Jinsi ya kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia
Muktasari:
Mkurugenzi wa Wildaf Anna Kulaya amewataka wananchi kila mmoja kuhakikisha anapinga vitendo vya ukatili wa akisema bado kuna changamoto licha ya jitihada za Serikali
Dar es Salaam.Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la Wildaf, linalojishughulisha na wanawake,sheria na maendeleo Afrika, Anna Kulaya amesema jukumu la kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ni la kila mwananchi kuanzia ngazi ya mtu mmoja hadi Taifa.
Kulaya amesema hayo leo Alhamisi Novemba 26, 2020 wakati akifungua mjadala wa Jukwaa la Fikra la nane lenye mada ya 'tupinge ukatili wa kijinsia mabadiliko yaanza na mimi'.
Jukwaa hili linafanyika katika ukumbi wa Kisenga na kurushwa mubashara na kituo cha ITV na Redio One pamoja na mitandao ya kijamii ya Mwananchi.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya inayoshughulikia masuala ya jinsia imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ikiwamo kuweka madawati ya jinisia katika kupambana na hali hiyo lakini bado changamoto haijaisha.
" Bado tuna wajibu na jukumu kwa kila mtu kuhakikisha anapiga vitendo vya ukatili wa jinsia kuanzia ngazi ya mtu binafsi, waliopo kwenyw mahusiano, jamii hadi Taifa," amesema Kulaya.
Kulaya amezungumzia suala la kampeni ya siku 16 kupinga ukatili wa jinsia akisema imekuwa na mafanikio mengi kwa kuwa ni sehemu mojawapo ya kuangalia fikra na mtizamo na makuzi ili kujua yanasaidia kwa kiasi gani ukatili wa kijinsia.