Gugu vamizi tishio kwa uhifadhi na malisho ya mifugo

Muktasari:
- Gugu hilo ambalo linadaiwa kutokea nchini Kenya na mbegu zake zinasambaa kwa upepo na hutua zaidi maeneo yenye miinuko, pia mifugo, magari na watu wanatumika kusambaza mbegu zake kwa wepesi, mpaka sasa mikakati madhubuti ya kukabiliana nalo haijapatikana.
Kusambaa kwa kasi kwa gugu vamizi aina ya Chromoleana Odorata ni tishio kwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mapori ya Akiba ya Ikorongo, Grumeti na Ikona Wma, ufugaji na kilimo kwa wilaya za Mkoa wa Mara.
Gugu hilo ambalo linadaiwa kutokea nchini Kenya na mbegu zake zinasambaa kwa upepo na hutua zaidi maeneo yenye miinuko, pia mifugo, magari na watu wanatumika kusambaza mbegu zake kwa wepesi, mpaka sasa mikakati madhubuti ya kukabiliana nalo haijapatikana.
Mmea huo ambao umebatizwa jina la (Amaachabongo) na wakazi wa Tarafa ya Ngoreme wakimaanisha uliokuja hivi karibuni, unazidi kusambaa pamoja na tafiti za ndani na nje hazijawahi kuja na mkakati wa nini kifanyike.
Tawiri
Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (Tawiri) Kituo cha Serengeti, Dk Robert Fyumagwa anasema mmea huo unaathiri mtawanyiko wa wanyamapori na una hatarisha uhifadhi ukiingia maeneo hayo bila kudhibitiwa.
“Invasive plant ni mmea hatari sana, kwa kuwa unaathiri uhifadhi, kilimo, mifugo na mazingira kwa ujumla uliingia nchini kwa usafiri wa meli, anga na barabarani kupitia njia ya nafaka na mbegu zake zinasambaa kwa upepo,” anasema.
INAENDELEA UK 26
INATOKA UK 25
Pia, mbegu zake hunasa kwenye nguo, kwato za wanyama na magurudumu ya magari, kwa njia hizo na nyingine husafirishwa maeneo mbalimbali na ndiyo chanzo cha kusambaa kwa wingi na haraka.
Mtafiti huyo anasema kwa sehemu kubwa binadamu ndiyo wameusambaza kwa njia ya mapambo kutokana na maua yake, hata hivyo kasi yake ni kubwa na kuwa jitihada zinatakiwa ili kudhibiti hali hiyo ndani na nje ya hifadhi kwa kuwa unachangia upungufu wa chakula kutokana na kuathiri mazao.
“Gugu hili ni tatizo la dunia maana mataifa mengi yameathiriwa nalo na inabidi sekta mbalimbali za kiserikali na zisizo za kiserikali kuhakikisha linadhibitiwa kwa kuwa athari yake ni kubwa kiuchumi, kama uhifadhi, kilimo na mifugo itaathirika unategemea mapato utapata wapi?” anahoji.
Anasema wilaya za Mkoa wa Mara zote zimeishaathiriwa na gugu hilo na kutokana na wananchi kutokujua hawachukui hatua haraka, maana linatakiwa kung’olewa kabla ya kuweka mbegu na kukomaa.
Senapa
Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, William Mwakilema anasema, “juhudi zinazofanyika ni Surveillance (uchunguzi) magugu vamizi hifadhini, mara moja kwa kila robo mwaka njia zote, kambi za utalii na maeneo mengine hudhibitiwa.”
Anasema njia ya kuliondoa ni kung’oa na kuchomwa moto kwa kuwa njia nyingine kama kufyeka huchipua na mbegu zikikomaa kusambaa maeneo mengi na kusababisha athari kubwa ya kiutalii na kuwa wao wanalichukulia kwa umakini mkubwa ikiwemo maeneo ya nje ya hifadhi wanayopakana.
Kung’oa na kupuliza dawa
Kampuni ya Grumeti Reserve Ltd inayoendesha vitalu vya utalii vya Ikorongo na Grumeti kwa wilaya za Serengeti na Bunda inakiri gugu hilo na mengine yenye athari kubwa kiuhifadhi kuingia katika maeneo yao.
Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Grumeti Game Reserves Ltd, Ami Seki anasema wanakabiliwa na aina mbili za mimea vamizi, lakini Chromoleana Odarata ndiyo unaenea kwa kasi na njia wanayotumia zaidi ni kung’oa na kuchoma.
“Tunaendesha zoezi la kung’oa na kuteketeza gugu vamizi aina ya Chromoleana Odarata ambayo ni hatari kwa uhifadhi katika mapori ya akiba ya Ikorongo na Grumeti hiyo ndiyo njia pekee ya kudhibiti gugu hilo kabla ya kuanza kutoa mbegu,”anabainisha na kuongeza.
