. 
Shahidi: Sahihi. 
Kimweri: Mheshimiwa Jaji naomba kumuonyesha nyaraka hii shahidi atueleze kama anaijua.
Shahidi: Ni barua kutoka CMC Automotors.
Kimweri: Kwa kuwa umetambua barua iliyoandikwa na bosi wako, una tatizo kama ikitolewa mahakamani kama kielelezo. 
Shahidi: Sina tatizo. 
Kimweri: Tunaomba ipokelewe kama kielelezo pamoja na viambatanisho vyake kwa sababu shahidi hana pingamizi. 
Wakili Peter Kibatala: Mheshimiwa Jaji tunapinga kwa sababu hatujamsikia shahidi akisema kuwa kuna viambatanisho vyovyote, lakini kwa upande wa barua hatuna pingamizi kwa sababu utaratibu umefuatwa. Hivyo vingine tunapinga. 
Wakili Kimweri alitoa hoja na mwishowe Jaji Kakolaki alitoa uamuzi kama ilivyoelezwa mwanzoni mwa habari hii.
Baada ya Mahakama kupokea nyaraka iliyozalishwa kutoka kwenye mfumo kuhusu gari namba T 307 CDH aina ya Ford Ranger na barua ya majibu kutoka kwa mmiliki wa kampuni Haji kwenda kwa DPP, wakili Kimweri aliendelea:
Kimweri: Mheshimiwa Jaji tunaomba shahidi asome (barua) ili kuonyesha viambatanisho vilivyokuwapo. 
Shahidi: Nyaraka hii ni job card (kadi ya matengenezo) ya CMC Automotors ya gari namba T 307 CDH aina ya Ford Ranger.
Alidai Mei 9, 2016 gari hilo liliingia CMC saa mbili asubuhi na lilitoka siku hiyohiyo saa 11 jioni. 
Katika historia ya gari lilianza kutengenezwa CMC mwaka 2015. Juni 21, 2015, Oktoba 6, 2015 na Novemba 27,2015 lilikwenda kutengenezwa mfumo wa kiyoyozi. 
Kimweri: Sasa shahidi kwa kielelezo hiki, kwanza kabla sijaendelea mbele utakubaliana na mimi ni lini gari lilikwenda huko CMC kwa ajili ya matengenezo (akimaanisha tarehe alizozitaja). 
Shahidi: Sikubaliani na wewe. 
Kimweri: Shahidi ni vilevile tu kwamba siku hiyo gari lilikuwa linashughulikiwa CMC Motos. 
Shahidi: Ni kweli. 
Jaji: Ni nyaraka gani uliyokuwa unasoma? 
Shahidi: Rekodi ya matengenezo. 
Kimweri: Kwa rekodi hiyo ya matengenezo ieleze Mahakama ni tarehe ngapi, mwezi gani na mwaka gani gari hilo linaonekana kufanyiwa matengenezo ni kweli kuna tarehe 9/5/2016. 
Shahidi: Sahihi kabisa gari lilikuja kufanyiwa matengenezo. 
Kimweri: Baada ya gari hilo kushughulikiwa Mei 9, 2016 pamepita muda gani, kurudi tena kufanyiwa matengenezo CMC au ni tarehe ngapi tena inaonyesha mlilifanyia tena matengenezo?
Shahidi: 19/10/2016.
Kimweri: Kwa rekodi hizi tangu Mei 9, 2016 hadi Oktoba 19, 2016 haionyeshi kwamba gari halijawahi kufanyiwa matengenezo tena. 
Shahidi: Ni kweli. 
Kimweri: Na hiyo gari ni namba ngapi vile. 
Shahidi: Ni T 307 CDH aina ya Ford Ranger. 
Kimweri: Hebu shika kielelezo chenu DE11 ambacho kimejazwa kwa mkono, nataka uangalie 9/5/2016 ni kweli gari hilo lilikuwa CMC. 
Shahidi: Ni sawa tarehe hiyo. 
Kimweri: Iambie Mahakama kwa hicho kielelezo chako cha kuandika kwa mkono ukiacha tarehe 9/5/2016 ni tarehe ngapi kinaonyesha gari liliingia tena CMC. 
Shahidi: 10/8/2016.
Kimweri: Tutakubaliana hizo ni tarehe za kuingia gari CMC. 
Shahidi: Ndiyo. 
Kimweri: Kielelezo ulichokitoa mahakamani vinasigana na nyaraka zilizozalishwa kutoka kwenye mfumo wa CMC kuhusu gari hilo. 
Shahidi: Havisigani/haina tofauti kuhusu tarehe. 
Kimweri: Sasa kama hakuna tofauti, ieleze Mahakama tarehe iliyofuata ya gari hilo kutengenezwa kwenye gereji ya CMC. 
Shahidi: Agosti 10, 2016. 
Kimweri: Kwa mujibu wa kielelezo DE 11 na PE 18 iambie mahakama kama hizo tarehe kwenye nyaraka zote mbili zinalingana? 
Shahidi: Havilingani. 
Kimweri: Katika kielelezo ulichokileta mahakamani hakuna tarehe nyingine ambayo gari liliingia yaani ile ya mwisho ambayo imefungwa kabisa hapo chini kwenye kielelezo chako DE 11.
Shahidi: Tarehe ya mwisho kabisa ni 10/8/2016.
Kimweri: Haionekani tena ni tarehe gani ilifanyiwa service tena CMC. 
Shahidi: Hii nyaraka kazi yake ni kuingia gari na kutoka. 
Kimweri: Baada ya kusoma kichwa cha habari cha hiyo nyaraka yako, utakubaliana na mimi kwamba ni kwa ajili ya services. 
Shahidi: Hapana si unaona kuna kilomita. 

Kimweri: Wakili wako alikuelekeza Mei 14/2016 na Mei 15/2016 gali hilo lilikuwa CMC kwenye matengenezo. 
Shahidi: Hapa kwenye nyaraka haionyeshi kama ilifanyiwa matengenezo.  
Katika ushahidi wa msingi shahidi huyo  aliieleza Mahakama kuwa gari aina ya Ford Rangers yenye namba za usajili T307 CBH linalohusishwa katika kesi hiyo liko kwenye gereji yake tangu Mei 9, 2016.
Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, Miriam na mwenzake walikwenda Kigamboni kwa marehemu Aneth mara ya kwanza Mei 15, 2016, wakiwa na gari aina ya Ford Rangers (T307 CBH) kwa ajili ya kufanya mipango ya mauaji hayo.
Ushahidi huo ulitolewa kwa nyakati tofauti na shahidi wa 22, Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Arusha, Mrakibu Mwandaimizi wa Polisi (SSP), David Mhanaya kutokana na maelezo ya aliyekuwa mfanyakazi wa ndani wa marehemu Aneth, Getruda Mfuru.
Getruda ambaye ni shahidi wa 25 na wa mwisho wa upande wa mashtaka pia alirudia maelezo hayo katika ushahidi wake, akidai kuwa washtakiwa walikwenda huko na akaonana nao mara tatu kwa siku tofauti  Mei 15, 18 na 23, 2016 wakiwa na magari tofauti likiwemo gari hilo.
Shahidi wa pili upande wa utetezi, Karim Mruma aliyejitambulisha kuwa dereva wa Miriam na familia yake aliieleza Mahakama kuwa yeye ndiye amekuwa akimwendesha na kwamba, Mei Miriam hakutoka nje ya Arusha.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi leo mshtakiwa wa pili, Revocatus Muyella akitarajiwa kuanza kujitetea.