IGP abebeshwa kitanzi cha haki

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camilius Wambura
Muktasari:
Siku moja baada ya mkuu mpya wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Camilius Wambura kuingia ofisini, wadau mbalimbali, wakiwemo wanasheria na wanasiasa wamemtaka kusimamia upatikanaji wa haki ndani na nje ya jeshi hilo.
Moshi. Siku moja baada ya mkuu mpya wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Camilius Wambura kuingia ofisini, wadau mbalimbali, wakiwemo wanasheria na wanasiasa wamemtaka kusimamia upatikanaji wa haki ndani na nje ya jeshi hilo.
IGP Wambura amechukua nafasi ya Simon Sirro, ambaye kwa sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe na wadau hao wametumia maono ya Rais Samia Suluhu Hassan na vipaumbele vya IGP huyo kumbebesha zigo la haki.
Mara baada ya kuapishwa Ikulu, Dodoma juzi, Wambura alikwenda kuripoti makao makuu ya jeshi hilo jijini humo na kutumia nafasi hiyo kubainisha vipaumbele vitatu atakavyovipa kipaumbele kwenye uongozi wake.
Wambura ambaye ni IGP wa 11 alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kuhakikisha uhalifu wa aina yoyote unatoweka, kurudisha na kuimarisha nidhamu ndani ya Jeshi la Polisi na kuhakikisha haki kwa raia inatendeka.
Vipaumbele vya mkuu huyo wa polisi vinashabihiana na mtazamo wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye tangu alipoingia madarakani Machi 19 mwaka jana amekuwa anasisitiza haki kwa makundi yote.
Rais Samia kila anapofanya shughuli na vyombo vya dola, likiwemo Jeshi la Polisi, amekuwa akisisitiza umuhimu wa jeshi hilo kutenda haki, kufuata sheria na kanuni, kuacha ucheleweshaji wa upelelezi, vitendo vya rushwa, kuepuka ubambikiaji kesi wananchi na maadili kwa askari kwa ujumla.
Katika kuhakikisha Jeshi hilo linakuwa na ufanisi, Rais Samia baada ya kumaliza kumwapisha IGP Wambura na wasaidizi wake juzi alitangaza kamati ya watu 12 ikiongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman, akiipa jukumu la kumshauri jinsi ya kuboresha utendaji wa vyombo vya dola, likiwemo lenyewe.
Vipaumbele alivyovitaja Wambura vya kupambana na uhalifu, maadili na haki, ni maeneo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wadau mbalimbali, wakiwemo wa kisiasa, hususan jinsi ambavyo jeshi hilo limekuwa likiingilia shughuli za kisiasa kwa kuzuia mikutano yao.
Mbali na hilo, maeneo mengine ambayo yamekuwa yakilalamikiwa ni matukio ya utesaji, vifo vya watuhumiwa mikononi mwa polisi, raia kupotea, vitendo vya rushwa.
Wakati wadau hao wakipigilia mstari vipaumbele vya IGP, katika mazingira tofauti, mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, Jaji Frederick Werema ameweka wazi kuwa hakubaliani na zuio la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kwa sababu Tanzania inafuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana, Werema alisema Sheria ya Vyama vya Siasa imebainisha mazingira yanayosababisha mikutano ya hadhara izuiwe baada ya mamlaka husika kufanya tathmini.
“…Lakini sijui, mimi nimetoka serikalini muda mrefu na sijui assessment (tathmini) inayofanywa na watu waliopewa mamlaka hayo ni ipi. Nilishalisema kwenye mahojiano yangu na kikosi kazi, nikasema sikubaliani nalo na nilitoa sababu nyingi tu, sitazisema hapa,” alisema Jaji Werema bila kuhusisha moja kwa moja na jeshi la polisi ambalo ndilo husimamia zuio hilo la mikutano.
Katika mahojiano hayo yatakayochapishwa katika gazeti hili kesho Julai 23, Jaji Werema alisisitiza kuwa suala la haki jamii ni muhimu na ndiyo maana Katiba ya sasa, rasimu ya Katiba ya Warioba na Katiba Inayopendekezwa, zote zinazungumzia haki jamii kama moja ya tunu za taifa.
Wakati Jaji Werema akisema hayo, Katibu mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alisema IGP anatakiwa afanye kazi ya ziada ya kuwajenga kisaikolojia askari wake na kuwaondoa katika fikra mgando kuwa ni jeshi la mabavu, na badala yake liwe ni jeshi linalotoa huduma kwa wananchi kwa weledi na kuzingatia sheria.
Pamoja na hayo, alisema kwa kauli ya IGP na hatua ya Rais kulipangua Jeshi la Polisi, ana imani nia ya (Rais) kufungua ukurasa mpya katika siasa inaweza kutimia.
