Jela miaka 60 kwa kumlawiti na kumbaka bintiye

Muktasari:
Mshitakiwa Ally Musa mkazi wa kijiji cha Kidete wilayani Sikonge ukumiwa kifungo miaka 60 kwa kumbaka na kumlawiti binti yake wa kumzaa, mwenyewe aanguka mahakamani.
Tabora. Ally Musa mkazi wa kijiji cha Kidete wilayani Sikonge, amehukumiwa kifungo cha miaka 60 baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka na kumlawiti binti yake mwenye umri wa miaka saba.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatatu Desemba 12, 2022 na Hakimu Jovin Katto, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi wanne wakiwamo wa Jamhuri, mwathirika mwenyewe wa tukio hilo na daktari aliyemfanyia uchunguzi.
Akisoma hukumu ya kesi hiyo, Hakimu Katto amesema kuwa shahidi wa kwanza ambaye ni mwathiriwa wa tukio hilo (jina linahifadhiwa), aliiambia mahakama kuwa mshitakiwa alimwingizia uume wake sehemu za siri.
Upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili Alice Thomas umedai mahakamani hapo kuwa Februari, 20, mwaka huu, mshitakiwa alimbaka na kumlawiti mtoto wake wa kumzaa mwenye wa miaka saba.
Amesema kuwa siku hiyo mshitakiwa ambaye ni baba mzazi wa mlalamikaji kabla ya kutenda makosa hayo, alimchukua mtoto huyo nyumbani kwa mama yake Tausi Daudi, akisema anakwenda kumnunulia madaftari.
Wakili Thomas ameongeza kuwa mshitakiwa ambaye alikuwa akitumia usafiri wa pikipiki, alimwingiza kichakani mtoto huyo na baada ya kutenda unyama huo, alishindwa kumrejesha nyumbani kwa mama yake.
Ushahidi wa daktari aliyemfanyia vipimo vya kitabibu umeonyesha kuwa mtoto huyo alikuwa akitokwa damu ukeni kwake na pia alikuwa na mchubuko sehemu ya kutolea haja kubwa.
Upande wa Jamhuri uliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa Mshitakiwa kwa kuzingatia matakwa ya sheria kwa vile mhanga wa tukio hilo ni mtoto chini ya miaka 10.
Kufuatia ombi hilo la Jamhuri, mahakama hiyo imemuhukumu mshitakiwa kifungo cha jumla ya miaka 60 jela kwa makosa yote mawili, lakini atatumikia adhabu ya kifungo cha miaka 30 kwa vile adhabu hizo zinaenda pamoja.