Kamati yaagiza wananchi washirikishwe miradi ya maji, umeme

Muktasari:
- Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imeilekeza Wizara ya Maji, Nishati na Madini kuwashirikisha wananchi wanapotekeleza miradi ya maji na umeme kuepuka migogoro inayotokea katika baadhi ya maeneo inapotekelezwa miradi hiyo.
Unguja. Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imeilekeza Wizara ya Maji, Nishati na Madini kuwashirikisha wananchi wanapotekeleza miradi ya maji na umeme kuepuka migogoro inayotokea katika baadhi ya maeneo inapotekelezwa miradi hiyo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Abdallah Rashid Aballah ametoa kauli hiyo leo Jumapili Agosti 21, 2022 wakati wa majumuisho ya ziara ya kamati hiyo iliyoifanya Unguja na Pemba kutembelea miradi ya maji na umeme inayotekelezwa chini ya wizara hiyo.
“Kamati imetoa maelekezo kwa changamoto ilizozibaini katika miradi ya maji na umeme, kuna shida ya kutowashirikisha wananchi, lazima wakazi wa maeneo inayotekelezwa miradi hiyo washirikishwe wakati wa kufanya utafiti kabla ya utekelezaji wake haujaanza,” amesema Abdallah
Amesema hatua hiyo itaondosha migogoro isiyo ya lazima ambayo imebainika baadhi ya maeneo wananchi wakisema hawashirikishwi kwenye hatua za mwanzo.
Hata hivyo, amepongeza ripoti ya utekelezaji wa miradi hiyo akisema kamati imeona vifaa vya umeme ambavyo vimenunuliwa na Shirika la Umeme (Zeco) na hatua mbalimbali zilizofikiwa katika miradi ya maji; uchimbaji visima, ujenzi wa matanki na usambazaji wa mambomba.
Awali, akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa miradi kwa kipindi cha Februari hadi Juni 2022, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Joseph Kilangi pamoja na mafanikio hayo, ametaja changamoto zilizowakabili ikiwamo za kitaalamu na vifaa kuchelewa kufika kwa wakati.
Kwa Upande wake, Naibu waziri wa wizara hiyo, Shabaan Ali Othman amesema wizara imepokea maelekezo yaliyotolewa na kamati hiyo, “tutayatekeleza kama tulivyoagizwa. Naomba kamati isisite kutukosoa itatusaidia kuleta ufanisi katika utendaji kazi wetu.”