Jela miaka 30 kwa kubaka, kumpa ujauzito mwanafunzi
Muktasari:
- Mahakama imemhukumu mshtakiwa kifungo cha miaka 30 jela na kulipa fidia ya Sh300,000 kwa muathirika.
Simiyu. Mahakama ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela, Luth Jacobo (50), mkulima wa kijiji cha Mwanundi, kata ya Sengwa wilayani humo, baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka 15 (jina linahifadhiwa) na kumsababishia ujauzito.
Hukumu hiyo ilisomwa leo Jumanne, Septemba 9, 2025 na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Enos Misana, katika kesi ya jinai namba 12270/2025.
Mshtakiwa alitiwa hatiani kwa kosa la kubaka kinyume na kifungu cha 130(1), (2)(e) na 131(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marejeo ya mwaka 2022.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Wakili Mwandamizi Vailent Mushumbusi, akisaidiana na Mkaguzi wa Polisi Vedastus Wajanga, katika hati ya mashtaka iliyowasomwa mahakamani hapo, imeeleza kuwa Oktoba 2023, usiku, mshtakiwa alimuingilia mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi na mtoto wa mdogo wa mke wake.
Mashahidi sita pamoja na kielelezo kimoja (fomu namba tatu ya polisi ya muathirika) waliwasilishwa mahakamani ushahidi wao kuthibitisha shtaka hilo.
Baada ya tukio hilo, Januari 26, 2024, mshtakiwa alikamatwa na mtendaji wa kijiji cha Mwanundi kwa kushirikiana na Sungusungu, mtendaji wa kata na walimu wa shule ya msingi Mwanundi, kabla ya kukabidhiwa polisi na kufikishwa mahakamani.
Katika utetezi wake, mshtakiwa alidai kuwa kesi hiyo amembambikizwa na kwamba anamwachia Mungu, madai ambayo Mahakama ilikataa baada ya ushahidi wa upande wa mashtaka kuthibitisha kosa bila kuacha shaka.
Hakimu Misana amesema kuwa Mahakama imemkuta mshtakiwa na hatia kulingana na ushahidi uliotolewa dhidi yake.
“Mahakama hii imethibitisha bila kuacha shaka kuwa mshtakiwa ametenda kosa. Kitendo hiki si tu ni ukatili wa kijinsia, bali pia kimeacha doa kubwa katika maisha ya muhanga na jamii kwa ujumla,” amesema.
Kutokana na hilo, Mahakama ilimhukumu mshtakiwa kifungo cha miaka 30 jela na kulipa fidia ya Sh300,000 kwa muathirika.
Awali, upande wa mashtaka uliomba adhabu kali itolewe ili iwe fundisho kwa mshtakiwa na onyo kwa wengine katika jamii.