Prime
Kamati ya Bunge yataka Ma-DED wasisimamie uchaguzi, Serikali nayo yakomaa

Muktasari:
- Hivyo ni dhahiri suala hilo la wakurugenzi wa halmashauri za majiji, manispaa, miji na wilaya kuendelea kusimamia uchaguzi, litaendelea kuibua mvutano kwa wadau wa demokrasia, kama wanavyoeleza baadhi yao waliozungumza na Mwananchi.
Dodoma/Dar. Pendekezo la Serikali la kutaka wakurugenzi wa halmashauri waendelee kusimamia uchaguzi linaonekana kuwa kaa la moto baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuja na pendekezo jipya juu ya suala hilo.
Hivyo ni dhahiri suala hilo la wakurugenzi wa halmashauri za majiji, manispaa, miji na wilaya kuendelea kusimamia uchaguzi, litaendelea kuibua mvutano kwa wadau wa demokrasia, kama wanavyoeleza baadhi yao waliozungumza na Mwananchi.
Baadhi ya vyama vya siasa, kikiwemo chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho ndicho chama kikuu cha upinzani nchini, wanaharakati, wanazuoni na viongozi wa dini wamepinga kundi hilo la watendaji wa Serikali kuendelea kusimamia uchaguzi.
Sababu kubwa inayotajwa na wanaopinga hadi kubisha hodi mahakamani kuomba tafsiri, ni kwamba watendaji hao ambao huteuliwa na Rais kushika wadhifa huo, baadhi yao wanatajwa kuwa ni makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), huku Tume ya Uchaguzi ikiwa haina mamlaka juu yao.
Mbali na hoja hiyo, baadhi ya wadau wa demokrasia wanaona si sahihi mtu aliyeteuliwa na Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa chama tawala kinachoshiriki uchaguzi, kusimamia uchaguzi na hivyo hauwezi kuwa huru na haki.
Katikati ya mjadala huo ambao bado ni mbichi, Kamati ya Bunge imekubaliana na maoni ya baadhi ya wadau kwamba wakurugenzi wa majiji, manispaa, miji na wilaya hawana ulazima wa kusimamia uchaguzi.
Soma zaidi: Miswada mitatu ya uchaguzi yatua kwa Spika
Badala yake kamati imeshauri wasimamizi wa uchaguzi watumike “watumishi wa umma waandamizi au mtu yeyote mwenye sifa kwa madhumuni ya uchaguzi katika jimbo au kata”.
Hayo yalielezwa jana bungeni jijini Dodoma na mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Joseph Mhagama wakati akisoma maoni na ushauri wa kamati kuhusu Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2023.
Pia, miswada ya Sheria ya Uchaguzi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa, yote ya mwaka 2023 nayo ilitolewa maoni na ushauri.
Ni baada ya miswada hiyo kuwasilishwa kwa nyakati tofauti na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama ikiwa na mabadiliko kadhaa kutokana na maoni ya wadau mbalimbali wa demokrasia.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga akizungumza na gazeti hili nje ya Bunge, alisema miswada hiyo haijazingatia mapendekezo mengi yaliyotolewa na wadau.
“Kama maoni ya wadau yamezingatiwa basi ni kwa asilimia 20, lakini niliyatarajia haya kwa sababu wasingeweza kufanya mabadiliko makubwa bila kugusa Katiba. Endapo mapendekezo ya wadau yangezingatiwa, ni lazima ingehusisha kuzifuta kabisa hizo sheria, ziandikwe upya,” alisema Dk Henga.
Maoni ya Dk Henga hayako mbali na ya John Mnyika, katibu mkuu wa Chadema, aliyesema, “miswada iliyosomwa mara ya pili jana haijakidhi haja ya wadau kama matokeo ya Rais kuhojiwa mahakamani, mgombea binafsi, muundo wa tume huru ya uchaguzi hayajashughulikiwa na ndio maana sisi (Chadema) tulisema yatanguliwe na mabadiliko madogo ya Katiba.”
