Wananchi jiandikisheni kushiriki uchaguzi mkuu

Wananchi wakiwa katika moja ya vituo vya kupigia kura kuchagua viongozi. Picha na Maktaba
Oktoba mwaka huu, Tanzania itafanya uchaguzi mkuu, tukio ambalo ni muhimu kwa kuwa linalotoa fursa kwa wananchi kuchagua viongozi wao.
Hata hivyo, kabla ya kufika kwenye hatua hiyo, kila raia mwenye sifa anapaswa kuhakikisha anajiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura.
Shughuli ya uandikishaji ni hatua muhimu inayompa kila mwananchi haki ya kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia wa kuchagua viongozi watakaowawakilisha na kushughulikia changamoto zao.
Kujiandikisha mapema kunawahakikisha kuwa hakuna mwananchi atakayekosa fursa ya kupiga kura, kwa sababu ya ucheleweshaji au visingizio vya muda wa mwisho.
Hivyo, ni muhimu wananchi wajitokeze kwa wingi katika maeneo yao wanapotangaziwa kuwa maofisa wa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) na wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) wanapatikana kwa ajili ya uandikishaji, ili baadaye waweze kuitumia fursa yao hiyo ya kikatiba.
Watu wengi mara nyingi huibua malalamiko baada ya uchaguzi kwamba walikosa nafasi ya kushiriki kwa sababu hawakujisajili kwa wakati. Hili ni jambo linaloweza kuepukwa endapo kila mwenye sifa atahamasika na kutumia fursa hii mapema.
Uandikishaji wa wapigakura unatoa nafasi kwa kila mwananchi mwenye sifa ya kupiga kura kuwa sehemu ya uamuzi wa kitaifa. Kupiga kura si tu haki ya kikatiba, bali pia ni wajibu wa kiraia ambao unaleta mabadiliko chanya katika jamii.
Kupitia kura zao, wananchi wanaweza kuchagua viongozi waadilifu, wenye maono na wanaoweza kuleta maendeleo yanayolenga kuboresha maisha yao.
Wananchi wasiposhiriki katika uandikishaji wa wapigakura, wanapoteza sauti yao katika uamuzi wa kitaifa. Kiongozi yeyote anayechaguliwa katika uchaguzi anakuwa na mamlaka ya kuamua juu ya masuala muhimu yanayohusu wananchi, ikiwa ni pamoja na elimu, afya, uchumi, miundombinu, na maendeleo ya kijamii.
Ni muhimu kwa kila mmoja kuhakikisha anajiandikisha na kisha kushiriki kikamilifu katika kupiga kura ili kuchagua viongozi wanaowataka.
Hivyo, ndio maana tunahimiza wananchi kwenda kujiandikisha muda utakapowadia katika maeneo yao kulingana na ratiba ya INEC na ZEC.
Serikali, vyombo vya habari, asasi za kiraia, na vyama vya siasa vina wajibu wa kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu umuhimu wa kujiandikisha.
Elimu ya uraia inahitajika ili kuwahamasisha watu kufahamu kuwa kushiriki kwenye mchakato wa uchaguzi huanza na hatua hii muhimu ya kujisajili, hivyo wanapaswa kuwa na moyo wa kizalendo kwa kutumia fursa hii ili kuhakikisha wanakuwa sehemu ya maamuzi yanayoathiri maisha yao ya kila siku.
Wananchi wanapaswa kutambua kuwa uchaguzi ni mchakato wa kidemokrasia unaohitaji ushiriki wao wa dhati tangu mwanzo. Kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura, ni hatua ya kwanza katika kuhakikisha kwamba kila mtu anapata nafasi ya kupiga kura na kuchagua viongozi bora.
Wakati wa kulalamika baada ya uchaguzi hautakuwa na manufaa ikiwa fursa ya kusajiliwa ilipita bila kuchukuliwa kwa uzito unaostahili. Hivyo, tunahimiza kila mmoja aitumie fursa hii ili baadaye asijilaumu kwa kutoshiriki katika mustakabali wa Taifa lake.