Prime
Hivi ndivyo Dola inavyowatikisa wakulima wa tumbaku

Dar es Salaam. Uhaba wa Dola nchini umeendelea kuumiza makundi ya watu wakiwemo wakulima wa tumbaku ambao wengi wao mpaka sasa wana mashaka na maandalizi ya msimu ujao wa zao hilo.
Mwananchi Digital imepokea malalamiko ya wakulima kutoka maeneo mengi ya nchi ikiwemo mikoa ya Shinyanga, Mbeya (Wilaya ya Chunya), Tabora na kwingineko kunakolimwa zao hilo.
Diwani wa Kata ya Ulowa inayoongoza kwa kulima tumbaku ndani ya Halmashauri ya Ushetu, Pascal Meyengo alisema wakulima wengi hususani waliouza kwa kampuni ya Mkwawa hali yao ni mbaya, huku akisema kuna wasiwasi msimu ujao ukaenda vibaya kwa kuwa wengi hawajapata pesa za maandalizi.
"Ukipita hata maeneo ya biashara kwa walima tumbaku yamepoa sio migahawa wala baa hamna watu, katika kilimo cha zao hilo huwa tunatumia wasaidizi ambao mikataba yao ni kuwalipa mwishoni mwa Juni, msimu huu hawajalipwa na hali hiyo imesababisha migogoro mikubwa," alisema.
Mkulima wa tumbaku, Makwaya Samweli alisema kila mara amekuwa akipewa ahadi ya uongo lakini amesikia kuwa kuna vyama viwili wameanza kulipwa hivyo matumaini yake ni kuwa na yeye atafikiwa.
Alisema mara zote wakulima wakisaini wanaambiwa kuna shida ya upatikanaji wa Dola, lakini changamoto ni kuchelewa huko kumeanza kuleta athari nyingi za kiuchumi miongoni mwao, "Unakuta mtu alikopa benki kwa makubaliano kuwa atarejesha kabla ya kuisha kwa Julai sasa muda umepita riba zitaanza kutuandama, hali ni mbaya wengi wameanza hata kukimbia familia zao," alisema.
Akilizungumzia hilo, Naibu Mkurugenzi wa Kampuni ya Mkwawa, Richard Sinamtwa alisema kuwa wakulima wanaodai fedha zao watatabasamu wiki hii kwani mipango ya kuwalipa wote imeiva huku akisema suala la uhaba wa Dola ndilo lililosababisha wachelewe kulipwa.
Sinamtwa alisema kwa msimu huu kampuni hiyo ambayo ina mwaka mmoja tu sokoni ilinunua tani 42, 000 ambayo ni karibu asilimia 40 ya jumla tani 124 zilizovunwa katika msimu huu.
"Licha ya uchanga wetu sokoni lakini sisi ndio wanunuzi wakubwa, hapa katikati tuliiomba wizara tulipe kwa Shilingi lakini baadaye wenyewe tukaona tukilipa kwa fedha hiyo mkulima hatapata thamani halisi," alisema Sinamtwa ambaye alisema thamani ya manunuzi yao kwa mwaka huu ni takribani Dola 100 milioni (Sh250 bilioni).
Kuhusu changamoto hiyo ya wakulima kulipwa pesa zao Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema, "Sio kwamba hawajalipwa, mwaka huu uzalishaji umeongezeka na bado hawajamaliza kuvuna, tumezalisha zaidi tani 120,000 za tumbaku, ambayo ni mara mbili ya uwezo wa mfumo uliopo, kampuni ambazo hazijalipa ni kampuni mbili tu," alisema Bashe.
Miongoni mwa kampuni zilizolipa watu wake ndani ya muda uliowekwa ni Alliance One Tobacco Tanzania Limited (AOTTL) ambayo imelipa wakulima zaidi ya 12,000 na vyama vya ushirika jumla ya Dola milioni 71.9 (Sh179.8 bilioni).