Haya hapa maeneo matano yanayoweza kuathiri Dira ya Taifa ya 2025

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko akizungumza wakati wa uzinduzi wa kongamano la kwanza la Kikanda kuhusu maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 lililofanyika leo Julai 20, 2024 katika ukumbi wa ‘Kwa Tunza’ wilayani Ilemela mkoani Mwanza. Picha na Mgongo Kaitira
Muktasari:
- Hadi kufikia Juni 24, 2024, watu 1, 054,393 walikuwa wametoa maoni yao kwa njia ya ujumbe mfupi ‘SMS’, kati yao wanaume ni 738,074 (asilimia 70) na wanawake ni 316,318 sawa na asilimia 30.
Mwanza. Mabadiliko ya tabianchi, teknolojia, demografia, mpasuko wa siasa za dunia na machafuko ya vita ni miongoni mwa matishio yanayoweza kuja kuathiri ufanisi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo kwa mwaka 2050 kama hayatawekea mkakati wa kuyakabili.
Hayo yamesemwa leo Jumamosi Julai 20, 2024 Jijini Mwanza na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko wakati wa uzinduzi wa kongamano la kwanza la kikanda kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Dk Biteko amesema mabadiliko hayo yana athari za moja kwa moja kwa siku zijazo katika mwelekeo wa utekelezaji wa shughuli za kiuchumi huku akitolea mfano mabadiliko ya tabia nchi kuwa yameathiri utekelezaji wa bajeti za nchi mbalimbali na kuzilazimu kuwekeza nguvu katika matumizi ya nishati safi.
“Mabadiliko ya teknolojia yanatuhamisha kwenye mfumo tuliokuwa tunaishi na kutufanya tuishi kama teknolojia inavyotaka, sasa hivi dunia inapitia katika kipindi ambacho kuna mpasuko wa hali ya juu, jirani na jirani hawaelewani kwa sababu mbalimbali na mitazamo ya kiusalama, hizi zote zinaathari katika Dira ya Taifa 2025 tuliyonayo sasa,” amesema Dk Biteko.
Hata hivyo, amesema Tanzania imepiga hatua katika kipindi cha miaka 25 ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2025 inayofikia tamati Juni, 2025, huku akidokeza kuwa nchi imeshuhudia kukua kwa uchumi kwa asilimia 5.6 katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2020.
“Tumekuja hapa kuwashirikisha wananchi kuandaa Dira wanayoitaka katika miaka 25 inayokuja. Tunaandaa dira ya wananchi siyo ya Serikali, maana kuna watu wanaweza kuibuka na kusema dira ni mali ya Serikali na siyo wananchi; tukifanya hivyo, wananchi watajitenga,” amesema naibu waziri mkuu huyo.
Ameitaka Tume ya Mipango kuhakikisha inafanya ushirikishwaji wa wananchi kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchakato wa utengenezaji wa dira hiyo kwa kile alichodai kufanya hivyo kutajenga uaminifu, hisia za umiliki, kupata maoni ya pamoja na kutengeneza umoja wa kitaifa.
“Kufanya hivyo kutachochea pia ahadi na ushiriki wa wadau katika kutekeleza sera muhimu na mageuzi kwenye nchi. Napongeza kwa sababu wananchi wamekuwa na mwitikio mkubwa mno katika utoaji maoni, mpaka sasa zaidi ya watu milioni 1.2 wametoa maoni kwa njia mbalimbali hadi kufikia Julai 9, 2024,” amesema Dk Biteko.
Amesema hiyo ni ishara kwamba wananchi wanataka kuwa sehemu ya mchakato huo, washirikishwe kwa njia zote.
Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema hadi kufikia Juni 24, 2024, watu 1, 054,393 walikuwa wametoa maoni yao kwa njia ya ujumbe mfupi ‘SMS’ na kati yao hao, wanaume ni 738,074 (asilimia 70) na wanawake ni 316,318 sawa na asilimia 30.
Profesa Mkumbo amesema hadi kufikia Juni 24, 2024, watu 11,454 walikuwa wametoa maoni yao kwa njia ya tovuti na wanaume ni 9,850 sawa na asilimia 86 huku wanawake wakiwa 1,604 sawa na asilimia 14.
Kwa mujibu wa Profesa Mkumbo, tume hiyo ya mipango pia imekusanya maoni kwa njia ya Sampuni ya bahati nasibu kwenye kaya na watu 7,968 walifikiwa huku wanawake wakiongoza kwa asilimia 59 (watu 4,701) na wanaume asilimia 41 sawa na watu 3,267.
“Kupitia ukusanyaji wa maoni uliofanyika kwa njia ya namba za simu wanawake wako vizuri, asilimia 52 na wanaume asilimia 48. Kupitia makundi ya kijamii, tayari makundi 16 yamefikiwa, viongozi waliostaafu 11 wamefikiwa akiwemo Spika mstaafu, Pius Msekwa,” amesema Profesa Mkumbo.
Waziri huyo ameeleza kufurahishwa na mwitikio wa vijana katika utoaji maoni huku akidokeza kuwa kati ya maoni 1, 054,392 yaliyokusanywa, watu 854, 056 sawa na asilimia 81 ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35 huku akisisitiza kuwa dira hiyo itakuwa na mafanikio kwa sababu imetokana na maoni ya vijana.
“Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, asilimia 76 ya Watanzania wako chini ya miaka 35, kwa hiyo hilo ni jambo lenye tija tunawashukuru sana vijana kwa mwitikio wao wa kutoa maoni yao, hii inaakisi hali halisi ya demokgrafia ya nchi yetu na vijana ambao ndiyo wenye nchi wamechangamkia fursa ya kutoa maoni yao,” amesema Profesa huyo.
Wakati huo, Mkazi wa Nyamagana mkoani hapa, Vivian Nyambui amependekeza Dira ya 2050 izingatie kigezo cha mgawanyo wa rasilimali na fursa ili kufikia lengo la usawa wa kijinsia (50/50) ifikapo 2050.
Pia ameishauri tume hiyo kuainisha vipaumbele vinavyohamasisha wanawake kuuteka uchumi wa nchi.
Mwakilishi wa Taasisi ya Wasosholojia Tanzania, Bituro Kazeri amesema dira hiyo inatakiwa kutoa taswira ya nchi kuweza kukabiliana na changamoto zinazoikumba dunia ikiwemo mabadiliko ya teknolojia, idadi ya watu na uwezo wa nchi kukabiliana na changamoto ilizonazo.