Prime
Kina mdee walivyobanwa kwa maswali mahakamani

Desemba 14, 2023, Mahakama Kuu ya Tanzania kupitia kwa Jaji Cyprian Mkeha, ilibatilisha uamuzi wa Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), lililothibitisha kuvuliwa uanachama Halima Mdee na wenzake 18.
Kamati Kuu ya Chadema, iliwavua uanachama kwa madai ya kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu wakati kamati hiyo ilikuwa haijafanya uteuzi wowote kwa mujibu wa Ibara ya 7.7.16(a) ya Katiba ya chama hicho.
Halima Mdee na wenzake walivuliwa uanachama wa hicho na Kamati Kuu ya Chadema, Novemba 27, 2020, wakakata rufaa Baraza Kuu la chama hicho ambalo liliketi Mei 11, 2022 kusikiliza rufaa na likabariki uamuzi wa Kamati Kuu.
Wengine waliovuliwa uanachama ni Grace Tendega, Esther Matiko, Ester Bulaya, Agnesta Kaiza, Anatropia Theonest, Asya Mohamed, Cecilia Paresso, Conchesta Rwamlaza, Felister Njau, Hawa Maifunga, Jesca Kishoa na Kunti Majala.
Katika orodha hiyo wamo Naghenjwa Kaboyoka, Nusrat Hanje, Salome Makamba, Sophia Mwakagenda, Stella Fiyao na Tunza Malapo na wote pamoja na akina Mdee, hawakuridhika na uamuzi wa Baraza Kuu kubariki maamuzi ya Kamati Kuu.
Katika mwendelezo wa Makala hii jana tuliwaletea kwa kirefu maelezo ya viapo vya waleta maombi na yale yaliyomo katika maelezo ya pamoja (joint statement) na leo tunawaletea namna waleta maombi walivyopigwa maswali ya dodoso na mawakili.
Maswali ya Dodoso ya Kibatala
Waleta maombi watano kati ya 19, walifika mbele ya Jaji Cyprian Mkeha kwa ajili ya kuulizwa maswali ya dodoso na mawakili kuhusiana na kile walichokiandika katika viapo vyao na leo tutaanza na mleta maombi wa pili, Grace Victor Tendega.
Akijibu maswali ya wakili Peter Kibatala aliyekuwa akiongoza jopo la mawakili wa wajibu maombi, Tendega aliiambia Mahakama kuwa Katiba ya Chadema inatambua mawasiliano kwa njia ya teknolojia (ICT) kama mawasiliano rasmi.
Tendega pia alikiri walipokea wito wa kuwataka kufika mbele ya kamati kuu ingawa sio rasmi na kusisitiza kuwa, barua pepe na njia nyingine za mawasiliano zinakubalika, haikuwa rasmi kwa kuwa Katibu mkuu alitumia njia ya WhatsApp.
Pia, alikiri kulikuwa hakuna ushahidi kuhusu barua ya Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ya kukataa ombi lao la kuahirishwa kikao na kubadilisha eneo la mkutano kama zilivyopokewa jioni ya Novemba 27, 2020.
Tendega alishikilia msimamo kuwa hawakuwahi kupewa haki ya msingi ya kusikilizwa, sio kwenye Kamati Kuu pekee, bali hadi kwenye Baraza Kuu na nafasi pekee waliyopewa Baraza Kuu ni ya kuwataka kuomba radhi.
Kwa upande wake, mleta maombi wa 11, Hawa Mwaifunga, alikiri katika majibu yake kuwa kulingana na Katiba ya Chadema, Kamati Kuu ilikuwa na mamlaka ya kuchukua hatua katika jambo au mazingira ya dharura yanayojitokeza.
Alilalamikia hatua ya wajumbe wa kamati kuu kushiriki katika kikao cha kamati kuu kilichowafukuza uanachama na Baraza Kuu lililothibitisha uamuzi huo.
Walichokisema Hanje na Pareso
Katika kuongeza mafuta kwenye moto, Jaji alisema Mleta maombi wa 15, Nusrat Hanje na wa 8, Cecilia Pareso walishikilia msimamo ilikuwa ni makosa kwa Kamati Kuu kushughulikia jambo kwa dharura wakati udharura ulikuwa umekwisha.
Kwa mujibu wa wawili hao, suala hilo halikuwa na dharura yoyote baada ya wao kuapa kama wabunge na kueleza haikuwa sahihi kwa wajumbe wa Kamati Kuu walioshiriki kikao kilichowatimua, kuwa tena wajumbe wa Baraza la Rufaa.
Pareso yeye alikiri kuwa katiba ya Chadema aliyokuwa akiifuata kabla ya kufukuzwa, inaruhusu mwenyekiti wa Taifa na Katibu mkuu wa chama kuendesha vikao vyote viwili, kwa maana ya Kamati Kuu na Baraza Kuu la chama hicho.
Kwa upande wake, Jesca Kishoa ambaye ni mleta maombi namba 12, katika kujibu maswali hayo ya dodoso ya wakili Kibatala, alikiri kupokea wito kufika mbele ya kamati kuu pamoja na tuhuma alizotakiwa kuzijibu mbele ya kamati kuu.
Kishoa alikiri pia kuwa ombi lao la kuahirishwa kwa kikao hicho cha kamati kuu, halikutokana na kukosekana hati ya tuhuma bali sababu za kiusalama.
