Prime
Kanisa lashinda kesi umiliki wa mali, mchungaji aagizwa kuondoka
Muktasari:
- Katika hukumu iliyotolewa Juni 22, 2026, Jaji Frank Mahimbali amekubaliana na madai ya EAGT kwamba mali hiyo ilitolewa kwa kanisa kupitia hati ya zawadi iliyotekelezwa mwaka 1996 na Cleopa Lotakajaki (marehemu), kwa madhumuni ya shughuli za kidini.
Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, imehitimisha mgogoro wa muda mrefu kuhusu umiliki wa mali ya kanisa iliyopo Elerai, jijini Arusha, kwa kuwatangaza Wadhamini Waliosajiliwa wa Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) kuwa wamiliki halali wa eneo hilo pamoja na majengo yote yaliyopo.
Katika hukumu iliyotolewa Juni 22, 2026, Jaji Frank Mahimbali amekubaliana na madai ya EAGT kwamba mali hiyo ilitolewa kwa kanisa kupitia hati ya zawadi iliyotekelezwa mwaka 1996 na Cleopa Lotakajaki (marehemu), kwa madhumuni ya shughuli za kidini.
Kesi hiyo ilifunguliwa na EAGT dhidi ya wadhamini waliosajiliwa wa Revival Evangelistic Assemblies of God Tanzania (REAGT) pamoja na Mchungaji, Marko Haule.
Mchungaji Haule alidai kuwa ardhi hiyo alipewa binafsi kwa njia ya mdomo na Lotakajaki mwaka 1986, kabla ya kuandaliwa kwa hati ya zawadi.
Mahakama ilieleza ushahidi uliowasilishwa na EAGT umethibitisha kuwa dhamira ya Lotakajaki ilikuwa kuikabidhi ardhi hiyo kwa kanisa na si kwa mtu binafsi.
Katika uchambuzi wake, Mahakama imebaini kuwa shughuli za ibada za Kikristo zilianza kufanyika katika eneo la Elerai katikati ya miaka ya 1980 baada ya waumini kuhamishwa kutoka Shule ya Msingi Elerai.
Chanzo cha mgogoro
Mgogoro huo ulitokana na mvutano wa umiliki wa majengo ya kanisa yaliyopo Elerai (Bonde la Baraka), Sakina jijini Arusha. Kanisa la EAGT lilidai kuwa eneo hilo ni mali yake tangu Juni 8, 1996, lilipotolewa kwa ajili ya shughuli za kidini.
Kwa upande wake, Mchungaji Haule alipinga madai hayo akisisitiza kuwa ardhi hiyo alipewa yeye binafsi kwa njia ya mdomo na marehemu Lotakajaki mwaka 1986.
Alidai kuwa ndiye aliyeanzisha shughuli za kanisa katika eneo hilo.
Hata hivyo, Kanisa la EAGT linadai kuwa tangu kupokea eneo hilo mwaka 1996, limekuwa likilitumia kwa shughuli za ibada na kuendeleza miundombinu mbalimbali, ikiwemo jengo la kanisa na nyumba ya mchungaji.
Miongoni mwa mashahidi wanne wa upande wa mlalamikaji alikuwa Askofu Shadrack Mollel, ambaye alieleza kuhusu usajili wa taasisi hiyo na umiliki wa mali zake.
Mashahidi wengine pia wametoa ushahidi kuhusu namna ardhi hiyo ilivyotolewa kwa EAGT na jinsi ilivyotumika kwa muda mrefu kama mali ya kanisa.
EAGT pia lilieleza kuwa Mchungaji Haule alikuwa mtumishi wake hadi mwaka 2019 alipofukuzwa kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu. Baada ya kuondolewa, aliendelea kutumia na kumiliki mali hizo kinyume cha sheria kwa kushirikiana na REAGT.
Kwa upande wake, REAGT ilikana kumiliki mali hiyo, ikieleza kuwa haijawahi kusajiliwa kama mmiliki wala kuhamishiwa umiliki wa eneo hilo kwa mujibu wa sheria.
Mahakama ilivyoamua
Baada ya kuchambua ushahidi wa mashahidi, vielelezo vya nyaraka na hoja za mawakili wa pande zote, Jaji Mahimbali amesema ameridhika kuwa marehemu Lotakajaki alikusudia kuipa EAGT ardhi hiyo na si mtu binafsi.
Alisema madai ya Mchungaji Haule kwamba alipewa ardhi hiyo kwa mdomo mwaka 1986 hayakuungwa mkono na ushahidi wa kutosha. Mahakama pia imebaini kuwa hakuna nyaraka zilizowasilishwa kuthibitisha kuwa marehemu Lotakajaki alimhamishia umiliki wa eneo hilo binafsi Mchungaji Haule.
Jaji alieleza kuwa ushahidi wa Mchungaji Haule ulikuwa na dosari na kutofautiana katika hatua mbalimbali za usikilizwaji wa kesi.
Kuhusu madai dhidi ya REAGT, mahakama ilikubaliana kuwa taasisi hiyo haikuwahi kusajiliwa kama mmiliki wa mali hiyo. Aidha, ushahidi ulionyesha kuwa shughuli zake za kidini zilikuwa zikiendelea katika eneo hilo kupitia Mchungaji Haule bila kuwa na msingi wa kisheria wa umiliki.
Kutokana na sababu hizo, Mahakama Kuu ilitangaza kuwa Wadhamini Waliosajiliwa wa EAGT ndio wamiliki halali wa mali hiyo na kuwaamuru washtakiwa kuondoka katika eneo hilo na kukabidhi umiliki ndani ya siku 60.
Mahakama pia ilitoa amri ya kudumu inayowazuia washtakiwa kuingia au kufanya shughuli zozote katika eneo hilo bila idhini ya EAGT.
Aidha, washtakiwa wameamriwa kulipa fidia ya jumla ya Sh20 milioni kwa kosa la uvamizi na matumizi ya mali hiyo bila idhini ya mmiliki halali.