Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hiki ndicho alichoamua Jaji kesi ya kina Mdee na wenzake

Dar es Salaam. Katika mfululizo wa hatua kwa hatua wa kesi ya Halima Mdee na wenzake 18 tulikuletea wasilisho la mwisho la mawakili wa wajibu maombi na pia hoja tano, ambazo Mahakama ilisema itajielekeza kuzijibu katika hukumu yake.

Hoja hizo ni kama Chadema, chini ya katiba yake au kanuni, zinakipa nguvu au mamlaka ya kusikiliza kikao cha nidhamu katika mazingira ya dharura, na kama jibu ni ndiyo, kama Mdee na wenzake walipewa haki ya kusikilizwa mbele ya kamati kuu.

Hoja nyingine ni kama walipewa haki ya kusikilizwa mbele ya baraza kuu ambacho ndicho chombo cha rufaa, kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu, baraza hilo lilikiuka kanuni ya kutopendelea na kama maombi hayo yamekidhi vigezo vya kukubaliwa.
 

Usikilizwaji wa dharura

Leo tunakuletea uamuzi wa Jaji Mkeha na kwa kuanza alisema pande zote zilikubaliana kuwa Chadema, chini ya kanuni ya 6.5.1 ya katiba yake ya mwaka 2019 ina mamlaka ya kuendesha kikao cha nidhamu kwa dharura.

“Ni msimamo wa waleta maombi kuwa udharura ulikoma baada ya kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu Novemba 24, 2020. Lakini mjibu maombi wa kwanza alisema hata baada ya kuapishwa bado lilikuwa lina udharura,” alisema.

“Kulingana na mjibu maombi, chama kilitaka kujinusuru na mgawanyiko, hivyo mgogoro huo ulihitaji kushughulikiwa kwa dharura,” alieleza Jaji Mkeha.

Jaji alisema Mdee na wenzake walikiri kupokea wito uliowataka kufika mbele ya kamati kuu, wakati pia waombaji hao waliomba kikao kiahirishwe ili wapate muda wa kutosha kujibu tuhuma na sababu za kiusalama.

“Pamoja na sababu za tishio la usalama walilolisema, hakuna hata mmoja miongoni mwa Mdee na wenzake aliyetoa taarifa kwa vyombo vya usalama,” alisema.
 

Matamshi ya Mbowe, Mnyika

“Pia waombaji walikuwa wanalaani matamshi yaliyotolewa na mwenyekiti wa taifa na katibu mkuu wa Chadema kabla ya kikao cha kamati kuu na baraza kuu kwamba yalikuwa kama yameshatoa hukumu, lakini yalipingwa na Chadema,” alisema.

Katika kuamua hoja, Jaji alisema ameona kanuni zilizotumika kuwafukuza zilifuatwa sawasawa na kamati kuu ya Chadema, na mahakama haina mamlaka ya kuingilia ingawa inaona waliopiga kura wanaweza kufikia hitimisho baya.

“Mzigo wa kuthibitisha uwapo wa nia njema upo, kwani mtu anatuhumu kuwa alifukuzwa kimakosa,” alisema Jaji na kunukuu katiba ya Chadema inayoelezea hatua na mchakato wa mwanachama kufukuzwa uanachama.
 

Katiba ya Chadema

“Ibara 5.4.3 na 5.4.4 vya katiba ya Chadema inatoa mamlaka ya kufukuza. Mamlaka hayo yanaweza kutumika dhidi ya mwanachama yeyote kama kutatokea lolote katika makosa ambayo yameorodheshwa na katiba ya chama hicho,” alisema.

“Katika mazingira ya kawaida chini ya ibara ya 6.5.1(a) na (b) vinaeleza kabla hatua za kinidhamu hazijachukuliwa, mwanachama lazima ajulishwe tuhuma zake kwa maandishi na atapewa muda wa wiki mbili kuzijibu,” alisema.

“Novemba 25, 2020 katibu mkuu aliwapelekea wito waombaji kufika mbele ya kamati kuu,” alisema Jaji na kunukuu barua ya John Mnyika, Katibu mkuu ikieleza wanatakiwa kufika wapi, lini na nini walitakiwa kujieleza mbele ya kamati kuu.

Jaji alieleza wito huo ulipokewa na waombaji wote lakini wakaomba kikao kiahirishwe wakitoa sababu kuwa ili kufanya hali itulie, kutafuta eneo salama la kufanyia mkutano na kupata muda wa kutosha kuandaa utetezi wao.

“Bila hata kupokea ujumbe kuwa ombi lao la kuahirisha kikao limekubaliwa na wakati katiba ya Chadema inaipa mamlaka kamati kuu kushughulikia jambo lolote la dharura, hakuna hata mwombaji mmoja aliyefika mbele ya kamati kuu,” alisema.