Majibu ya Baraza la wadhamini Chadema
Katika majibu yake juu ya maelezo ya jumla (joint statement) ya waombaji, mjibu maombi wa kwanza, Baraza la Wadhamini alisema maombi hayo hayana mashiko kwa vile hakuna hata mmoja kati ya waombaji 19 ni mwanachama wa Chadema.
Pia, hawakudhaminiwa na Chadema kuwa wabunge wa viti maalumu na kwamba waleta maombi walikuwa wameghushi barua ya uteuzi na unafuu wanaoutafuta hauwezi kufikiwa kwa sababu waligoma kufika wenyewe mbele ya Kamati Kuu.
Jaji alisema ilielezwa katika majibu hayo kuwa mjibu maombi huyo wa kwanza alifuata taratibu zote zilizotakiwa kabla ya kufikia maamuzi katika hatua ya kamati kuu na baadaye Baraza Kuu lililokuwa ndio hatua ya rufaa ya suala hilo.
Ilielezwa kuwa waombaji hawakumtafuta mjumbe yeyote wa Kamati Kuu au Baraza Kuu kwamba rufaa yao isikilizwe na kwamba waombaji hao walipewa haki kamili ya kusikilizwa na kamati kuu na baraza kuu na hawakudai hilo kwa namna yoyote.
Waombaji walipewa tuhuma zao
Majibu hayo yalienda mbali na kuonyesha kuwa matamshi yaliyotolewa na katibu mkuu hayakutolewa katika muktadha unaoelezwa na kwamba katibu mkuu peke yake hana uwezo wa kushughulikia hatima ya kinidhamu ya waleta maombi.
Majibu hayo yanaonyesha zaidi kuwa waombaji walipewa mashitaka yao na ndiyo maana waliomba waongezewe muda wa kujibu, mashitaka yalikuwa wazi mno na hata vifungu vya katiba ambavyo waombaji walituhumiwa kuvikiuka vilinukuliwa.
Ilielezwa kamati kuu haikufanyia kazi uvumi kama ilivyodaiwa na waombaji kwa kuwa walijulishwa kikamilifu kwa njia zote pamoja na tuhuma zao zilizohusisha kudanganya na kujiteua kuwa wabunge bila kuzingatia Katiba ya Chadema.
Kuhusu kitisho cha usalama, mjibu maombi alisema hilo halikuripotiwa kituo chochote kile cha polisi na kwamba hakuna hata mmoja aliyefuata maelekezo ya kuomba kuahirishwa kwa kikao cha kamati kuu, bali waliamua kutohudhuria.
Pia, bodi hiyo ya wadhamini ilisema haikufahamu kudanganya na kujifanya kwao kuwa waliteuliwa wabunge wa viti maalumu hadi waliona hilo kupitia vyombo mbalimbali vya habari kuwa waombaji hao wameapishwa kuwa wabunge.
Hakuna ushahidi walikuwa Dodoma
Bodi hiyo katika majibu yake ikaongeza kusema kuwa kulikuwa hakuna ushahidi kwamba Novemba 25, 2020, waombaji hao walikuwa Dodoma wala ushahidi kuonyesha kuwa bado walihitaji kuwa Dodoma Novemba 26 na 27, 2020.
Ilieleza kuwa Katibu Mkuu wa Chadema aliwashauri kuwa ombi la kuahirishwa kwa kikao cha kamati kuu liwasilishwe kamati kuu na wala hakuna hata muombaji mmoja, aliyeomba usikilizwaji kwa njia ya video au njia nyingine yoyote. Badala yake, waombaji wote 19 kwa makusudi na katika mpango uliopangwa kwa umakini, waliamua kutohudhuria wenyewe kikao cha kamati kuu ili kujipatia jukwaa la kuitumia Mahakama kuhuisha viti maalumu bungeni.
Kwamba kikao cha kamati kuu kilipangwa kuanza saa 4:00 asubuhi lakini kiliahirishwa hadi saa 5:40 kwa matumaini waombaji wangehudhuria lakini hawakutokea na kwamba tangu 2020, kamati kuu na Baraza haikuwahi kukaa.
Baraza hilo la wadhamini la Chadema lilieleza kuwa Kamati Kuu na Baraza Kuu zilikuwa hazijakaa vikao vya kawaida lakini kwa vikao vya dharura, mihtasari yote iliambatanishwa na hati ya viapo haikuwa na sahihi na zilitimiza wajibu wake.
Kulingana na majibu hayo, mjibu maombi huyo alieleza kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Chadema, wote wawili Mwenyekiti wa Taifa na Katibu mkuu ni wajumbe wa kamati kuu na vile vile Baraza Kuu na waombaji hawakumtafuta hata mmoja.
Baraza hilo limeeleza kuwa waombaji wote walipofika mbele ya Baraza Kuu, kila mmoja alikaribishwa kufanya wasilisho la rufaa yake lakini wakaamua kutowasilisha na matokeo yake wajumbe wakapiga kura dhidi ya rufaa zao.Lilieleza kuwa wakati wajumbe wa Baraza Kuu ni 442, waliopiga kura ni 437
Usikose kufuatilia mfululizo huu wa hatua kwa hatua wa kesi hii kesh