Jatu mikononi mwa Takukuru, wenyewe wafunga ofisi

Wakati Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe
Muktasari:
- Wakati Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akitangaza kuipeleka kampuni ya Jenga Afya Tokomeza Umasikini (Jatu) katika Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), hofu imetanda miongoni mwa wakulima wanaodai kupoteza mabilioni ya fedha katika kampuni hiyo.
Dar/Mbeya. Wakati Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akitangaza kuipeleka kampuni ya Jenga Afya Tokomeza Umasikini (Jatu) katika Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), hofu imetanda miongoni mwa wakulima wanaodai kupoteza mabilioni ya fedha katika kampuni hiyo.
Aprili mwaka huu Waziri Bashe alikutana na wawakilishi wa wakulima na viongozi wa JATU jijini Dodoma, na baada ya kusikiliza madai ya pande mbili, aliunda kamati kwa ajili ya kukagua mashamba yanayodaiwa kulimwa na kampuni kwa ajili ya wakulima waliotoa fedha.
Akizungumza hivi karibuni jijini Dodoma na baadhi ya wanachama wa kampuni hiyo kuhusu ripoti ya kamati hiyo, Waziri Bashe alisema walichokiona kiko nje ya uwezo wao, hivyo wanawakabidhi ripoti Takukuru.
“Mahali ilipofika hili jambo kwetu sisi Wizara ya Kilimo it’s over and above (tumefika mwisho na liko juu yetu). Ndiyo maana leo nimeongea na DG (Mkurugenzi) wa Takukuru nikamwomba watu ili sisi tukabidhi tulichopata,” alisema Bashe.
Alieleza kusikitishwa na menejimenti ya JATU kufunga ofisi ya Morogoro, Dar es Salaam na Dodoma akisema wamehamia Rukwa.
“Tumekubaliana na DG wa Takukuru ataongea na IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi), ataongea na Financial Intelligence Unit wote watakutana na kuunda timu,” alisema.
Bashe pia alieleza kusikitishwa na uongozi wa JATU kukatataa kuhudhuria mkutano huo, akisema walimwamweleza kuwa watakutana Septemba.
Malalamiko ya wanachama
Akizungumza hivi karibuni kupitia mtandao wa Zoom, mwenyekiti wa wanachama wa JATU wanaoishi nje ya nchi, Shukrani Magoma, alisema waliamua kuwekeza kwenye kampuni hiyo baada ya kujiridhisha kuwa imesajiliwa na vyombo vya Serikali.
“Tulivutiwa baada ya kuona kuwa JATU inatambuliwa na taasisi nyeti za Serikali na baada ya kushawishiwa na viongozi wa Serikali wanaotembelea nchi hizi wakitaka tuwekeze nchini kwetu,” alisema anayeishi nchini Marekani.
Katika umoja huo, Magoma alisema wako watu 27 wanaoishi Marekani, Uingereza, Saudi Arabia, Dubai, Ubelgiji, Ufaransa Ujerumani, Ethiopia na Korea ya Kusini.
“Changamoto tuliyokutana nayo ni wakati wa malipo, ambapo JATU wamekuwa wakikwepa kutekeleza jukumu lao. Badala yake JATU wamekuwa wakitoa ahadi na tarehe za malipo na muda wa malipo, lakini hawalipi,” alisema Magoma.
Alisema kutokana na JATU kushindwa kulipa, wengi wao walilazimika kuwekeza zaidi kile walichokuwa wakiidai kampuni wakitumaini kuwa miaka ya mbele JATU itaweza kulipa. Matokeo yake ndiyo imekuwa kulimbikiza mitaji ya miaka yote ambayo mpaka sasa hawajalipwa.
“Tunadai malipo baadhi yetu ikianzia msimu wa 2019/20, Misimu ya mwaka 2020/2021 na 2021/2022 pia haijalipwa. Kwa mazao yaliyokwishavunwa, tunaidai JATU zaidi ya Sh1.05 bilioni,” alidai.
Juhudi za kuupata uongozi wa JATU kuzungumzia suala hilo, hazikufanikiwa baada ya msemaji wake ambaye pia ni mkurugenzi wa sheria wa kampuni hiyo kutopokea simu wala kujibu ujumbe mfupi.
