IGP Wambura awaonya wahalifu

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camilius Wambura
Muktasari:
- Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camilius Wambura ameanza kazi rasmi kwa kuonya wenye dhamira ya kufanya uhalifu wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Dar es Salaam. Siku moja baada ya kuapishwa kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camilius Wambura ametoa rai kwa wananchi kutoa taarifa iwapo wataona tukio la kihalifu huku akionya wanaojihusisha na vitendo hivyo watachukuliwa hatua.
Akiwa mkoani Arusha kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Wambura amesema ni jukumu la jeshi hilo kulinda viongozi na wananchi.
Hili ni jukumu la kwanza la Wambura akionekana hadharani tangu ateuliwe juzi Jumanne na kuapishwa jana Jumatano Julai 20, 2022 baada ya kuhudumu katika nafasi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa takriban mwaka mmoja.
“Wananchi wawe watulivu, lakini watoe taarifa zozote zile watakapoona kuna viashiria vya kihalifu au uvunjifu wa amani ili kuhakikisha tunashughulikia haraka ili viongozi wetu wawe na furaha ya uwepo wako,” amesema.

Pia, Wambura ameonya raia wenye dhamira ya kufanya vitendo hivyo, akiwataka jeshi hilo litashughulika naye.
Wakuu wa nchi za EAC wanaanza kikoa chao leo na kesho Ijumaa Julai 22, 2022 jijini Arusha.
Wakuu hao na nchi zao kwenye mabano ni, Paul Kagame (Rwanda), Uhuru Kenyatta (Kenya), Yoweri Mseven (Uganda), Evariste Ndayishimiye (Burundi), Félix Tshisekedi (DR Congo) na Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ambaye ni mwenyeji wa mkutano.