Sababu kampuni ya Mwananchi kuanzisha Jukwaa la Fikra yatajwa

Muktasari:
Kaimu mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communication Ltd (MCL), Bakari Machumu ameeleza sababu za kampuni hiyo kuanzisha mjadala wa jukwaa la fikra kwamba umelenga kutafuta suluhisho na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
Dar es Salaam. Kaimu mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communication Ltd (MCL), Bakari Machumu ameeleza sababu za kampuni hiyo kuanzisha mjadala wa jukwaa la fikra kwamba umelenga kutafuta suluhisho na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
Machumu ameeleza hayo leo Alhamisi Novemba 26, 2020 wakati akifungua mjadala wa jukwaa hilo la nane lenye mada ya 'tupinge ukatili wa kijinsia mabadiliko yaanza na mimi' linalorushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha ITV na Redio One pamoja na mitandao ya kijamii ya Mwananchi.
Machumu amesema kwa mwaka mmoja Mwananchi imekuwa ikiendesha mijadala ya jukwaa la fikra ambalo limejitofautisha na mengine kutokana na kujikita kwenye suluhisho ya changamoto.
"Hili ni jukwaa la nane tulianza mada za magonjwa yasiyoambukizwa, uendelezaji wa viwanda, mazingira, kilimo, elimu na ajira, tatizo la corona na utalii na leo tunaangazia masuala ya jinsia.”
"Kama nchi tunajivunia tupo mahali pazuri tumepiga hatua licha ya kuwepo kwa changamoto. Tunajivunia kuwahi kuwa na spika mwanamke pamoja na makamu wa rais, naamini leo tutakuwa na mjadala nafasi ya mwanamke na uongozi," amesema Machumu.