Mwananchi pia lilimtafuta Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni hiyo, Zaipuna Yonah, lakini simu yake ilikatwa na akatuma ujumbe akisema atumiwe ujumbe wa simu, ambao hata hivyo alipotumiwa hakujibu.
Hata hivyo, aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa JATU, Peter Gasaya, akizungumza katika mkutano wa wanachama Juni 25 jijini Dar es Salaam, aliwataka kuingiza madeni yao katika mfumo wa hisa, jambo lililopingwa na wanachama.
Mwananchi pia limefika katika ofisi za JATU zilizopo katika jengo la PSSSF katikati ya Jiji la Dar es Salaam, lakini walinzi waliokuwepo walisema ofisi hizo zimeshafungwa.
Ripoti ya Bashe
Akifafanua kuhusu ripoti hiyo, Bashe alisema JATU imeorodheshwa kwenye soko la Hisa na ililenga kuwekeza kutokana na michango ya wanahisa.
“Lakini sisi wizara kilichotusukuma tuingilie ni the second component (kipengele cha pili) waliyotengeneza, ambayo wanasema leta hela, nakwenda kukulimia maharagwe Sumbawanga, leta Sh5 milioni, 10 milioni, 20 milioni ambazo hazina uhusiano na uwekezaji wa hisa.
“Anaambiwa kwamba nakwenda kukulimia, msimu ukiisha, mimi mwenyewe JATU nitanunua mazao halafu nitakulipa,” alisema.
Alisema kulikuwa na wanachama zaidi ya 1,000 walioleta malalamiko yao wizarani.
“Wengine wameambiwa wanalimiwa Morogoro, wengine wanalimiwa soya Rukwa, wengine waliambiwa mazao yako kwenye maghala Tanga, wengine maeneo mbalimbali, wengine wakiambiwa tumekuvunia maharage yako, tumeyachakata yanauzwa kwa distributors. (wasambazaji)”
Alisema kamati aliyoiunda ilimbetembelea maghala yao, hawakukuta mazao, na mashamba waliyotembelea hayana thamani ya fedha zilizochangwa.
“Tulikwenda mbali zaidi, kuangalia fedha walizokusanya na hesabu zao za benki wana hizo fedha? Hakuna.”
Alitoa mfano fedha zilizokusanywa kwa Watanzania waishio nje ya nchi (diaspora), akisema walikuta zaidi ya Sh4.066 bilioni, ambazo zilipaswa kulipwa kwa wakulima katika msimu wa 2019/20 na 2020/21.
“Baada ya kupitia uhakiki wa taarifa za hesabu za kwao za 2020, imeonekana kampuni hiyo ilikuwa na Sh362 milioni tu ambayo ndiyo mapato yaliyotokana na shughuli za kilimo...’’ alisema.
Takukuru, Soko la Hisa wazungumza
Mwananchi lilipomtafuta kwa simu, Mkurugenzi wa Takukuru, Salum Hamduni, alisema:
“Na mimi nimelisikia kama ulivyosikia, kwa sababu niko nje ya ofisi, sijalipokea rasmi.’’
Naye Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Charles Shirima alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema hawezi kuzungumzia kwa kuwa Waziri Bashe ameshalipeleka kwenye uchunguzi.
“Waziri alisema ameshakabidhi kwenye vyombo vya uchunguzi, sasa nikianza kuzungumza sasa hivi sitaeleweka. Kwa sasa hilo ni suala nyeti, nikilizungumzia nitakuwa nashindwa kulinganisha huku na huku,” alisema.
Mbeya walia
Mbali na wanachama wa diaspora, mkoani Mbeya nako wakulima zaidi ya 400 wamedai kupoteza Sh10 bilioni walizowekeza kwenye kampuni hiyo.
Wakizungumza na Mwananachi juzi kwa nyakati tofauti walidai kuwa madai hayo ni msimu wa kilimo 2020/21 ambapo kampuni iliuza wastani wa tani 333.4 sawa na magunia 333,428 za mazao mchanganyiko.
Mkulima Furahini Mkoma alidai miongoni mwa mazao hayo ni alizeti magunia 1,474, maharagwe (144,402), mpunga (103,768) na mahindi (83,784) na kwamba tangu yaingizwe sokoni hawajalipwa madai yao.