Prime
Huduma ya utengamao mkombozi kwa watoto wenye ulemavu

Ni maarufu kwa jina la ‘Nyumba ya matumaini’, ambayo imerudisha tabasamu kwa watoto wenye ulemavu kwa zaidi ya miaka 25 sasa.
Kituo hicho kilichoanzishwa mwaka 1996, ambacho kimekuwa kikitoa huduma ya utengamao mkoani Kilimanjaro na maeneo jirani ni tawi la CCBRT Moshi, ambacho kimewawezesha watoto wengi na familia zao kupata huduma bora na kuboresha hali za maisha yao kiuchumi.
Albert Chaki, mtoa huduma kwa watoto wenye ulemavu katika kituo hicho anasema karibu asilimia 90 ya watoto wanaowahudumia wana tatizo la mtindio wa ubongo.
Anasema mtoto hufanyishwa mazoezi tofauti kulingana na uhitaji wake kama mazoezi ya kusimama, kukaa na milalo sahihi.
“Sehemu hii ni muhimu kwa sababu watoto wanaozaliwa na tatizo la mtindio wa ubongo wanakuwa na shida kwenye mijongeo na mikao sahihi. Hivyo, ukimuacha mtoto bila kumuweka kwenye mikao sahihi, ndio unakuwa wale wenye mikao siyo sahihi, anakakamaa vibaya au akijongea anatembea isivyo sahihi.
“Lakini ukimuwahi akapata mazoezi kama haya unakuwa umemsaidia sana. Mama akijifungua ukiona imepita miezi mitatu, minne, mitano shingo ya mtoto haijakaza, miezi sita mtoto hajaweza kukaa na hata anapofikisha mwaka hajaweza kutembea, wahi kumleta kituoni apatiwe matibabu, kwa sababu tunasema samaki mkunje angali mbichi,” anasema Chaki.
Anasema mtoto akianza kufanyiwa mazoezi sahihi ya mijongea, anakuwa na maendeleo mazuri, lakini akichelewa inachukua muda mrefu kuona maendeleo yake.
Kitu wanachozingatia anasema ni vifaa saidizi wakati wa utoaji wa huduma hiyo na kutoa mfano kuna kifaa cha kumsaidia kumsimamisha na kiti mwendo.
“Mtoto kama anahitaji kifaa cha kumsaidia kukaa akiwa na miezi sita, kikakosekana, inakuwa shida ukianza kumfundisha kukaa akiwa na umri mkubwa.
“Tunahamasisha jamii kuhakikisha watoto wanapata vifaa saidizi sahihi mapema, sio kama vile vinavyogawiwa mitaani kwa sababu vifaa tunavyovitoa ni vifaa tiba. Vigezo na masharti lazima vizingatiwe, ni kama vile mtu anapopewa dawa, kwa sababu kile kifaa tiba ni dawa vilevile,” anasema na kuongeza:
“Sio kifaa cha mtoto huyu, unampa na yule na yule kwa sababu kila kifaa kimepimwa kulingana na mahitaji maalumu, sawa na dozi ya dawa. Huwezi kuhamisha dozi ya mtoto huyu kwa mwingine,” anasema.
Anasema vikikosekana vifaa sahihi katika muda sahihi, inaathiri maendeleo ya mtoto na huenda mtoto akabaki kuwa wa kutumia kiti mwendo badala ya kutembea.
Kwa upande wake, Meneja wa kituo hicho, Lucy Kavishe anasema mpaka sasa wameshatoa huduma kwa watu wenye ulemavu na familia zao zaidi ya 18,000.
Anasema kwa kushirikiana na Serikali na wadau wa ndani na nje ya nchi, pia wanatoa huduma katika mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Tanga, Dodoma, Iringa, Shinyanga, Kigoma na Morogoro.
“Hapa kituoni, watoto wenye ulemavu hupatiwa matibabu ya kina wakati wa wiki maalumu ya mazoezi tiba. Programu hii inajumuisha wiki nzima ya mazoezi tiba kwa watoto na jopo la wataalamu (daktari wa watoto, fiziotherapia, wataalamu wa tiba kwa vitendo na mtaalamu wa lishe).
