Gharama za kusomea urubani Tanzania Sh70 milioni

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kufanya marejeo ya viwango vya mikopo ya urubani na kutoa kipaumbele kwa wahitaji wa fani hiyo huku masomo yake kwa mwaka ikiwa ni Sh70 milioni.
Agizo hilo la Majaliwa, ni kufuatia kauli ya uhaba wa wataalamu hao, iliyoelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari katika kilele cha Maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo.
Akijibu changamoto hiyo, Majaliwa amesema Watanzania wengi hawamudu gharama ya fani hiyo hivyo ni muhimu kwa Bodi ya Mikopo kuanza ufadhili wa taaluma ya urubani.
"Bodi ya Mikopo angalieni namna mfanye marejeo ya viwango vya mikopo vinavyotolewa kwa wanafunzi wa urubani na kutoa kiaumbele kwa wahitaji wa fani za masuala ya usafiri wa anga," amesema na kuongeza kuwa,
Ni lazima tuwe na mikakati mahususi kujitosheleza na mahitaji ya ndani Wizara ya Uchukuzi ishirikiane na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kutanua wigo wa mafunzo kwenye tasnia ya anga, hii itakuwa suluhusisho la uhaba wa wataalamu," amesema.
Pia, Majaliwa ametaka uwepo wa motisha kwa wataalamu hao ili kuwabakiza kufanya kazi nchini huku akiwataka wazazi kuwahimiza watoto wao kusomea fani hiyo.
Tayari Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kipo kwenye hatua za mwisho kuanza kutoa mafunzo ya urubani ambayo imetangaza gharama ya mafunzo hayo ni Sh70 milioni.
Kulingana na NIT, kati ya fedha hizo, Sh21 milioni ni kwa ajili ya kozi ya awali yenye kumuwezesha mwanafunzi kusoma masomo ya awali na kuruka angani kwa saa 50 na Sh70 milioni itamuwezesha mwanafunzi kusoma na kurusha ndege saa 200.
Kusomea nje aghari zaidi
Mdau wa anga ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, amesema kuwa rubani wa kurusha ndege lazima asomee mafunzo hayo kwa miaka miwili hadi mitatu kwa saa 250.
“Mara nyingi watu wanakwenda kusoma nje ya nchi, hela utakayolipia darasani kusoma itaendana na saa zako, kwa kawaida ndege ndogo ya kujifunzia unatozwa Dola 220 (Sh550,000) kwa saa moja hivyo kwa Saa 250 ni Sh137.5 milioni kwa kima cha chini gharama ikiwa ni tofauti kulingana na nchi,”amesema.
Amesema kwa mtu ambaye amefikisha saa 1,000 ndiye anayeuzika kwa urahisi na mshahara wake ni zaidi ya Dola 5,000 sawa na zaidi ya Sh12.5 milioni.
Utendaji wa TCAA
Kuhusu utendaji wa mamlaka hiyo, Majaliwa ameitaka TCAA kufanya kazi kuendana na mabadiliko ya teknolojia ili kuongeza ufanisi wa taasisi hiyo ya Serikali.
"Mabadiliko hapa ni lazima, wataalamu wetu angalieni namba ya kuendana na mabadiliko, tunahitaji ubunifu wa hali ya juu na mikakati mipya ya kuinua soko shirika letu limudu kasi ya mabadiliko haya," amesema.
Pia ameielekeza TCAA kuhakikisha inaimarisha mifumo ya usalama ili kuepusha usafiri wa anga kuwa kichochoro cha kusafirisha bidhaa haramu.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema kulingana na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (IATA) viwanja vya ndege viko salama kwa asilimia 90.
Alisema kwa ubora wa viwanja vya ndege, Tanzania ni nchi ya nne Afrika kuwa na viwanja bora ikipata asilimia 86.7 ya ubora.
Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Johari amefafanua kuwa, “Mwaka 2013 tulipata asilimia 37.4 kwa hiyo hatukuweza kufikia kiwango cha asilimia 60, kwa hiyo tulifumua sheria zetu zote hivyo mwaka 2017 tukafanyiwa ukaguzi na tukafikia asilimia 69.4 tukatunukiwa tuzo ya kufikia mafanikio hayo.
Pia, tumefanyiwa mwingine na Shirika la Uslama wa Anga Duniani, ukaguzi huo umekamilika mwezi Mei na tumepata asilimia 86.7 hii ina ashiria kuwa mashirika ya ndege yanayotaka kuja hapa nchini yawe na uhakika kuwa nchi yetu ni salama,”amesema.
Amesema ni miaka 20 sasa tangu mamlaka hiyo kuanzishwa mwaka 2003 kwa Sheria ya Bunge 10 ya mwaka 2003 wamekuwa na mafanikio mbalimbali ikiwemo ununuzi wa rada nne.
Johari amesema tayari wanafanya majadiliano na nchi ya Marekani ili kufikia makubaliano ndege za Tanzania zitue nchini humo.
Kuhusu mapato ya ndani amesema, kuanzia mwaka 2017 hadi 2022 TCAA ilikusanya Sh319.9 bilioni na kuchangia mfuko mkuu wa Serikali Sh24.8 bilioni.
Majukumu ya TCAA
TCAA ni mamlaka chini ya Serikali ambayo baadhi ya majukumu yake ni kutoa na kubadili leseni za huduma za anga kuweka viwango vya sheria na masharti ya usambazaji wa bidhaa na huduma zinazodhibitiwa; kusambaza taarifa kuhusu mambo yanayohusiana na kazi za TCAA pamoja na kuwezesha utatuzi wa malalamiko na migogoro.