Jamii ya watu wasioona kuanza kunufaika na elimu ya Lishe bora

Muktasari:

  • Jamii ya watu wasiona nchini wataanza kunufaika na elimu ya Lishe bora,baada ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kuzindua vitabu rafiki kwa watu wa aina hiyo vinavyotoa muongozo wa kuzingatia aina  ya chakula ili  kujenga afya zao na kujikinga na magonjwa ya Utapiamlo.

Dar es Salaam. Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wamezindua Vitabu wiwili maalumu vyenye ujumbe wa lishe bora kwa jamii ya watu wasioona nchini.

 Vitabu hivyo vilivyoandikwa kwa mfumo wa nukta nundu vinalenga kuhamasisha watu wa jamii hiyo kupata elimu kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa ustawi ukuaji, na maendeleo ya watoto na afya ya watu wote.

Akizungumza Dar es Salaam Machi 21, 2023, baada ya uzinduzi huo Kaimu Mkurugenzi wa idara ya mafunzo na elimu ya lishe, Dk Esther Nkuba amesema jamii hiyo imekuwa ikikabili na changamoto ya upatikanaji wa taarifa sahihi za lishe.

“ kwa sababu taarifa nyingi zinazoelezea lishe zimeandikwa katika mfumo wa maandishi ambao hawawezi kuyaona wala kuyasoma, hivyo tumezindua vitabu viwili vikiwa na maandishi ya nukta nundu na sauti ili kutoa elimu kwao,”amesema

Dk Esther amesema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo imekuwa ikitoa elimu kwa jamii kuzingatia lishe bora ili kuepukana na magonjwa ya utapiamlo wa aina zote.

“Tumekuwa tukiyafikia makundi mbalimbali ya wanawake wajawazito,watoto wachanga,vijana balee na wazee lakini jumuiya ya watu wasiona walikuwa na changamoto hiyo hivyo tumeandaa ujumbe huu,”amesema

Kwa upande wake Sarah Gibson ambaye ni  Mkurugenzi na Mwakilishi wa WFP,nchini amesema wanaunga  mkono juhudi za dhati zinazofanywa na serikali kuona jamii yake inazingatia lishe bora huku akieleza hata shirika hilo linatambua ilikuwe na nguvu kazi  ya kutosha katika ujenzi wa Taifa lolote ni lazima kuwe na jamii ya watu wenye afya nzuri.

“ Tumefadhili mpango huu wa kuandaa vitabu, sauti na redio zitakazotolewa kwa jamii ya watu wasioona ili wapate elimu ya kuzingatia lishe bora,”amesema Sarah

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya watu wasioona Tanzania,Omary Itamba ameshukuru kwa kuwapatia vitabu hivyo huku akiwaomba wafadhili kuangalia namna ya kuwafikia hata wanaoishi vijijini.

“Tunashukuru kwa kutukumbuka kwa sisi tunaoishi mijini ni rahisi kupata vitabu hivi kusoma ujumbe lakini kwa waoishi vijijini ambako wako wengi ni ngumu na jumuiya haina raslimali fedha za kusaidia,”amesema Itamba

Itamba amesema waliopo vijijini wanachangamoto kubwa hata kusoma hawajui hivyo wanatakiwa kusaidiwa zaidi ili wanufaike na elimu hiyo itakayo wawezesha kulinda afya zao.