Hamisa Mobetto afunguka baada ya kuteuliwa

Muktasari:

Mwanamitindo Hamisa Mobetto ameishukuru Serikali kwa kumteua kuwa miongoni mwa mabalozi wa kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari akibainisha kuwa atatumia nafasi hiyo ili lengo lifikiwe.

Dar es Salaam. Mwanamitindo Hamisa Mobetto ameishukuru Serikali kwa kumteua kuwa miongoni mwa mabalozi wa kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari akibainisha kuwa atatumia nafasi hiyo ili lengo lifikiwe.

Leo Jumanne Juni 22, 2021 Waziri wa Fedha na Mipango,  Dk Mwigulu Nchemba akiwa bungeni mjini Dodoma  amemtangaza Mobetto, Mbwana Samatta, Edo Kumwembe na wengineo kuwa mabalozi wa kuhamasisha wananchi kulipa kodi.

Katika shukrani zake,  Hamisa amesema ni heshima kuteuliwa kuitumikia nchi yake na ni mwendelezo wa Serikali ya awamu ya sita kuwaamini vijana katika utendaji kazi. 

"Nimshukuru pia Rais wangu Samia Suluhu Hassan na Serikali nzima akiwemo waziri Nchemba kwa kuendelea kuamini vijana kwenye ujenzi wa Taifa letu.”

"Kwa kutambua umuhimu wa kodi kwenye uendeshaji wa miradi ya nchi na kuchagia maendeleo ya Taifa, naahidi kuitumikia vyema nafasi yangu niliyoteuliwa ya ubalozi wa uhamasishaji wa ulipaji kodi kwa maslahi ya Taifa langu, naahidi kushirikiana na mabalozi wenzangu Kumwembe na Samatta pamoja na viongozi na wadau mbalimbali wa masuala ya ulipaji kodi" amesema. 

Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amesema, "asante Mwigulu Nchemba kwa kutumia sanaa na michezo katika utoaji wa hamasa na elimu ya ulipaji kodi. Natoa wito kwa wasanii kuzidi kujiheshimu na kuheshimisha tasnia. Serikali inayoongozwa na Samia inaendelea kufanya maboresho makubwa katika tasnia ya sanaa na michezo.”