Hospitali ya Mkapa yaanza kufanya upasuaji kwa matundu

Madaktari wa Hospitali ya Kisasa ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma walifanya upasuaji wa matundu madogo ( Laparoscopy surgery)
Muktasari:
Matibabu hayo yanatolewa na madaktari wa Tanzania wanaoshirikiana na madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kutoka Marekani
Dodoma. Hospitali ya Benjamin Mkapa Ultra Modern iliyopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) imeanza kufanya uchunguzi na upasuaji kwa kutumia matundu madogo (Laparoscopic Surgery).
Akizungumza leo Alhamisi Julai 19, 2018 mkuu wa kitengo cha uhusiano na masoko katika hospitali hiyo, Karim Meshack amesema huduma hiyo inatolewa na madaktari wa Tanzania wanaoshirikiana na madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kutoka Marekani.
“Wanawake wenye uhitaji wanahimizwa kufika hospitalini hapa ili wachunguzwe na kupatiwa matibabu. Hii sio kampuni ni huduma ambayo tutaendelea kuitoa siku zote. Hapa hospitali tuna wataalam na vifaa vya kutosha kutoa huduma hiyo," amesema.
Amesema wamewaalika wataalam hao kutoka Marekani kwa ajili ya kuwaongezea ujuzi na kufanya uchunguzi na upasuaji.
Amesema faida ya upasuaji huo, mgonjwa hawi na kidonda kikubwa baada ya kufanyika.
Amesema jana walifanya uchunguzi na upasuaji kwa wagonjwa watatu, leo watawafanyia watatu huku kesho watatu wengine wakitarajiwa kufanyiwa upasuaji huo.