Mnyika alisema kilichofanyika kwa Serikali kuiwasilisha miswada hiyo na Kamati ya Bunge kusoma taarifa zake kinathibitisha hoja yao ya kuondolewa kwa miswada hiyo ili iandikwe vizuri.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatibu alilipongeza Bunge na Serikali kwa kufanyia kazi maoni yaliyotolewa na wadau kupitia vikao mbalimbali.
“Hili ni jambo zuri kufanyia kazi maoni ya wananchi, japo yapo mambo yaliyochukuliwa na mengine kuachwa, hasa suala la ruzuku ya vyama, lakini hatukati tamaa, tutaendelea kupaza sauti ili tunapokwenda kwenye uchaguzi vyama vyote viwe sawa,” alisema.
Alisema kuna vyama vingi havipati ruzuku, lakini kwa hatua iliyofikiwa sasa, wataendelea kupambana.
Ma-DED si lazima
Moja ya mada moto katika mjadala huo ni ya Ma-DED kuendelea kusimamia chaguzi, ambayo Dk Mhagama alisema, “kamati bado ina maoni kwamba hakuna ulazima wa sheria kuweka sharti kwa mkurugenzi wa jiji, manispaa, mji na wilaya kuwa msimamizi wa uchaguzi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi kwa kuwa uzoefu unaonyesha wapo wakurugenzi ambao kwa sababu mbalimbali, wanapoteza sifa za kuwa wasimamizi wa uchaguzi.”
Dk Mhagama alisema Ibara ya 6(1) inaeleza kuwa kila mkurugenzi wa jiji, mkurugenzi wa manispaa, mkurugenzi wa mji na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya atakuwa msimamizi wa uchaguzi kwa madhumuni ya kuendesha uchaguzi katika jimbo au kata.
Alisema pia kamati yake inatambua wakurugenzi kutajwa kwenye sheria kwa kuwa mahakama ya Rufani ya Tanzania kwenye kesi ya madai namba 138/2019 na Mahakama ya Afrika ya Watu na Haki za Binadamu kwenye kesi ya madai namba 11/2020 zote ziliamua kuwa wakurugenzi kusimamia uchaguzi hakukiuki masharti ya Katiba wala Mkataba wa Afrika wa Watu na Haki za Binadamu, mtawalia.
“Kamati ilikuwa ina maoni kwamba sheria isiweke ulazima kwa mkurugenzi mtendaji kusimamia uchaguzi na badala yake, kuwepo na masharti ya mtumishi wa umma mwandamizi au mtu mwingine yeyote mwenye sifa, kuteuliwa kuwa msimamizi wa uchaguzi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi,” alisema Dk Mhagama.
Maoni ya Kamati yanatofautiana na ya Serikali, lakini yanakwenda sambamba na ya wadau mbalimbali wa siasa, akiwemo Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliyetoa maoni katika mkutano wa demokrasia uliofanyika hivi karibuni, kuwa wakurugenzi wasisimamie uchaguzi na badala yake watafutwe maofisa waandamizi serikalini.
Pia, Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) kupitia kiongozi wao, Susan Lyimo waliwasilisha maoni yao kwenye kamati hiyo ya wabunge, akisema si sahihi wakurugenzi kusimamia uchaguzi kwa kuwa ni watumishi wa umma na wamekuwa wakisimamia masilahi ya aliowateua.
“Mfano, Rais Magufuli (John) ambaye amefariki dunia aliwahi kutamka kwa kuwaeleza wakurugenzi kwamba hawezi kuwalipa mshahara waje kumtangaza mgombea wa upinzani ameshinda,” alisema Lyimo.
Pia, alisema wakurugenzi wako chini ya Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na wanawajibika huko na si kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), hivyo alishauri wasimamizi waajiriwe na Tume.
Mwanaharakati wa Katiba, Deus Kibamba akizungumza na gazeti hili alisema pamoja na Serikali kusisitiza wakurugenzi kusimamia uchaguzi, ameshangazwa taarifa ya kamati kukubali watumishi wa umma kusimamia uchaguzi pamoja na watu wengine wenye sifa.
