Hekaheka za mvua ya dakika 45 Morogoro

Maji ya mafuriko yakiwa yametapakaa barabara ya Korogwe Manispaa ya Morogoro kufuatia mvua kubwa kunyesha na shughuli za kiuchumi kusimama baada ya maji ya mto kikundi kuzidiwa mkoani hapa. Picha na Juma Mtanda
Muktasari:
- Mvua hiyo imesababisha barabara za kuingia katikati ya mji kushindwa kutumika kwa muda baada ya maji kupita juu ya madaraja katika barabara ya Makongoro, Madaraka na Korogwe.
Morogoro. Mvua iliyonyesha kwa zaidi ya dakika 45 mjini Morogoro imesababisha barabara za kuingia katikati ya mji kushindwa kutumika kwa muda kutokanana na maji kupita juu ya madaraja katika barabara ya Makongoro, Madaraka na Korogwe.
Katika kadhia hiyo, mwendesha pikipiki ambaye hajafahamika alinusurika kifo baada ya pikipiki yake kutumbukia katika mtaro, eneo la Mtawala Hood, huku barabara ya Msamvu-Mjini na soko kuu la Mkoa wa Morogoro la Chifu Kingalu likizingizwa na maji ya mto Kikundi.
Akizungumza na Mwananchi Digitali leo, Alhamisi Januari 25, 2024 mjini hapa, shuhuda wa tukio hilo, Arnold Arnold amesema mvua iliyoanza kunyesha saa 6 mchana imesababisha mafuriko katika mitaa ya Manispaa ya Morogoro, hali iliyosababisha baadhi ya shughuli za uchumi kusimama.
Akizungumzia tukio la mwendesha pikipiki kunusurika kifo, Arnold amesema kijana huyo alipofika eneo la Mtawala Hood aliingia katika mtaro na kutumbukia na pikipiki yake. Hata hivyo, amesema watu walikwenda kumuokoa.
“Kama tukio lile lisingeonwa na watu, uhai wa yule bodaboda ulikuwa shakani, kwa sababu baada ya kutumbukia huwezi kujua kama mkono, mguu ameumia au la,” amesema Anold.
Mkazi wa Manispaa ya Morogoro, Thadei Hafigwa amesema mvua hiyo imeleta madhara kwa wafanyabiashara na kuzuia shughuli za kiuchumi kusimama kutokana na maji kusambaa katika mitaa ya Makongoro, Korogwe, Juwata na Madaraka huku maji yakiingia katika maduka.
“Mto Kikundi umezidiwa maji kiasi cha kusambaa katika mitaa ya Madaraka, Korogwe, Makongoro na Juwata baada ya mvua hiyo kunyesha,” amesema Hafigwa.
Naye mfanyabiashara katika mtaa wa Makongoro, Ismail Vajihee amesema kufurika kwa maji katika mto Kikundi kumesababisha maduka kuingiliwa na maji na bidhaa kuharibika.
“Halmashauri yetu inaweza kufikiria njia nyingine sahihi za kudhibiti maji ya mto Kikundi, kwani mvua kubwa ikinyesha yanashindwa kupita katika mto kutokana na uwingi wake,” amesema Vajihee.