Jowuta: Waandishi msibebe vyama, tendeni haki uchaguzi mkuu

Muktasari:
- Katika mafunzo ya kuwajengea uwezo, wanahabari wamehimizwa kuzingatia maadili, usalama wao na kutoa taarifa zisizoegemea upande wowote.
Morogoro. Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (Jowuta), kimewataka viongozi wa vyama vya kisiasa wenye tabia ya kuwasimanga waandishi wa habari wakati wakitimiza majukumu yao, waache kufanya hivyo ili watimize wajibu wao kwa uhuru, hasa kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu.
Chama hicho kimesema ni muhimu waandishi wafanye kazi zao bila mashinikizo na kutimiza malengo ya wananchi kwa kufuata maadili na misingi ya kazi.
Wito huo umetolewa Alhamisi, Aprili 24, 2025, mjini Morogoro na mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Mussa Juma, wakati wa mafunzo kuhusu uchaguzi yaliyowahusisha waandishi wa habari kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.
Mafunzo hayo yanayoratibiwa na Jowuta yamedhaminiwa na Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari (IFJ), Mtandao wa watetezi wa haki za binaadamu nchini (THRDC), Taasisi ya wanahabari ya usaidizi wa jamii za pembezoni (MAIPAC) na Shirikisho la waandishi barani Afrika (FAJ).
Juma amesema viongozi wa vyama vya kisiasa wanapaswa kuwaacha wanahabari kufanya kazi kwa uhuru na kuacha kuwapiga ama kuwazomea kwenye misafara.
Hivyo, amewahimiza wanahabari kuzingatia maadili na weledi katika utendaji wao wa kazi katika kuripoti habari za uchaguzi mkuu kabla, wakati na baada ya uchaguzi huo, bila kuegemea chama chochote cha siasa.
“Tunataka waandishi wasiwe na upendeleo katika vyama vya siasa, watoe fursa sawa kwa vyama vyote kipindi chote cha uchaguzi.
“Tumekutana kuwakumbusha pia suala la usalama wao wakati wa uchaguzi. Ili uchaguzi unapomalizika wabaki salama; jinsi gani wanaweza kujilinda na majanga mbalimbali, tumewaelekeza jinsi ya kujilinda na majanga ya mtandaoni,” amesema Juma.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo waandishi kuripoti uchaguzi mkuu kwa amani, kutoa fursa sawa kwa vyama vya siasa, na kuhakikisha usalama wao wenyewe kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Akitoa mada juu ya ulinzi na usalama kwa waandishi wakati wa uchaguzi, Juma amewataka wanahabari kujali usalama wao na usalama wa vyombo vyao vya kazi wakati wa uchaguzi na kabla.
“Kabla hujaandika habari fanya tathimini ya habari yako, inawagusa kina nani, je ina athari gani na kama ina vitisho chukua tahadhari,” amesema.
Awali, akifungua mafunzo hayo, Ofisa Uchaguzi wa Manispaa ya Morogoro, Shabani Duru, amewasisitiza wanahabari kuwa na ushirikiano wa karibu na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) wakati wa kutekeleza majukumu yao kwenye mchakato mzima wa uchaguzi mkuu.
Mwakilishi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Wakili Jones Sendodo, akitoa mada juu ya sheria za uchaguzi na kuripoti habari za uchaguzi, amewataka wanahabari kuzijua sheria pamoja na kuzingatia ukweli, usahihi na masuala ya jinsia.
Pia amewataka wanahabari kutambua umuhimu wa usalama wao kazini na kujua kuwa kuna vyombo vya kuwatetea wanapokabiliwa na majanga.