“Tunatumia njia mbili ya kukata na kupuliza dawa, mmea huu ni hatari kwa kuwa si chakula cha wanyama, unaua mimea mingine ya asili na unawakwaruza wanyama.”
Anabainisha kuwa vijiji vingi jirani na maeneo yaliyohifadhiwa vimevamiwa na magugu hayo, ili kuyadhibiti kabla ya kusambaa wanalazimika kuomba vibali kwa vijiji hivyo na kuyang’oa na kuyateketeza.
“Mmea huo ukiufyeka unachipua na kusambaa haraka, tunatumia gharama kubwa kuliangamiza, kampuni imelazimika kuajiri watu kwa ajili ya kudhibiti gugu hilo lisisambae na kusababisha madhara kiuhifadhi,” anasema.
Anasema pia kampuni inasaidia vikundi vingine vinavyopambana na gugu hilo kwa ajili ya kuelimisha jamii hasa Tarafa ya Ngoreme ambako limeshamiri kila kona, lengo ni kuhakikisha linadhibitiwa na kupunguza madhara kwa sekta za kilimo, mifugo, maji na uhifadhi.
“Mbali na vikundi pia tumetoa gari aina ya Land Cruiser kwenye Kituo cha Utafiti Serengeti ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao vema, maana tunatambua umuhimu wao katika sekta ya utalii na uchumi wa Taifa,” anasema.
Seki anasema kuna wakati kampuni yao iliomba kibali cha kutumia wadudu maalumu wanaokula magugu hayo, njia ambayo imetumika katika nchi mbalimbali ikiwemo Afrika Kusini ambazo zinakabiliwa na gugu hilo, hata hivyo mchakato wake bado.
Baadhi ya wataalamu wanasema kuwa magugu hayo yakiota pembeni mwa mito huathiri mazalia ya mamba na samaki, hivyo eneo ambalo liko hatarini ni Mto Mara ambao ni Uti wa Mgongo wa Utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Haki asili
Katibu wa Asasi isiyo ya Kiserikali ya Haki Asili Serengeti, Gabriel Mwita anasema maeneo lilipoota gugu hilo mimea mingine imedumaa, mizizi na majani hayaliwi na wanyama, mbegu zake ni hatari kwa wanyama kutokana na ncha kali huwachoma machoni na kusababisha upofu.
“Asilimia 60 ya ardhi katika Tarafa ya Ngoreme imevamiwa na gugu hilo, wafugaji wanapata shida na malisho, afya za mifugo zinazidi kudorora na kuathiri uchumi wa wananchi, kwa wakulima wanapata shida kwa kuwa wanalazimika kuchimba na kuchoma,” anasema.
Halmashauri
Daktari wa Mifugo Wilaya ya Serengeti, Tito Kagize anakiri gugu hilo limepunguza sana maeneo ya malisho hasa yaliyoko kwenye miinuko katika eneo la Ngoreme, ubora wa mifugo unazidi kupungua.
“Kwa upande wa kilimo halina shida kubwa kwa kuwa wananchi wanalazimika kung’oa na kuchoma, wasipofanya hivyo wasitegemee mavuno kwa kuwa unakua kwa kasi na kufunika mazao na kuathiri ukuaji wake,”anasema.
Nemc
Richard Mayungi kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), anakiri kuwa hawakuwa na taarifa sahihi kuhusu gugu hilo na athari zake.
“Itabidi tutume timu ya wataalamu Mkoa wa Mara ili kuona hali ilivyo na namna ya kuweka mikakati ya kukabiliana nalo,” anasema.
Anasema watakuwa na mikakati mbalimbali baada ya kufika na kuona hali ilivyo na watashirikiana na wadau mbalimbali ili kudhibiti aina ya magugu ambayo ni mageni lakini yenye madhara makubwa kimazingira, kiuchumi na kijamii.
Nini kifanyike?
Fyumagwa anasema utafiti upewe kipaumbele maana uendelevu wa uhifadhi, kilimo, ufugaji na mazingira unategemea sekta hiyo, hivyo fedha nyingi zitengwe kuwawezesha kufanya kazi yao na kuwasilisha matokeo kwa jamii.
“Taarifa nyingi za kitafiti zimefungiwa haziwafikii wananchi kutokana na ukosefu wa fedha, hata wanasiasa hawazitumii kwenye vikao vyao, ndiyo maana wananchi hawapati taarifa nyingi kwa kuwa kuna ufa katikati ya watafiti na wanasisa,” anabainisha.