Hospitali binafsi zalalamika majibu ya Covid-19 kuchelewa

Muktasari:
- Hospitali binafsi nchini zimeeleza kuwa kuna ucheleweshaji wa majibu ya Covid-19 kutoka katika maabara ya Taifa jambo linalowalazimu kusubiri hadi siku tatu mpaka nne na wakati mwingine hawapati kabisa majibu.
Dar es Salaam. Hospitali binafsi nchini zimeeleza kuwa kuna ucheleweshaji wa majibu ya Covid-19 kutoka katika maabara ya Taifa jambo linalowalazimu kusubiri hadi siku tatu mpaka nne na wakati mwingine hawapati kabisa majibu.
Wamesema jambo hilo linawafanya washindwe kutoa tiba kwa wakati kwa wagonjwa wanaofikishwa katika hospitali zao.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Agosti 12, 2021 na mkurugenzi wa matibabu Hospitali ya Aga Khan, Dk Harrison wakati akizungumzia mchango wa hospitali binafsi katika kupambana na Covid-19 kwenye mdahalo wa kitaifa kuhusu Covid-19 unaofanyika katika ukumbi wa mwalimu Nyerere JNICC.
“Waziri upo hapa na tutalisema hapa, tunapata wakati mgumu sana tunapokea wagonjwa wenye dalili za Covid-19 na tunapochukua sampuli na kuzipeleka maabara ya Taifa tunasubiri majibu kwa siku tatu mpaka nne na wakati mwingine majibu yanarudi na yanaweza yasirudi hivyo inabidi tuchukue sampuli upya kutuma tena maabara,” amesema Dk Chuwa.
Ametoa mapendekezo kwa Serikali kwamba ni vyema utaratibu mpya ukawekwa ili hospitali binafsi na nyingine zenye changamoto hiyo ikatatuliwa ili kupata majibu kwa haraka kwa kuwa wagonjwa wenye dalili hutengewa eneo maalum hivyo kusababisha maeneo mengine kutumika kwa dharura.
Dk Chuwa amesema wamekuwa wakipeleka sampuli 20 mpaka 30 za kupima Covid-19 kwa siku katika maabara ya Taifa.
“Changamoto kubwa kwetu hivi sasa ilikuwa ni namna ya kuwarudisha vijana wengi pamoja na watu wa mataifa ya kigeni ambao walihitaji kuchanja. Kwa siku Aga Khan tumekuwa tukichanja watu 1000 chanjo ya Covid hivyo sasa tutaweza kuchanja idadi kubwa zaidi,” amesema Dk Chuwa.
Imeandikwa na Herieth Makwetta na Rukia Kiswamba, Mwananchi [email protected]