Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jela kwa kubaka na kumpa mimba mwanafunzi

Muktasari:

  • Mahakama imemuhukumu mshtakiwa wa ubakaji kwenda jela miaka 30 kwa kila kosa, na kuelekeza kwamba adhabu hizo zitaenda kwa pamoja na hivyo atatumikia miaka 30.

Mwanza. Mahakama ya Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela mkazi wa Kijiji cha Kinamweli, Iddy Makungu (30) kwa kosa la kubaka na kumpa ujauzito mwanafunzi mwenye umri wa miaka 14.

Hukumu hiyo imetolewa jana Jumanne Aprili 8, 2025 na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ndeko Dastan Ndeko, ambaye amesema mtuhumiwa atahukumiwa kifungo cha miaka 30 kwa kila kosa, na adhabu hizo zitakwenda pamoja, hivyo atatumikia kifungo cha jumla cha miaka 30 jela.

Hakimu Ndeko amesema kuwa Iddy alitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Aprili na Mei, 2024, katika Kijiji cha Kinamweli, wilayani Kwimba.

Hakimu Ndeko ameeleza kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo katika kesi ya jinai namba 31962 ya mwaka 2024, kinyume na vifungu vya 130(1)(2)(e) na 131(1) vya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, Marejeo ya mwaka 2022.

Mbele ya Mahakama, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Juma Kiparo, amesema mshtakiwa alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani Novemba 11, 2024, ambapo alisomewa mashtaka ya kubaka na kumpa mimba binti huyo, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Kinamweli.

Upande wa mashtaka ulileta mashahidi watano, akiwemo mwanafunzi huyo mwenyewe na Mahakama ilijiridhisha pasipo na shaka kuwa mtuhumiwa alitenda makosa hayo.

Hata hivyo, Iddy alikana kutenda makosa hayo, akijitetea kwa kusema kuwa amesingiziwa, kwani awali alikuwa akifanya kazi ya kuchunga ng'ombe kwa mjomba wa binti huyo.

"Mheshimiwa Hakimu, nimesingiziwa kesi hii baada ya kudai pesa zangu za mshahara nilizochunga ng'ombe," alijitetea.

Baada ya kusikiliza utetezi huo, Mahakama ilitupilia mbali madai yake kwa kutokuwa na mashiko na kumhukumu kifungo cha miaka 30 jela kwa kila kosa. Hakimu alielekeza kuwa adhabu hizo zitakwenda kwa pamoja, hivyo Iddy atatumikia kifungo cha jumla cha miaka 30.