“Madai ya kitisho cha usalama waliyoyatoa waombaji hayakuthibitishwa na chombo chochote cha usalama na yalishashughulikiwa na Chadema, ndiyo maana eneo la kikao lilibadilishwa na kwenda Bahari Beach Hoteli,” alisema.

Jaji alisema, “Madai ya waombaji kuwa taarifa ya kubadilishwa kwa eneo la mkutano walizipokea nyakati tofauti kati ya usiku wa Novemba 26, 2020 na Novemba 28, 2020 hayakuthibitishwa kwa kutoa ujumbe wa WhatsApp. Yalikuwa maneno matupu.

Kuhusu malalamiko juu ya matamshi ya katibu mkuu na mwenyekiti wa taifa yaliwaondolea heshima ya kuendelea kushughulikia suala hilo, Jaji alikuwa na maoni tofauti kwamba hiyo haikuathiri wao kushiriki kikao cha nidhamu.
 

Saa 36 za kusafiri

“Kuhusu dhana waombaji walikuwa bado Dodoma baada ya kuapishwa Novemba 24, 2020, mtu atashawishika kujiuliza kama kwa miundombinu ya barabara wangeshindwa kufika mbele ya kamati kuu Novemba 27, 2020,” alisema na kuongeza:

“Waombaji wanakiri kupokea wito Novemba 25, 2020 jioni. Walikuwa na saa 36 za kusafiri kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam lakini wakaamua kutohudhuria kikao cha kamati kuu.”

Kuhusu hoja ya kutopewa haki ya kusikilizwa, Jaji alisema hakuna ubishi kuwa waombaji wote walifika mbele ya baraza kuu ambapo walialikwa kutoa maoni yao kuhusu rufaa zao, na wote waliamua kutoongeza chochote katika rufaa hizo.

“Ni ukweli kuwa mtu anapopewa nafasi ya kuwasilisha kesi yake kwa maandishi, kunakuwa hakuna kukiukwa haki ya asili kama anapewa nafasi hiyo kwa kuongea. Kwa hiyo suala la kutosikilizwa halipo,” alisema Jaji Mkeha.

“Lakini waombaji waliendelea kulalamika kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa kanuni. Kwamba kwa kuwa wao walikuwa wabunge, kulitakiwa kutumike ‘mwongozo wa chama’ katika kushughulikia suala lao lakini haukutumika,” alieleza Jaji.
 

Alivyobatilisha uamuzi

Jaji alisema hoja nyingine ya kushughulikiwa na Mahakama ilikuwa ni kama baraza la wadhamini lilikiuka kanuni ya kutenda haki pasipo upendeleo.

Kulingana na Jaji, kanuni hiyo ina maana kuwa mtu anazuiwa kuamua kesi ambayo anaweza au kudhaniwa kuwa hatatenda haki na hiyo imewekwa ili kujenga imani kwa umma juu ya mifumo ya utoaji wa haki.

“Katika kesi tuliyonayo, baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu akiwamo mwenyekiti wa taifa wa Chadema na katibu mkuu wametuhumiwa kwa upendeleo,” alisema.

“Kwamba wakati walishiriki kutoa uamuzi wa waombaji kufukuzwa uanachama na kamati kuu Novemba 27, 2020, walishiriki pia kuthibitisha uamuzi huo mbele ya baraza kuu la Chadema Mei 11, 2022,” alieleza Jaji Mkeha.

“Hii tuhuma haikubishwa na wajibu maombi. Baadhi ya wajumbe wa baraza kuu waliofika mbele ya Mahakama na kudodoswa maswali walikuwa na maoni tofauti. Baadhi waliona hilo ni tatizo la katiba ya Chadema,” alisema na kuongeza:

“Wengine walikuwa na msimamo kuwa hata kama kura za wajumbe wote wa kamati kuu zisingehesabiwa, bado kura zilizobakia zilikuwa zinathibitisha kufukuzwa kwao uanachama na hiyo inatosha kuhalalisha uamuzi huo.”

Jaji alisema hakubaliani na hoja za mawakili wa wajibu maombi akisema kama akikubaliana na hoja hiyo atakuwa anakwenda kinyume cha kanuni ya msingi ya haki ya asili, na anaona baraza kuu lilikiuka kanuni ya kutopendelea.

Kulingana na Jaji, baraza kuu la Chadema ni kama chombo cha kimahakama kikiwa na mamlaka ya kisheria kushughulikia rufaa za waombaji, kilipaswa kujiendesha kwa mfumo huo wa kimahakama ili kutokuwa na upendeleo.

Hivyo Jaji akatoa amri ya kubatilisha uamuzi wa baraza kuu la Chadema uliofikiwa Mei 11, 2022 na pia mjibu maombi akaamriwa kuhakikisha anaheshimu haki ya asili ya kusikilizwa, anaposhughulikia masuala yanayogusa haki za waombaji.
Katika uamuzi huo, Jaji akasema kila upande utabeba gharama zake za kesi.
Tumefika mwisho wa simulizi ya hatua kwa hatua ya kesi hii.