“Tukitaka kitu kamili kipatikane kitu kamili, maoni yalikuwa wakurugenzi wasisimamie uchaguzi na wasimamizi wa uchaguzi watokane na ajira za Tume ya Taifa ya Uchaguzi,” alisema.
Alisema muswada huo unapaswa kuwaondoa wakurugenzi na watumishi wa umma kusimamia uchaguzi.
Akinukuu maoni ya wadau wengine, Kibamba alisema wadau walipendekeza wakurugenzi na watumishi wa umma wasisimamie uchaguzi, bali Tume ya Taifa ya Uchaguzi iajiri watu wengine huru.
Uchaguzi serikali za mitaa
Kuhusu hoja kwamba uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu usimamiwe na NEC, Serikali imesema suala hilo haliwezekani kwa kuwa ni vigumu kufanya mabadiliko hayo sasa.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Florent Kyombo alisema kwa mujibu wa Serikali maandalizi yameanza.
“Ibara ya 11 ya muswada inaeleza majukumu ya Tume yatahusiana na uratibu na usimamizi wa uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani. Sheria haijajumuisha mapendekezo na maoni ya wadau ya kuitaka Tume iwe ndicho chombo pekee cha usimamizi wa uchaguzi nchini, ikiwemo usimamizi wa chaguzi za serikali za mitaa, vijiji na vitongoji,” alisema.
Kyombo alisema itakuwa vigumu kwa sasa kubadili majukumu ya usimamizi wa uchaguzi huo na kwamba, Serikali inaendelea kufanya utafiti juu ya namna bora ya kusimamia uchaguzi huo kwa siku za usoni.
“Kamati inaishauri Serikali kuharakisha mchakato utakaowezesha kuwa na chombo kimoja pekee cha kusimamia chaguzi zote nchini, ikiwemo uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji,” alisema
Katika hoja hiyo, Mnyika, aliyezungumza na gazeti hili baadaye alisema, “hoja hiyo ni kisingizio kwa sababu muda wa maandalizi hauwezi kuwa finyu, mpaka sasa hawajatengeneza kanuni za uchaguzi, utasemaje ni muda finyu?”
Mbunge huyo wa zamani wa Kibamba na Ubungo alihoji kunapotokea vifo vya wabunge au nafasi za uchaguzi huwa inatumia muda gani kuandaa?
“Uchaguzi wa serikali za mitaa unaweza kusogezwa mbele na ukafanyika mwakani na hili jambo si geni kwa sababu uchaguzi uliwahi kusogezwa mbele, wa madiwani na ukafanyika kwa pamoja.
“Suala si muda, bali hawataki uchaguzi wa serikali za mitaa usimamiwe na Tume Huru ya Uchaguzi. Serikali inapaswa kusikiliza na kuzingatia maoni ya wadau.”
Hoja hiyo ilizungumzwa pia na Kibamba, akisema suala hilo ni mfupa mgumu.
“Kamati inaacha mfupa huu mgumu uendelee kuwepo, uchaguzi wa Serikali za mitaa lazima usimamiwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, inaweza isianze mwaka huu lakini tukaanza kidogo kidogo,” alisema.
Kamati ya usaili
Kuhusu hoja kwamba mkurugenzi wa uchaguzi wa NEC kuwa katibu wa kamati ya usaili wa nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa NEC, Serikali imekubaliana na maoni ya wadau kwamba bosi huyo wa NEC hawezi kuwa katibu wa kamati ya usaili.
Dk Mhagama alisema ibara ya 9(3) ya muswada huo imemtaja mkurugenzi wa uchaguzi kuwa ndiye atakuwa katibu wa kamati ya usaili wa wajumbe wa Tume.
Alisema ibara ya 18(1) ya muswada inaeleza mkurugenzi wa uchaguzi atateuliwa na Rais baada ya kupendekezwa na Tume.
Kuhusu ibara hiyo, Waziri Jenista alisema Serikali inapendekeza ibara ya 9 inayohusu kamati ya usaili ifanyiwe marekebisho.
