Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kamanda Mwakyoma aagwa Kilimanjaro, kuzikwa kesho Mbeya

Muktasari:

  • Mwakyoma alifariki dunia Aprili 7, 2025 katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) alikopelekwa kwa matibabu na anatarajiwa kuzikwa kesho, Aprili 11, 2025, mkoani Mbeya.

Moshi. Mwili wa Kamanda mstaafu wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Absalom Mwakyoma umeagwa leo Alhamisi, Aprili 10, 2025 nyumbani kwake mjini Moshi na kusafirishwa kwenda Mbeya kwa maziko.

Mwakyoma alifariki dunia Aprili 7, 2025 katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) alikopelekwa kwa matibabu na anatarajiwa kuzikwa kesho, Aprili 11, 2025, mkoani Mbeya.

Akizungumza wakati wa ibada iliyofanyika nyumbani kwake Mtaa wa Kibo YMCA, Manispaa ya Moshi, Mchungaji wa Kanisa la Moraviani,  George Kijazi amewataka wananchi kutenda matendo mema nyakati zote.

Mke wa Marehemu Absalom Mwakyoma akiwa ameshikiliwa akilia wakati mwili wa mume wake ukiagwa. Picha na Omben Daniel

"Mtu anapokufa, matendo yake yanafuatana naye na hakuna ambaye matendo ya mtu yatamfuata, kila mtu katika ulimwengu huu ataondoka na matendo yake,” amesema Mchungaji Kijazi.

Katika ibada hiyo ya kumuaga, iliyotawaliwa na vilio na simanzi, imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa siasa, dini, Serikali na wafanyabiashara.

Akizungumza wakati akitoa salaam za rambirambi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema Mwakyoma atakumbukwa kwa uchapakazi wake na kuitaka familia kudumisha upendo ili kumuenzi kwa mema yote aliyoyatenda wakati wa uhai wake.

"Wito wangu kwa familia niwaombe mshikeni Mungu, biblia inasema mheshimu baba na mama yako na ili mama aendelee kuwa na maisha marefu, mnapaswa kuonyesha mapenzi kwake, mumuheshimu na mpendane kama familia na hivyo ndivyo mnavyoweza kumuenzi baba yenu,” amesema Kamanda Maigwa.

Akitoa salamu za pole kwenye msiba huo, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Mjini, Faraji Swai amesema kamanda mstaafu Mwakyoma atakumbukwa kwa ucheshi wake na namna alivyoishi vizuri na watu na jamii iliyokuwa inamzunguka.

"Kwa niaba ya CCM tumepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa CCM Kata ya Mfumuni kuanzia mwaka 2017 hadi 2023, alipostaafu,” amesema Swai.

 "Hakika tumemkosa mtu muhimu kwenye chama chetu. Alikuwa mtu mcheshi, mwenye mapenzi na watu, alijichanganya na watu na aliishi kwa upendo na kila mtu.”

Mwakyoma alijiunga na Jeshi la Polisi Septemba 1973 na ameshika nyadhifa mbalimbali katika mikoa mbalimbali nchini ikiwamo ukuu wa polisi wilaya (OCD) na mkuu wa upelelezi mkoa (RCO) kabla ya kuteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kilimanjaro na Mara.

Mwakyoma baada ya kustaafu mwaka 2013, aliingia kwenye siasa, mwaka 2017 aligombea uenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, alikosa na nafasi hiyo ilichukuliwa na Alhaji Omari Shamba.

Katika uchaguzi huo, Shamba alipata kura 170 huku Mwakyoma akiambulia kura 55, Joseph Mtui kura 72 na Faraji Swai alipata kura 84.

Wakati akigombea uenyekiti wa wilaya, tayari alikuwa amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mfumuni, nafasi aliyoishika hadi mwaka 2024 mwanzoni alipoomba kujiuzulu.