“Ukichanganya nia ya dhati ya Rais na vipaumbele hivyo vya Wambura, basi tutakuwa na ukurasa mpya. Rai yetu mageuzi ya Jeshi la Polisi yatakamilishwa vizuri zaidi kwa kuwa pia na mageuzi ya kikatiba, kisheria na kitaasisi,” alisema Shaibu.
Mtazamo wa shaibu unafanana na ule wa James Mbatia, mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi aliyesema “tatizo tuna Jeshi la Polisi ambalo ni la mabavu kwa jina lake na si la huduma kwa wananchi.”
Alisema IGP ana kazi kubwa ya kurudisha mahusiano ya Jeshi na wananchi kwa kuwa polisi peke yao hata vita ya ujambazi hawaiwezi.
“IGP anatakiwa arudishe kipaumbele cha jeshi hilo ambacho ni usalama wa raia na mali zao na katika vipaumbele hivyo, haki ya msingi ya kuishi ni muhimu zaidi,” alisisitiza.
Weledi uwe ndio sifa
Ukiacha hao wanasiasa, wadau wengi, wakiwemo maofisa wa polisi wastaafu na wanasheria, wamemshauri IGP kusimamia dhamira ya Rais ya kukomesha rushwa iliyosimika mizizi na kulifumua jeshi hilo kwa kuweka mifumo imara ya uteuzi wa makamanda wa mikoa, wilaya na wakuu wa vikosi kwa kuzingatia uwajibikaji na weledi badala ya utashi wa mtu.
Wakili Hudson Ndusyepo, aliyewahi kuwa kachero wa polisi, mwendesha mashtaka, amemtaka IGP kupiga vita dhana iliyojengeka kwa raia kuwa kuingia polisi ni bure bali kutoka ni pesa.
Alisema kwa uzoefu anaouona ni kwamba askari wa kizazi cha sasa cha vijana hakiangalii Jeshi la Polisi kama taasisi ya kuwahudumia wananchi.
“Kuna kitu kimejengeka kwa polisi, wanamuona raia kama sehemu ya kuwaingizia kipato na si wa kupata huduma. Lazima IGP mpya apige vita hii dhana iliyojengeka muda mrefu,” alisema.
“Hili akiweza kuliondoa na Jeshi likawa ni la huduma tutakuwa tumesogea sana mbele na kuendana na dira ya Rais wetu. Unamuona kabisa Rais anapata hasira namna baadhi ya trafiki wanavyofanya kazi huko barabarani,” alisema wakili huyo.
Alisema ni lazima IGP abadili utendaji kazi wa polisi na kuwarudisha baadhi yao kwenye mstari kwa kuzingatia Sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA) na Kanuni za jeshi la polisi (PGO).
“Waondokane na ukamataji wa kihuni ambapo polisi hawajitambulishi wala kumweleza mtuhumiwa kosa. CPA na PGO ziko wazi kabisa, unapomkamata mtu polisi ajitambulishe kwa jina na cheo chake na amweleze mtu kuwa uko chini ya ulinzi kwa kosa fulani. Lakini ukamataji wa sasa tunashindwa kuelewa tatizo ni mafunzo au nini,” alihoji.
Wakili mwingine, Stephen Mduma aliungana na Ndusyepo kulitaka Jeshi la Polisi kuachana na utaratibu wa kuajiri askari ambao walifeli, badala yake waajiri wenye weledi na pia kutazama mfumo wa kuwapata viongozi wake kwa kigezo cha uwajibikaji.
Mtazamo huo pia umebainishwa na Rais wa mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume aliyesema katika mabadiliko hayo, jeshi hilo linapaswa kuendeshwa kwa weledi.
“Hii ina maana gani? Kwa maneno rahisi, linatakiwa kufuata Katiba, sheria na kanuni za mwongozo wa utendaji kazi wa Jeshi la Polisi (PGO),” alisema.
Fatma, mwanasheria na mtoto wa Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, alisema iwapo jeshi hilo lingefuata sheria lingekuwa na nguvu inayoheshimika.
“Tatizo wameingizwa kwenye siasa na hivyo kushindwa kujiendesha kitaaluma,” alisema.
Kwa upande wake Hussein Mfinanga wa jijini Dar es Salaam, alisema ujio wa IGP mpya utakuwa na maana endapo atalifumua jeshi hilo na kuwapa wananchi na Rais usingizi kuliko kusikia kila mara mambo mabaya yanayofanywa na polisi kwa raia.
Lakini Haji Sadick, dereva wa magari ya watalii, alimtaka IGP kutoa mafunzo ya huduma kwa wateja kwa askari kwa kuwa wananchi wakienda vituoni, hata bila kujua ana shida gani, anaweza kutolewa kauli kali.
Ofisa mmoja mstaafu wa Jeshi la Polisi ambaye hakutaka jina litajwe, alisema katika miaka ya karibuni kulikuwa na tatizo la uteuzi wa baadhi ya makamanda usiozingatia uwajibikaji na weledi, jambo analodhani litakomeshwa.