Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kanuni za Kibiblia za kupata utajiri

Mwalimu George Mbwambo.

Wapendwa katika Kristo Bwana Yesu asifiwe! Leo tunaangazia somo muhimu na lenye changamoto kwa kila mmoja wetu: Kanuni za Kibiblia za kupata utajiri.

Mara nyingi utajiri huonekana kwa jicho la mashaka ndani ya kanisa, lakini Biblia haikatazi utajiri bali inatuonyesha jinsi ya kuupata kwa njia ya haki na jinsi ya kuutumia kwa utukufu wa Mungu.

 Katika maandiko, tunakutana na watu waliobarikiwa kwa wingi kama Ibrahimu, Ayubu, Daudi, na Sulemani. Lakini si mali zao tu zilizowavuta kwa Mungu bali moyo wao, bidii yao na uaminifu wao.


Katika somo hili, tutachambua kanuni tano kuu za Kibiblia ambazo, zikitumiwa kwa uaminifu, zinaweza kumuwezesha mtu kupokea baraka za kiuchumi kutoka kwa Mungu.


1. Kutafuta Ufalme wa Mungu Kwanza – Mathayo 6:33

"Bali utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na haki yake, na hayo yote mtazidishiwa."

Kanuni ya kwanza ya kupata utajiri wa kweli ni kumuweka Mungu mbele ya kila kitu. Watu wengi hukimbilia mali na biashara kabla ya kuimarisha uhusiano wao na Mungu. Biblia inatufundisha kuwa, tunapotanguliza kutafuta utakatifu na upendo wa Mungu, kwani hutupatia yale tunayoyahitaji ikiwa ni pamoja na fedha na mali. Hii siyo tu ahadi, bali ni kanuni ya maisha.


2. Kufanya kazi kwa bidii – Mithali 10:4

"Mkono wa mtu aliye na bidii huleta utajiri."

Mungu hawezi kuwabariki wavivu. Mungu huwakumbatia wale wanaofanya kazi kwa bidii, waaminifu na wanaotumia vipawa walivyopewa. Katika Biblia, tunaona kuwa hata Yesu mwenyewe alifanya kazi akiwa hapa duniani akiwa seremala kabla ya kuanza huduma yake. Paulo aliandika kwamba asiyeweza kufanya kazi asile. Kwa hiyo, kazi ni baraka na ni njia ya Mungu ya kutufanikisha.

Bidii yako inapaswa kwenda sambamba na maombi yako. Hauwezi kuomba baraka huku hulimi, huuzi, husomi, au kufanya juhudi yoyote.


3. Uaminifu katika kidogo – Luka 16:10-11

"Aliye mwaminifu katika kilicho kidogo, huwa mwaminifu katika kilicho kikubwa pia."

Mungu huwapima watu katika mambo madogo kabla ya kuwapa makubwa. Ikiwa huwezi kusimamia mshahara mdogo au biashara ndogo kwa hekima na uaminifu, Mungu hatakuaminisha na mapato makubwa.

Hii ni kanuni muhimu ya kuwa msimamizi bora wa kile Mungu amekuwezesha nacho sasa. Ukiwa mwaminifu na sahihi katika matumizi ya fedha zako sasa, Mungu atafungua milango ya baraka kubwa zaidi.


4. Kutoa kwa ukarimu – Mithali  11:24-25; Malaki 3:10

"Kuna mtu atawanyaye, lakini huongezewa zaidi... mtoaji kwa moyo mweupe atanenepeshwa."

Biblia inatufundisha kwamba moja ya njia kuu ya kupokea ni kutoa. Kutoa ni mbegu, unapotoa kwa moyo wa upendo na imani, unapanda mbegu itakayokuzalia mavuno. Mtoaji hawezi kosa, kwani Mungu mwenyewe anahakikisha kuwa anatunza watu wanaoshiriki baraka na wengine.


Katika Malaki 3:10, Mungu anasema:

"Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu; mkanijaribu kwa jambo hili... kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni."

Kutoa zaka, sadaka na kusaidia maskini ni funguo za Kibiblia za baraka za kifedha.


5. Kusikiliza na kufuata mwongozo wa Mungu – Kumbukumbu la Torati 8:18

"Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akuapaye nguvu za kupata utajiri."

Mungu ndiye anayetoa uwezo wa kupata mali. Siyo akili peke yako, siyo elimu tu, bali ni neema ya Mungu inayokuwezesha kufanikisha kazi zako. Lakini hiyo neema huja kwa wale wanaomsikiliza na kumtii.

Ukiwa na usikivu kwa Roho Mtakatifu, Mungu anaweza kukuongoza kufanya maamuzi bora ya kifedha, kuchagua biashara au kazi inayofaa, na kukuongoza kuepuka mitego ya shetani katika masuala ya fedha.

Kumbuka katika maisha yako ya hapa duniani, Mungu anapokupa baraka ya fedha usimuache kwa sababu hizo fedha ukizibeba vibaya unaweza kuzitumia kama silaha ya uharibifu, lakini ukiwa na Mungu utazibeba kwa moyo wa unyenyekevu, huku ukijua kwamba ni chombo cha kumtukuza Mungu, kusaidia masikini na kuwajali wengine wasiokuwa nacho.


Wapendwa, utajiri si kitu kibaya. Tatizo si kuwa na mali, bali mali kukumiliki wewe. Mungu anatamani watoto wake waishi maisha ya baraka ili wawe baraka kwa wengine. Lakini hiyo baraka huja kwa wale wanaotii kanuni zake.


Hebu tukumbuke: Tuwe waaminifu kwa Mungu kwanza, Tufanye kazi kwa bidi, Tuwe waaminifu hata kwa kidogo, Tutoe kwa ukarimu, Tumsikilize Mungu na kufuata mwongozo wake.


Kwa kufanya haya, hatutakimbiza utajiri bali baraka za Mungu zitatufuata sisi. Na tunapobarikiwa, tusisahau kwamba mali zote ni za Bwana na sisi ni wasimamizi tu. Tuitumie kwa utukufu wake!

Tuombe; Ee Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo, tunakuomba utufundishe njia zako za kweli za baraka. Tupe moyo wa kumtafuta kwa bidii, uaminifu, ukarimu na usikivu. Fungua milango ya baraka juu ya maisha yetu ili tuwe baraka kwa familia zetu, jamii zetu na kanisa lako. Katika jina la Yesu Kristo. Amina


Mwalimu George Mbwambo anapatikana Usharika KKKT Buza, kwa ushauri na maombezi simu +255 788 873 267.