Mafuriko yalivyoacha maumivu, waanza maisha upya

Muktasari:
- Baada ya daraja kukatika, aliyetoka kujifungua kwa upasuaji alazimika kutembea umbali wa kilomita 10 kwenda nyumbani
Dar es Salaam. Ni kama maisha yanaanza upya kwa waathirika wa mafuriko jijini Dar es Salaam, waliopoteza kila kitu ndani ya nyumba zao, huku watoto wakishindwa kwenda shule kutokana na vitu vyao kupotea.
Pia mvua hizo zimesababisha kukatika kwa madaraja na kuacha maumivu kwa baadhi ya watu, wakiwemo wagonjwa walioshindwa kuvuka ama kuvushwa kutoka upande mmoja kwenda mwingine.
Mvua hizo zilizonyesha Jumamosi na Jumapili (Januari 21 na 22, 2024) zimesababisha baadhi ya watu kuomba hifadhi katika makanisa, misikiti na wengine kwa majirani kutokana na nyumba zao kudondoka au kujaa maji kutokana na mvua hizo.
Baada ya mvua kutokunyesha leo Januari 23, 2024 maeneo mengi maji yamepungua na mengine kukauka, hivyo wamiliki kuanza usafi, huku wengine wamesharejea kuendelea na maisha.
Jacob Julius, mkazi wa Mbopo Madale ni miongoni mwa walioathiriwa na mvua, anasema yeye na mkewe aliyekuwa ameruhusiwa kutoka hospitali walishindwa kuvuka ng’ambo ya pili kwenda nyumbani baada ya daraja kukatika.
"Tulifika kwenye daraja la Mbopo na kukuta limeharibika, kadri mvua ilivyokuwa inanyesha lilizidi kumeguka, magari hayakuweza kupita. Mke wangu ana kidonda kibichi cha upasuaji,” amesema.
Julius amesema licha ya kutambua kuwa mkewe ni mwenye maumivu ya kujifungua, walilazimika kuacha gari ili wavuke upande wa pili.
"Alivyokuwa akitembea na maumivu aliyokuwa akiyahisi siwezi kusimulia, ilikuwa ni mateso. Kule upande wa pili kulikuwa na gari nyingine ambayo alikwenda kupanda ili kufika nyumbani, lakini tulilazimika kutembea mwendo wa kilomita 10 kutokana na ubovu wa barabara na hakuna njia mbadala zaidi ya hiyo,” amesema.
Alichopitia Julius, pia kiliwasibu wazazi wengine wenye familia zenye watoto wadogo ambao hawakuwa na uwezo wa kujiokoa, badala yake waliwategemea wazazi wao.
Aisha Ramadhani, mkazi wa Msimbazi amesema alikuwa amelala akashtuka baada ya mwenye nyumba kumgongea mlango.
Amesema alipotoka tayari maji yalikuwa yameingia ndani, ikambidi ambebe mtoto wake wa miaka minne na kwa msaada wa wanaume waliokuwa wakipita kuokoa watu.
Amesema amekuwa akilala kwa majirani, huku akiwa amepoteza kila kitu vikiwamo vifaa vya mtoto vya shule.
“Chakula, vyombo vya ndani sikuweza kuokoa chochote, nilipofungua mlango vingine vilibebwa, tulikula kwa majirani, kulala kwa majirani hadi leo Januari 23, 2024 ndipo tumekuja kufanya usafi,” amesema.
Amesema nguo zilizosalia ni chache nyingine amezitupa kwa kuwa hazifai.
Kwa upande wake, Happiness Raphael amesema baada ya kelele za maji kujaa, alimbeba mwanaye na kumpeleka eneo lenye mwinuko ili awe salama.
“Nilipompeleka nikamuacha hapo nikawa narudi kujaribu kuokoa baadhi ya vitu, lakini sikufanikiwa kwa chochote, hapa ndiyo tumeanika godoro vingine vyote tumepoteza,” amesema.
Deogratius Raphael, anasema licha ya kupoteza samani za ndani, pia amepoteza asilimia 90 ya bidhaa zake dukani kutokana na mvua.
Jokofu alikuwa akilisafisha jokofu lililokuwa limejaa tope, huku akiwa hana uhakika iwapo litafanya kazi tena.
Raphael anasema amelazimika kumhamisha mkewe na watoto wake watatu kwenda kwa ndugu, huku yeye akisalia nyumbani kuangalia namna anavyoweza kulinda mali zake.
“Maisha yanaanza upya, hali ni mbaya, hatuna kitu,” amesema Raphael.
Rally Kyando, mkazi wa Tegeta amesema mkewe na watoto wanne wamekuwa watu wa kulala msikitini kutokana na nyumba kubomoka na hawana pa kwenda.
Nyumba hiyo iliyokuwa na vyumba sita, vinne kati yake alikuwa amepangisha.
“Tunalala msikitini, saa 11 asubuhi tunakuja hapa kulinda vibaka wasibebe vitu, tunashindwa kurudisha hata familia kwa sababu sehemu ya nyumba iliyobakia ina ufa,” amesema Kyando.
Mchungaji wa Kanisa la Berthel Nyumba ya Maombi na Majibu, Asajile Masisi ni miongoni mwa waliohudumia familia nyingi kupita kanisa lake lililopo eneo la Kigogo baada ya kulazimika kuwalisha na kuwapa hifadhi ya muda watu ambao nyumba zao zilizingirwa na maji.
Katika eneo lilipo kanisa hilo, nyumba huzingirwa na maji inaponyesha mvua kubwa hivyo hulazimika kuwapa hifadhi wao na mali zao.
“Wamepoteza kila kitu, wakiamka asubuhi kuna watoto pale, inabidi unaingia mfukoni kutafuta hela ili wapate hata mikate, mchana chakula,” amesema.
Mvua iliathiri miundombinu ya barabara na kusababisha kupanda bei ya nauli katika baadhi ya maeneo.
"Huwa naangalia kama barabara ni mbovu, eneo la kwenda kwa Sh1,500 nawapeleka kwa Sh3,000, hii nafidia na chombo changu ikitokea kimeharibika," amesema Nathan Emmanuel, dereva wa bodaboda eneo la Mbezi Mwisho.
Dereva wa bajaji, Juma Khatibu amesema kuna maeneo kipindi cha mvua hakubali kupeleka wateja.
"Kuna maeneo barabara ni mbovu mno, unajikuta unaenda kutafuta Sh5,000 lakini unaharibu bajaji yako. Kuna abiria niliwahi kuwashushia njiani huko Mbweni, barabara ilikuwa mbovu nikaona isiwe tabu na pesa nikasamehe," amesema.