Prime
Kero ya maji, umeme, afya kilio kikubwa ziara ya Chongolo

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo akizungumza na wanachama, viongozi wa CCM wa Mpanda Mjini, Jumatatu Oktoba 2, 2023 katika ofisi za chama hicho mkoani Katavi. Picha na Mpiga Picha wetu
Katavi. Kero za maji, umeme, miundombinu ya barabara na uhaba wa watumishi wa sekta ya afya zimeibuliwa na wananchi na viongozi katika ziara ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo mkoani hapa.
Ziara hiyo ya siku tano jana Jumanne Oktoba 3, 2023 ilianzia wilayani Tanganyika kwa kukagua ujenzi wa hospitali teule ya wilaya hiyo iliyopo Kata ya Ikola, kisha kutembelea Bandari ya Karema itakayohudumia nchi za Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Burundi na Zambia.
Baada ya kuibuliwa kero hizo kwa nyakati tofauti, Chongolo aliwataka mawaziri wanaohusika na changamoto hizo kufika mkoani hapa kuzitafutia ufumbuzi, akiwemo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ili ashughulikie umeme wa Gridi ya Taifa.
Mawaziri wengine ni Jumaa Aweso (Maji), Innocent Bashungwa (Ujenzi) na Mohamed Mchengerwa wa Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Tatizo la umeme lilianza kuibuliwa juzi jioni katika kikao cha ndani kilichokuwa na lengo la kumpa taarifa za mkoa za chama hicho na ya Serikali iliyowasilishwa kwake na Mkuu wa Mkoa wa Katavi (RC), Mwanamvua Mrindoko.
Baada ya kupokea taarifa hizo, alipata wasaa wa kuwasalimia mamia ya wananchi waliojitokeza kumpokea katika ofisi za chama hicho, akisema haiwezekani mkoa huo umeunganishwa na barabara nzuri ya lami kutoka Tabora hadi Katavi halafu ukakosa umeme wa uhakika utakaochochea maendeleo ya mkoa huo ulioanzishwa mwaka 2012.
“Nimekuja kufuatilia utekelezaji wa Ilani yetu ya mwaka 2020/25 ambayo ndani yake imebeba ahadi za barabara, afya, umeme, kilimo, pembejeo na mambo mengi. Tuliahidi, hivyo tunakuja kutembelea na kukagua miradi hiyo,” alisema Chongolo.
Akiendelea kutoa salamu zake, Chongolo alisema amepokea taarifa ya chama pamoja na ya Serikali iliyowasilishwa na mkuu wa mkoa huo yenye masuala mbalimbali, ikiwamo changamoto ya mkoa huo kutokuwa na umeme wa uhakika.
Alisema katika taarifa zao mbili za CCM na Serikali walizowasilisha viongozi hao wa chama na Serikali, alidai kuwa wamesisitiza kuhusu suala la umeme ambalo ni kero kwa wananchi na wawekezaji wanaotaka kuwekeza mkoani hapa.
Chongolo alisema ameelezwa kumekuwa na ahadi zinazotolewa na viongozi mbalimbali ili kukamilika kwake, lakini utekelezaji wake unasuasua wakati chama tawala kiliahidi mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma itaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, lakini mpaka sasa ni Rukwa na Kigoma pekee imeunganishwa.
“Kigoma wamekwisha kuunganishwa kwa sehemu kubwa, Rukwa tayari, bado Mkoa wa Katavi, niwaahidi mimi natamani kuchaguliwa kwa kishindo ndani ya mkoa huu,” alisema Chongolo, huku akishangiliwa na sauti zikisikika, “tumekwisha shinda babaaaa.”
Baada ya kueleza hayo, aliuliza kama mradi huo upo chini ya Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) au Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kujibiwa Tanesco.
“Basi niachieni mimi, nitakwenda kukaa na waziri anayehusika na hiyo Tanesco na bahati nzuri amepewa mamlaka makubwa, kwa hiyo hana sababu ya kujitetea.
“Nitakwenda kumwambia kwanza yeye mwenyewe aje aangalie uhalisia wa utekelezaji wa huu mradi, lakini mbili ahakikishe anaweka nguvu zake zote hapo ili wananchi wa Mkoa wa Katavi wajielekeze kupata umeme wa Gridi ya Taifa,” alisema Chongolo.
Pia, alisema mkuu wa mkoa amemweleza kuwa, watu wengi wanataka kuwekeza, ikiwamo viwanda kama vya kuchakata alizeti lakini changamoto ni umeme wa uhakiki.