“Pia kunakuwa na kliniki ya vifaa tiba, mafunzo kuhusu lishe na baada ya wiki maalumu ya mazoezi, watoa huduma majumbani na wataalamu wanawafuatilia wateja kwenye jamii kuwapatia mafunzo, ikiwemo jinsi ya kujikwamua kiuchumi, matumizi sahihi ya vifaa na uangalizi wa vifaa vyao saidizi,” anasema.
Pia anasema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama maofisa elimu maalumu wa Halmashauri ya Moshi, watoto wenye ulemavu wamefanikiwa kuandikishwa shule za kawaida na kujumuika na wale wasiokuwa na ulemavu baada ya kupata huduma za utengamao na vifaa tiba saidizi.
Matibabu kwa bima ya afya
Lucy anasema wapo kwenye mchakato kutoa huduma kwa kutumia bima ya afya na wameshaanza kufuatilia Wizara ya Afya, lakini kuna vitu vinahitaji fedha ili waweze kufanya marekebisho yanayoendana na Wizara ya Afya.
Hata hivyo, anasema hata kama kutakuwa na uwezekano wa kutumia bima ya afya, kuna huduma ambazo hazipo kwenye kifurushi. “Mfano mtoto mwenye mtindio wa ubongo hawezi kupata huduma kamilifu kama amepata rehabilition, lakini kifaa hana, sidhani kama kitimwendo zipo kwenye kifurushi.”
Hivyo, CCBRT kwa kushirikiana na wadau wengine wanaendelea kufanya ushawishi kwa Serikali vifurushi hivyo viboreshwe, ili mtoto aweze kupata huduma kamilifu.
Mafanikio utoaji huduma
Pamoja na kuwahudumia watu hao, anasema pia wametoa vifaa saidizi zaidi ya 10,000 kwa watu wenye ulemavu, viti mwendo 3,500, kuboresha uchumi wa familia na kutoa mafunzo kwa wadau na wafanyakazi wa afya wa Serikali zaidi ya 12,000.
Pia kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na wadau mbalimbali, anasema wamewezesha Serikali kuwa na Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Huduma za Utengamao uliozinduliwa mwaka 2021, ili kusaidia mifumo ya utoaji huduma za afya na masuala ya watu wenye ulemavu kuwa jumuishi.
Hata hivyo, anasema changamoto wanazokabiliana nazo ni utegemezi wa wafadhili wa nje kwa zaidi ya asilimia 90, gharama kubwa na upatikanaji wa shida wa vifaa tiba na uchache wa wataalamu wanaotoa huduma ya utengamao.
“Ufadhili huo kutoka kwa wenzetu umepungua kwa kiasi kikubwa, tumelazimika kusitisha baadhi ya huduma tunazozitoa kwa watu tunaowahudumia na kwa watoa huduma wetu,” anasema.
“Changamoto nyingine ni hali duni ya kiuchumi miongoni mwa familia za watoto wenye ulemavu ambao husababisha watoto kushindwa kupata huduma stahiki na kwa wakati pamoja na miundombinu katika majengo kama ofisi, shule, hospitali na katika vyombo vya usafiri kutokuwa rafiki kwa watumiaji wa vifaa saidizi kama viti mwendo.
Vituo vya utoaji huduma
Sabas Kimario, Mfiziotherapia wa kituo cha CCBRT Moshi anasema kuna vituo 30 vya kutoa huduma hiyo katika vituo vya afya na zahanati katika kata mbalimbali ambavyo vipo chini ya Mganga Mkuu wa Halmshauri ya Moshi.
Anasema katika kufanikisha hilo, wamekuwa wakitoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ili waendelea kutoa huduma hiyo katika vituo hivyo.
“Vituo hivi vimekuwa msaada mkubwa, idadi ya watoto wenye changamoto hii wenye umri chini ya miaka mitano wanaongezeka kutokana na kuwepo utambuzi wa awali vituoni,” anaeleza Kimario.