Lengo la kuweka utaratibu wa kupendekeza kwa Rais majina kwa ajili ya uteuzi wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti na kufanya usaili wa wajumbe watano wa tume kama ilivyo sasa.
“Ibara hiyo inapendekezwa kufanyiwa marekebisho ili kumuondoa mkurugenzi wa uchaguzi kuwa katibu wa kamati hiyo na badala yake kumwezesha Rais kuteua ofisa mwandamizi katika utumishi wa umma kuwa katibu wa kamati ya usaili,” alisema Jenista.
Hoja hiyo pia iliwahi kutolewa maoni na Zitto kwamba chama chake kinapendekeza kwenye kamati ya usaili kwenye kifungu cha 9(3) ambacho kinamfanya mkurugenzi wa uchaguzi kuwa katibu wa kamati ya usaili, kirekebishwe ili asiwe katibu wa kamati ya usaili.
“Tunaweza kumchukua Katibu wa Bunge kuwa katibu wa kamati ya usaili, au katibu wa Tume ya Utumishi ya Mahakama kuwa katibu wa kamati ya usaili au Katibu wa Haki wa Tume za Binadamu,” alisema Zitto.
Hoja za Serikali
Akiwasilisha mapendekezo ya Serikali Bungeni, Waziri Jenista alisema Serikali imekubaliana na baadhi ya hoja za wadau, ikiwamo ya kuifanyia marekebisho ibara za 12, 20 na 21 kwa kuongeza hali ya ulemavu kuwa miongoni mwa taarifa zitakazokuwa kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga Kura.
Jenista alisema pia Serikali imekubaliana na hoja za wadau za kuondoa ada ya marekebisho ya taarifa na ada ya kupewa kadi mpya ya mpiga kura pale inapokuwa imepotea au imeharibika.
Hoja ya kuondoa ada ya kitambulisho cha mpiga kura ilitolewa na viongozi wengi wa vyama vya siasa, waliosema kuweka ada kwa aliyepoteza kitambulisho cha mpiga kura au kuharibika kutasababisha watu wengi kukwepa kulipia, hivyo kupunguza idadi ya wapiga kura.
Kuhusu pingamizi kwa wagombea kwa mujibu wa Jenista, Serikali inapendekeza ibara ya 26, 27, 28 na 29 zifanyiwe marekebisho kwa kumuondoa mkurugenzi wa uchaguzi na ofisa mwandikishaji kuwa miongoni mwa waweka pingamizi pamoja na kufuta Mahakama ya Wilaya na kuweka Mahakama ya Mwanzo.
Hata hivyo, hoja ya mgombea pekee kutangazwa mshindi kwa kupata kura nyingi, bado iko vilevile, tofauti na maoni ya wadau kwamba mgombea pekee ashinde kwa asilimia 51.
Maoni hayo yalitolewa na Katibu wa Chadema Kanda ya Kati, Emmanuel Masonga aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kwamba chama hicho kinapendekeza kiongezwe kifungu kwamba mgombea pekee atangazwe kushinda kwa zaidi ya asilimia 50.
Pia, Serikali imekubaliana na hoja kwamba NEC itangaze kata ya udiwani inapokuwa wazi.
“Serikali inapendekeza ibara ya 57 ifanyiwe marekebisho kwa kuipa Tume mamlaka kutangaza nafasi iliyo wazi ya udiwani baada ya kupata taarifa kutoka kwa waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa kama inavyobainishwa katika Aya ‘L’ ya Jedwali la Marekebisho,” alisema Jenista kwenye taarifa yake Bungeni.
Jenista alisema pia Serikali inapendekeza ibara ya 79 ifanyiwe marekebisho kwa kuongeza sharti la karatasi ya kura kuwa katika muundo utakaowezesha matumizi kwa watu wenye mahitaji maalumu kama inavyobainishwa katika Aya ‘M’ ya Jedwali la Marekebisho.
Hoja hii ilitolewa na baadhi ya wadau kutaka karatasi za kura ziwe na nukta nundu na mazingira rafiki kwa wenye ulemavu kuweza kupiga kura.