“Na sisi ni jukumu letu kuleta umeme na kazi yangu ni rahisi, kwenda kusimamia tuliyoyaahidi yanakwenda kutekelezwa. Niwaambie tu nakwenda kusukuma mradi huu uwe historia,” alisema Chongolo.
“Hatuwezi kuwa na barabara nzuri kutoka Tabora hadi hapa Katavi halafu nguzo tu za umeme zikatushinda, tutakuwa hatutendei haki dhamira zetu na Rais aliyetuamini kuwa wasaidizi wake kwenye maeneo mbalimbali.”
Mradi huo uliwekwa jiwe la msingi Oktoba 2019 na Rais wa wakati huo, John Magufuli (aliyefariki Machi 17, 2021) kuunganisha Mkoa wa Katavi kwenye Gridi ya Taifa kwa njia ya msongo wa Kilovolti 132 kutoka mkoani Tabora.
Suala hilo likaibuliwa tena jana katika Bandari ya Karema na mbunge wa viti maalumu, Taska Mbongo aliposema bandari hiyo haitakuwa na maana kama hakutakuwa na umeme wa uhakika," tunaomba sana katibu mkuu, tupate umeme wa Gridi ya Taifa. Katavi inahitaji sana umeme na hili linawezekana kabisa."
Akijibu hilo, Chongolo alisema, "jana usiku (juzi) nilizungumza na waziri (Biteko) amenihakikishia hili linakwenda vizuri. Ameniambia fidia kwa wale wanaopisha mradi hadi Oktoba 15 mwaka huu watakuwa wamelipwa na mimi niwahakikishie, umeme wa Gridi ya Taifa utafika, ili umeme unaotumika nchi nzima, utumike Katavi."
Mikataba isainiwe hapa
Kero nyingine ni ya barabara ya kilomita 112.9 ya kutoka barabara kuu ya Tanganyika kwenda Bandari ya Karema, akasema Waziri Bashungwa anapaswa kuisimamia ipasavyo ianze haraka.
Kabla ya maagizo hayo, Mbunge wa Tanganyika (CCM), Suleman Kakoso alimweleza Chongolo barabara hiyo imekuwa kero, hasa mvua inaponyesha, hali inayosababisha adha kwa wananchi.
Kutokana na hilo, Chongolo alimwita Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara, Albert Laizer ambaye alisema kandarasi zimetangazwa na hadi Novemba mwaka huu atakuwa amepatikana.
Alisema ni makandarasi wawili ambao mmoja atajenga kilomita 50 na mwingine zaidi ya 40.
Hata hivyo, Chongolo alisema pindi makandarasi watakapopatikana, mikataba ikasainiwe Karema mbele ya wananchi na si Dar es Salaam.
"Nimemwambia Waziri Bashungwa mkandarasi atakapopatikana waje kutia saini hapa Karema na wananchi washuhudie na sio wafanyie Dar es Salaam. Wananchi waone hatua ambazo Serikali inafanya na hili nitalisimamia kuona linatekelezwa," alisema Chongolo.
...Aweso aje ndani ya wiki mbili
Maji ni kero iliyoibuka kila eneo na ilianza katika Hospitali Teule ya Wilaya ambako wananchi walilalamika kutokuwapo kwa maji, licha ya chanzo chake kupatikana takribani kilomita saba.
Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Mkoa wa Katavi, Mhandisi Peter Ngunula alisema katika bajeti ya mwaka 2023/24 zimetengwa Sh6 bilioni zitakazomaliza tatizo la maji.
Akizungumza katika hilo, mbunge Kakoso, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge wa Kamati ya Miundombinu alisema msukumo unahitajika wa fedha hizo kutolewa eneo la Ikola kwa kuwa idadi ya wananchi imeongezeka, tofauti na mahitaji yalivyo sasa.
Hoja ya maji ikaibuliwa katika mkutano wa Shina namba 5, Kata ya Kapalamsenga, baada ya mwenyekiti wa shina hilo, Michael Lugelelo kusema kuna tatizo kubwa la maji.
Kakoso aliunga mkono kauli hiyo akisema, “kuna mradi wa maji wa Sh1 bilioni, lakini huu mradi hauendi vizuri kabisa."
Chongolo akamwita Ngunula wa Ruwasa kuzungumzia hilo akasema mradi “unaendelea na umefikia asilimia 45, tunaendelea kumhimiza (mkandarasi)."