Ukifikiria wingi matukio ya ukatili wa wanawake, watoto kichwa kinauma

Muktasari:
Mwanamke mmoja kati ya watatu duniani amepitia ukatili wa kijinsia au unyanyasaji wa namna yoyote katika kipindi cha maisha yake.
Dar es Salaam. Mwanamke mmoja kati ya watatu duniani amepitia ukatili wa kijinsia au unyanyasaji wa namna yoyote katika kipindi cha maisha yake.
Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia (WB), hadi mwaka 2019 asilimia 35 ya wanawake ulimwenguni kote wamepitia unyanyasaji wa kingono au ukatili wa namna nyingine kutoka kwa watu hao wa karibu watu wengine.
Takwimu hizo zinabainisha kuwa asilimia saba ya wanawake waliofanyiwa ukatili wa kingono walifanyiwa na watu wasio wapenzi wao. Wakati huohuo asilimia 38 ya mauaji ya wanawake hufanywa na wapenzi/watu wao wa karibu.
Katika tukio la hivi karibuni lililotokea nchini Novemba 15, 2020 mkoani Morogoro mwanamme aliyefahamika kama Yakobo Tahoro (38) aliuawa na wananchi baada ya kubainika kuwa alitaka kumuua binti yake kwa miaka tisa.
Binti huyo ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la pili katika kijiji cha Kibedya aliwahishwa na kulazwa katika Kituo cha Afya Gairo baada ya kukatwa na sime shingoni na baba yake mzazi tukio linalohisishwa na imani za kishirikina.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa amesema kuwa baada ya baba huyo kumjeruhi binti yake kwa lengo la kumuua alikamatwa wananchi na kushambuliwa kwa kupingwa na alipofikishwa hospitali alifariki dunia.
Katika tukio jingine lililotokea Kigoma ambapo mahakama kuu ilimwachia huru mkazi wa Kambi ya Wakimbizi Nduta wilayani Kibondo, Hassan Sedekia, aliyekuwa akitumikia kifungo cha miaka 30 jela, kwa kosa la kufanya ngono na binti yake, baada ya kutilia mashaka ushahidi wa binti huyo.
Sedekia alihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama ya Wilaya ya Kibondo, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kufanya ngono na bintiye, kinyume cha kifungu cha 158 (1) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu.
Katika hukumu hiyo, Mahakama ya Wilaya Kibondo ilimtia hatiani mzazi huyo baada ya kuridhika kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa bila kuacha mashaka yoyote.
Vilevile katika aina nyingine ya ukatili, ni ukeketaji ambapo takwimu za WB zinakadiria takribani wanawake milioni 200 duniani kote wamekeketwa.
Takwimu za nchini zinazotolewa na katika utafiti wa Idadi ya Watu na Afya na Kiashiria cha Malaria (DHS) ya mwaka 2015/16 ilionyesha kiwango cha ukeketaji kilipungua kutoka asilimia 18 mwaka 1998 hadi asilimia 10 mwaka 2015/16.
Licha ya takwimu hizo, ipo mikoa yenye idadi kubwa zaidi ya uwiano wa wanawake waliokeketwa, kwa mfano, Manyara inafikia asilimia 58, Dodoma asilimia 47 na Arusha asilimia 41 na mikoa mingine ikiwa na uwiano usiozidi asilimia 30.
Katika mikoa yote mitano ya Zanzibar, Kigoma, Katavi, Rukwa, Ruvuma na Kagera uwiano wa wanawake waliokeketwa ni chini ya asilimia moja.
Masuala haya si ya kuumiza tu kwa waathirika na familia zao, lakini pia yana athari kubwa za kijamii na kiuchumi. Katika baadhi ya nchi duniani unyanyasaji dhidi ya wanawake unakadiriwa kugharimu nchi hadi asilimia 3.7 ya Pato la Taifa – ambapo ni zaidi ya mara mbili ya kile Serikali nyingi hutumia katika elimu.
Kushindwa kushughulikia suala hili pia kuna athari kubwa katika siku zijazo. Baadhi ya tafiti zimeonyesha kuwa watoto wanaopitia ukatili wana uwezekano mkubwa wa kuwa waathirika au watuhumiwa katika siku za mbeleni.
Taarifa ya Benki ya Dunia ina sema unyanyasaji huu una sifa ya kutojali mipaka ya kijamii au kiuchumi na inaathiri wanawake na wasichana wenye kipato cha aina yoyote na kupendekeza suala hili linahitaji kushughulikiwa katika nchi zote zile zinazoendelea na zilizoendelea.
Kupunguza unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana inahitaji ushiriki wa jamii na ushiriki endelevu wa wadau wengi.
Katika kutambua haya Tangu mwaka 2003, Benki ya Dunia imeshirikiana na nchi na washirika mbalimbali duniani kusaidia miradi na warsha za kuongeza maarifa zilizolenga kupambana dhidi ya matukio ya unyanyasaji.
WB inasaidia zaidi ya dola milioni 300 za Marekani katika miradi ya maendeleo inayolenga kupingana na ukatili dhidi ya makundi hayo.
Ukatili dhidi ya watoto
Katika miaka ya karibuni kumekuwepo na ongezeko kwa baadhi ya matukio ya ukatili dhidi ya watoto kama ilivyobainisha mwanzo wa habari hii. Kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polisi matukio ya utelekezaji wa watoto yaliongezeka hadi kufikia 148 mwaka 2019 ukilinganisha na matukio 112 mwaka uliopita.
Wakati huohuo, takwimu za Tamisemi, idadi ya wanafunzi wanaoacha shule kwa sababu ya kupata mimba katika shule za sekondari na msingi inaongezeka.
Wanafunzi wa kike wa shule za msingi nchini walioacha shule kwa sababu hiyo waliongezeka kwa zaidi ya mara nne mwaka 2017 hadi 1,040, ukilinganisha na wanafunzi 251, mwaka 2015. Idadi hiyo ni takribani mara mbili ya wanafunzi hao mwaka 2016 ambo walikuwa 594.
Vilevile kwa shule za sekondari kulikuwa na ongezeko la asilimia 55.1 la wanafunzi waliopata mimba wakiwa shuleni na kufikia idadi ya wanafunzi 5,336 mwaka 2017 kutoka wanafunzi 3,439 mwaka 2015. Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 20 ukilinganisha na wanafunzi 4,442 waliopata mimba mwaka 2016.
Matukio ya wizi wa watoto yalipungua hadi kufikia matukio 89 pekee mwaka 2019 kutoka 113 mwaka 2018.
Jitihada
Utafiti wa ukatili dhidi ya watoto Tanzania na Mpango wa kitaifa wa kudhibiti ulio chini ya uongozi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto unapendekeza ushirikishwaji wa sekta mbalimbali kuanzia sheria na polisi, afya, elimu, ustawi wa jamii, asasi za kiraia, jamii na wana habari katika kupambana na ukatili.
Pia kulipendekezwa, kuanzishwa na kutumika kwa mfumo wa kisheria utakaosaidia kulinda watoto dhidi ya ukatili, udhalilishaji na unyanyasaji, ambao utaendana sambamba na sheria ya mtoto na 21 (2009), huduma yenye kujumuisha masuala mengi ya kiafya inatolewa kwa watoto waliofanyiwa ukatili na udhalilishaji.