Mbali na kutoa matbabu hayo, Kimario anasema wanaziwezesha kiuchumi familia za watoto hao ili waweze kuwahudumia vizuri watoto wao.
Kituo cha afya Himo
Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Sudi Mohamed anasema wanashirikiana na CCBRT kutoa huduma ya utengamao, kwani baadhi ya watumishi wamefundishwa jinsi ya kutoa huduma hizo.
Muuguzi katika Zahanati ya Manushi, iliyopo Kijiji cha Maushi Kati, Getrude Makoi anasema wanafanya utambuzi kwa watoto wanaozaliwa na changamoto hiyo na kisha kuwashauri waanze huduma ya utengamao CCBT.
Anasema baada ya kuwatambua watoto hao, ikitokea mzazi hampeleki kwenye mazoezi humfuatilia nyumbani ili aendelee na huduma hiyo.
“Kila baada ya miezi mitatu tunapatiwa mafunzo jinsi ya kuwahudumia watoto hawa,” anasema.
Wanufaika wanasemaje?
Debora Lyimo, mwenye mtoto wa miezi saba ambaye bado hajaanza kutambaa, anasema tangu waanze mazoezi katika kituo hicho, sasa anaweza kujigeuza kidogo. Alianza kupata huduma hiyo Julai mwaka huu.
Kwa upande wake, Naomi Mosses, anasema alipojifungua mtoto akiwa na siku moja alipata homa kali na kisha degedege na baadaye alibaini kuwa shingo yake haijakaza akiwa na miezi saba.
“Nilimpeleka kuanza kupata huduma, sasa ana miaka mitano, shingo imekaza na anatembea kwa kushikilia vitu,” anasema.
Mwamva Juma, anasema alipojifungua mtoto wake alikuwa na changamoto ya miguu na mikono kutokuwa na nguvu, lakini baada ya kufanya mazoezi tiba, alianza kutembea akiwa na miaka sita.
Naamini Mosses, mkazi wa Uchira naye anasema mwanawe alikuwa na changamoto hiyo, lakini baada ya kuanza mazoezi sasa anatembea kwa kutumia vitu.
“Nilianza kumpeleka kwenye mazoezi akiwa na miezi saba, sasa ana miaka mitano, lakini bado hajaanza shule,” anaeleza.
Kutokana na tatizo la mwanawe, anasema anashindwa kuchangamana na jamii kwa kuwa analazimika kuwa naye muda mwingi, hali inayomkwamisha kiuchumi.
“Mimi ni fundi nguo, lakini biashara si nzuri kwa kuwa hapa ninapoishi majirani ni wachache,” anasema na kueleza kuwa anapata ushirikiano kwa mwenza wake ambaye anajishughulisha na biashara ya bodaboda.
Rosemary Malya, mama mzazi wa Lameck mwenye umri wa miaka minane anasema alipozaliwa alipata ugonjwa wa manjano, hivyo kulazwa hospitali kwa wiki mbili.
“Tulilazwa KCMC, mtoto alipofikisha miezi mitatu kila nikijaribu kumkalisha alikuwa hakai, viungo vilikuwa vimelegea. Ndugu zangu walishauri niende CCBRT ambako alianza kufanyishwa mazoezi, sasa anaendelea vizuri,” anasema.
Rosemary anasema pia ameelekezwa jinsi ya kuendelea kumfanyisha mazoezi akiwa nyumbani, kwenye mikono kumsugulia mchanga au mchele na kwa mazoezi ya miguu amemtengenezea miti ambayo anaishika anapofanya mazoezi.
“Hata sasa ile kutokwa udenda imepungua, kiti mwendo alichopatiwa kinamsaidia sana,” anasema.
Babu wa mtoto huyo, Josephat Malya anasema kituo hicho kimewasaidia kupata mradi wa mbuzi mbao umemwezesha kujenga choo bora.
“Pia Lameck anapata maziwa nusu kikombe kila siku, mbuzi wakizaa wanawagawa kwa familia nyingine zenye uhitaji,” anasema.