Hukumu ya kifo ya miaka 30 iliyopita, yatekelezwa kwa sindano hatari
Muktasari:
Hukumu ya kifo aliyopewa mkazi wa Alabama aliyepatikana na hatia ya kumuua mwanamke katika tukio la uporaji miaka 30 iliyopita, imetekelezwa jana (Alhamisi).
Washington, Marekani (AFP). Hukumu ya kifo aliyopewa mkazi wa Alabama aliyepatikana na hatia ya kumuua mwanamke katika tukio la uporaji miaka 30 iliyopita, imetekelezwa jana (Alhamisi).
Willie Smith, 52, aliuawa jana saa 8:47 usiku kwa kuchomwa sindano hatari akiwa katika gereza lililo kusini magharibi mwa Alabama.
"Haki imetendeka. Leo usiku, Willie Smith aliwekwa mautini kwa uhalifu alioufanya karibu miongo mitatu iliyopita: utekaji na uuaji unaofanana na wa kisheria kwa msichana asiye na hatia, Sharma Johnson," mwanasheria wa serikali wa Alabama, Steve Marshall alisema katika taarifa yake.
Smith amekuwa akisubiri kutekelezwa kwa hukumu hiyo ya kifo kwa miaka 30 baada ya mwaka 1991 kupatikana na hatia ya kumuua Sharma Ruth Johnson, 22, mjini Birmingham.
Hukumu ya Smith ilizuiwa kwa saa 11 mwezi Februari baada ya Mahakama ya Juu ya Marekani kutoa uamuzi kuwa kumzuia kiongozi wa kidini kuwa pembeni yake wakati wa kutekeleza hukumu hiyo ni kinyume cha sheria.
Tangu wakati huo, maofisa wa magereza walisema watamruhusu mchunguzaji wa Smith awepo katika tukio hilo, lakini wanasheria wake walikuwa wakijaribu kuzuia utekelezaji wa hukumu hiyo ya kifo kwa sababu nyingine.
Walijenga hoja kuwa Smith alikuwa na matatizo ya kiakili na hakuruhusiwa kuchagua njia ya kutekeleza hukumu ya kifo chake.
Mwaka 2018, jimbo la Alabama liliidhinisha matumizi ya gesi ya nitrogen kama njia ya kutekeleza hukumu ya kifo, kuongezea katika matumizi ya sindano hatari.
Kutokana na ulemavu wake wa akili, Smith hakuweza kuelewa kuwa alikuwa na uwezo wa kuchagua njia ya kutekeleza hukumu hiyo ya kifo dhidi yake, wanasheria wake walisema.
Mahakama ya Juu ilikataa ombi hilo la kuzuia hukumu jana na hivyo kuruhusu mchakato wa kumuua kuendelea.
Adhabu ya kifo imeondolewa katika majimbo 23, wakati mengine matatu -- California, Oregon na Pennsylvania -- yamezuia kwa muda.