Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mara yapata gari jipya la wagonjwa

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere maarufu kama Hospitali ya Kwangwa ya mjini Musoma, Dk Osimund Dyegura akionyesha baadhi ya vifaa tiba vya kisasa vilivyomo kwenye gari jipya la wagonjwa lilitolewa na Serikali kwa hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa wa Mara. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
Pamoja na Hospitali ya Kwangwa, Chuo cha Maofisa Tabibu Musoma pia kimepata gari moja wakati wa hafla ya makabidhiano yaliyoongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Robert Msalika.
Musoma. Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere maarufu kama Hospitali ya Kwangwa ya mjini Musoma imepokea magari mawili likiwemo moja la kubeba wagonjwa ikiwa ni miongoni mwa mikakati ya kuimarisha na kuboresha huduma kwa wananchi.
Magari hao ni sehemu ya magari manne yanayotarajiwa kupokelewa na hospitali hiyo inayotoa huduma za kibingwa kwa wagonjwa kutoka hospitali za wilaya za Mkoa wa Mara.
Pamoja na Hospitali ya Kwangwa, Chuo cha Maofisa Tabibu Musoma pia kimepata gari moja wakati wa hafla ya makabidhiano yaliyoongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Robert Msalika.
‘’Kutolewa na kukabidhiwa kwa magari haya ni utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuboresha huduma ya afya kila kona ya nchi. Nawasihi viongozi na watendaji katika maeneo yote ya huduma kuhakikisha magari haya yanaleta tija inayokusudiwa ambayo ni wananchi kupata huduma bora, sahihi na kwa wakati muafaka,’’ amesema Msalika
Ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutekeleza ahadi ya kuipatia Hospitali ya Kwangwa magari manne kumaliza upungufu wa magari ya wagonjwa.
‘’Magari mengine mawili ya wagonjwa kwa ajili ya Hospitali ya Kwangwa yatawasili wakati wowote kuanzia sasa; magari hayo tayari yamewasili nchini, Wizara ya Afya inakamilisha mchakato wa usajili,’’ amesema Msalika
Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa Kwangwa, Dk Osimund Dyegura amesema hadi sasa, hospitali hiyo ina magari matatu ya wagonjwa, hivyo inahitaji angalau mengine mawili kukidhi mahitaji.
‘’Kwa wiki, hospitali yetu inatoa rufaa kwa wagonjwa sita kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza; kuna umuhimu wa kuwa na magari ya kutosha ya wagonjwa na tunaishukuru Serikali kwa magari tuliyopokea huku tukisubiri mengine yanayokuja,’’ amesema Dk Dyegura
Amepongeza ubora wa magari mapya ya wagonjwa yaliyokabidhiwa kwa hospitali akisema siyo tu ni ya kisasa kwa mwendokasi, bali pia yana vifaa vyote muhimu kwa huduma za dharura kiasi cha kuwezesha wataalam kufanya hata upasuaji mdogo wakiwa njiani kumkimbiza mgonjwa kwenda hospitali za rufaa kwa matibabu zaidi.
Mkuu wa Chuo Cha Maofisa Tabibu Musoma chenye wanafunzi zaidi ya 400, Dk Gaston Kitira ameishukuru Serikali kwa kukipa chuo hicho gari mpya akisema itarahisisha shughuli za kila siku chuoni hapo.
‘’Kilio na kipaumbele cha chuo chetu sasa ni kupata basi kwa ajili ya safari za mafunzo kwa vitendo katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa Kwangwa umbali wa takriban kilomita saba; lengo ni kuwaondolea wanafunzi adha ya kutumia usafiri wa boda boda na bajaji kwenda na kurudi kutoka kwenye mafunzo kwa vitendo,’’ amesema Dk Kitira