Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kada CCM aliyemwagiwa tindikali abisha hodi kwa DPP

Muktasari:

  • Amemuomba DPP aone umuhimu wa kuunda timu huru ya uchunguzi itakayojumuisha wajumbe kutoka vyombo vya haki jinai.

Dar es Salaam. Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kilimanjaro, Idrisa Moses amemwandikia barua Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), akimuomba aitishe jalada la uchunguzi ili kulipitia na kushauri kadri atakavyoona inafaa.

Hata hivyo, barua yake hiyo ya Machi 28, 2025 iliyotumwa kwenda Ofisi ya DPP Dodoma na nakala kutumwa kwa barua pepe, haijamfikia DPP.

DPP Sylvester Mwakitalu alipoulizwa Aprili 25, 2025 na Mwananchi alisema hajaiona barua hiyo lakini akaahidi kufanyia kazi nakala ya barua hiyo aliyotumiwa na Mwananchi kwa njia ya WhatsApp kama rejea.

Moses ameandika: “Ninapokuandikia barua hii leo, zimepita siku 189 (sasa 217) tangu nitendewe unyama huu, hakuna Prime Suspect (mshukiwa) hata mmoja amekamatwa na kufikishwa kortini jambo linaloniweka katika mashaka makubwa,” amedai.

“Ninasema hivyo kwa sababu japokuwa mimi si mtaalamu wa upelelezi, lakini vipo viashiria vya kiini cha mimi kumwagiwa tindikali kuwa vilianzia katika malumbano yalitokea katika kundi la WhatsApp.

“Malumbano yalihusu nafasi ya ubunge katika uchaguzi mkuu 2025 na kwa siku ambazo uchunguzi umefanyika na hakuna washukiwa licha ya uwepo wa viashiria vyote vya waliofanya uhalifu kuwa wazi, inaonekana kuna jambo haliko sawa.”

Kada huyo amemuomba DPP atumie mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 16(2) cha sheria ya usimamizi wa mashitaka namba 27 ya mwaka 2019, kuitisha jalada la uchunguzi ili kupitia ushahidi uliokusanywa na ulikuwa na tija ama la

“Ninakuomba uitishe jalada la polisi la uchunguzi kupitia ushahidi uliokuwa umekusanywa awali pamoja na vielelezo, ili kujiridhisha kama ushahidi huo haukuwa na tija katika kufungua shauri la jinai mahakamani.”

Mbali na ombi hilo, lakini amemuomba DPP aone umuhimu wa kuunda timu huru ya uchunguzi itakayojumuisha wajumbe kutoka vyombo vya haki jinai kwa ajili ya kufanya uchunguzi maalumu juu ya suala hilo kwa mujibu wa kifungu cha 16(2).

“Nimeamua kukuandikia na kukuomba uchukue hatua hizo nikitambua kuwa, bila kitendawili cha tukio hilo kuteguliwa, nina wasiwasi matukio ya aina hii yanaweza kushika kasi zaidi kadri tunavyoelekea katika uchaguzi mkuu Oktoba 2025.

“Ni kwa msingi wa ibara hiyo, ninaomba suala hili lisiishie hewani.”

Akizungumza kwa simu na gazeti hili Aprili 25, 2025 kutoka hospitali alikolazwa akiuguza vidonda baada ya kufanyiwa upasuaji huo, kada huyo amesema kwa ahadi hiyo ya DPP, anaamini kitendawili cha waliomharibu sura kitateguliwa.


Tukio lilivyotokea

Baada ya tukio hilo kutokea na video za kada huyo akipatiwa huduma ya kwanza katika Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi kusambaa katika mitandao, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alijitokeza na kutoa taarifa kuwa polisi wameanzisha uchunguzi.

Kamanda Maigwa alinukuliwa akiwaambia wanahabari kuwa siku ya tukio, Moses ambaye ni dereva bodaboda akiendesha pikipiki yake aina Sinorai namba MC 854 DCB alikodishwa na mtu asiyemjua saa 2:00 usiku kutoka kijiweni kwake.

Mtu huyo alimtaka ampeleke eneo la Njoro katika Manispaa ya Moshi.

Kwa mujibu wa RPC Maigwa, baada ya kufika hilo, abiria aliyembeba alimwambia asimame ili amchukue mwenzake ndipo alipojitokeza kijana mwingine akammwagia kimiminika hicho usoni na kumpora pikipiki yake hiyo aina ya Sinorai.

Baadaye pikipiki hiyo ilipatikana imetelekezwa msitu wa Njoro ambao hauko mbali na eneo la tukio na Desemba 2024, polisi walimrudishia Moses simu yake na pikipiki hiyo wakati wakiendelea na uchunguzi.


Aisubiri kwa hamu THBUB

Machi 5, 2025, Moses aliiandikia Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) akiiomba itumie mamlaka yake ya kikatiba kuchunguza tukio hilo na kuondoa wingu lililogubika kuhusu nani ni wahusika.

Mwenyekiti wa THBUB, Jaji mstaafu Mathew Mwaimu, alipoulizwa Machi alijibu kwa kifupi:"Tumeipokea (barua) na hatua za awali tumeona ni suala ambalo linatupasa kufuatilia na kulifanyia uchunguzi. Nimeshatoa maelekezo."

Katika barua hiyo, kada huyo amedai kwa jinsi sura yake ilivyoharibika, hata watoto wake wadogo, mmoja anayesoma chekechea na mwingine anayesoma darasa la kwanza wanaogopa kumsogelea isipokuwa kama amevaa miwani.

“Ninakuandikia (mwenyekiti) barua hii nikitambua majukumu iliyonayo tume kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 130,” ameeleza kada huyo katika barua hiyo ambayo THBUB ilikiri kuipokea.

“Ibara hiyo imeainisha majukumu ya tume kuwa ni pamoja na (b), kufanya shughuli za kupokea malalamiko ya uvunjaji wa haki za binadamu kwa jumla.

“Lakini ibara ndogo ya (c), tumeitafanya uchunguzi juu ya mambo yanayohusu uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

“Ni kutokana na majukumu hayo mazito ya kikatiba, ninakuandikia barua hii ili tume yako ifanye uchunguzi huru wa tukio langu la kumwagiwa tindikali.”

Moses amesema anatambua Ibara ya 130 ya Katiba haiizuii tume kufanya uchunguzi wowote hata kama jambo linachunguzwa na chombo kingine.

Moses katika barua hiyo, alisema amesukumwa kuiomba tume kuchunguza kutokana na uzito na mazingira ya tukio lenyewe ili ifanye uchunguzi huru na kufahamu nini kilitokea, nani walifanya hivyo na sababu za kufanya hivyo.