Idadi ya watu yafikia milioni 68 Tanzania
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, wkati akiwasilisha taarifa ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/27 bungeni jijini Dodoma leo Alhamis Juni 11, 2026. Picha na Said Khamis
Muktasari:
- Katika kila saa takriban watu 215 waliongezeka Tanzania mwaka 2025.
Dar es Salaam. Idadi ya watu nchini Tanzania imeongezeka kwa takriban asilimia 2.8 ndani ya mwaka mmoja, kutoka milioni 66.27 mwaka 2024 hadi milioni 68.15 mwaka 2025.
Hiyo ni sawa na ongezeko la karibu watu milioni 1.9 ndani ya mwaka mmoja. Kwa siku wanaongezeka takriban watu 5,100, sawa na takriban watu 215 kwa saa.
Hayo yameelezwa leo, Alhamisi Juni 11, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alipowasilisha taarifa ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/27 bungeni jijini Dodoma.
“Kasi ya ongezeko la watu inaendelea kutoa fursa chanya kwa maendeleo ya nchi, ikiwemo upatikanaji wa nguvu kazi ya kutosha na uwezekano wa kuchochea mageuzi ya kidijitali katika shughuli mbalimbali za uzalishaji,” amesema.
Fursa hizo, amesema zinaimarishwa zaidi na uwiano wa kundi la vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35, ambao ni nguzo muhimu ya ustawi wa uchumi wa kisasa.
Pamoja na fursa hizo, Profesa Kitila amesema ongezeko la idadi ya watu linasababisha kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za kijamii na mageuzi katika mifumo ya elimu, mafunzo na utendaji kazi.
“Ni muhimu kutekeleza mikakati mahsusi ya kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli zenye tija katika uzalishaji,” amesema.
Hatua hizo, amesema zitasaidia kuimarisha ubora wa rasilimali watu, kuongeza ushindani wa Taifa katika soko la kimataifa na kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi.
Kwa upande mwingine, amesema kiwango cha utegemezi kinakadiriwa kubaki asilimia 0.87 mwaka 2025 na kupungua kidogo hadi asilimia 0.86 mwaka 2026.
“Hali hii inaonesha kuwa mzigo wa utegemezi bado ni mkubwa kwa kundi la watu wanaozalisha. Hivyo, hatua zaidi zinahitajika kupanua ajira zenye tija na kuongeza uzalishaji,” amesema Profesa Kitila.
Aidha, kwa kuzingatia mwenendo wa ongezeko la watu na kasi ya maendeleo ya kiuchumi, amesema ni muhimu kutekeleza mikakati ya kukuza uchumi jumuishi, inayowahusisha wadau wote muhimu katika kuleta maendeleo, hususan katika sekta za huduma za kijamii na miundombinu ya kiuchumi.
“Kwa muktadha huu, Serikali inatakiwa kuendelea kuwekeza kwa katika sekta za elimu, mafunzo ya ujuzi, lishe bora, afya, maji safi na salama, miundombinu ya barabara, nishati, mawasiliano na teknolojia na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya maeneo ya miji na vijiji,” amesema.
Amesema uwekezaji katika sekta hizo, ni nyenzo muhimu za kuongeza tija, kuboresha ustawi wa wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.