INEC yabaini watu kujiandikisha zaidi ya mara moja Dar

Muktasari:
- Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na.1 ya Mwaka 2024 kujiandikisha zaidi ya mara moja ni kosa la jinai, atakayetiwa hatiani adhabu yake ni faini isiyopungua Sh100,000 na isiyozidi Sh300,000 au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili gerezani au vyote kwa pamoja.
Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ikiendelea kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura mkoani Dar es Salaam, imesema kumejitokeza changamoto ya baadhi ya watu kujiandikisha zaidi ya mara moja katika vituo tofauti.
INEC imesema hayo leo Machi 20, 2025 katika taarifa kwa umma kuhusu uandikishaji wapigakura mkoani Dar es Salaam, iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima.
Amesema baada ya uandikishaji kukamilika katika vituo, Tume huchakata taarifa za watu wote walioandikishwa kupitia mfumo maalumu (Automatic Fingerprint Identification System-AFIS), ambao una uwezo wa kuwabaini wapigakura wote waliojiandikisha zaidi ya mara moja.
Kailima amesema Tume pia hufanya kazi ya kulinganisha sura za watu wote waliopo kwenda daftari lengo likiwa kubaini iwapo kuna waliojiandikisha zaidi ya mara moja.
Amesema iwapo itabainika mtu amejiandikisha zaidi ya mara moja jina na taarifa za mtu huyo, hufutwa na mfumo katika vituo vingine na kubakizwa katika kituo cha mwisho alichojiandikisha katika daftari, hivyo, taarifa nyingine zote za awali hufutwa.
“Kwa mujibu wa masharti ya Kifungu cha 114(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na.1 ya Mwaka 2024 kujiandikisha zaida ya mara moja ni kosa la jinai, akitiwa hatiani adhabu yake ni faini isiyopungua Sh100,000 na isiyozidi Sh300,000 au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili gerezani au vyote kwa pamoja, kulipa faini na kifungo gerezani,” amesema.
Kailima amesema baada ya uchakataji wa daftari kwa mfumo wa AFIS watakaobainika kujiandikisha zaidi ya mara moja, orodha yao itakabidhiwa Jeshi la Polisi kwa hatua za kisheria.
“Mpigakura atakayejiandikisha zaidi ya mara moja, mbali ya kutenda kosa anaweza kushindwa kupiga kura kwa kuwa atafutwa katika vituo alivyojiandikisha na kuachwa kituo cha mwisho pengine siyo kituo chake sahihi anachopaswa kupiga kura,” amesema.
Ametoa wito kwa wakazi wa Dar es Salaam kuendelea kujitokeza katika siku nne zilizosalia kufikia Machi 23, 2025. Uandikishaji mkoani hapa ulianza Machi 17.
“Tunaendelea kufuatilia hatua hii kwa karibu ili kila mwananchi anayestahili kuandikishwa au kuboresha taarifa zake apate haki hiyo,” amesema.