Fursa ya mikopo sasa nje nje kwa wanafunzi stashahada

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda
Muktasari:
Idadi ya wanafunzi wa vyuo vya kati inatarajiwa kuongezeka baada ya kuzinduliwa kwa mwongozo wa utoaji mikopo ngazi ya stashahada kuanzia mwaka wa masomo 2023/2024 katika fani sita za kipaumbele.
Dar es Salaam. Idadi ya wanafunzi wa vyuo vya kati inatarajiwa kuongezeka baada ya kuzinduliwa kwa mwongozo wa utoaji mikopo ngazi ya stashahada kuanzia mwaka wa masomo 2023/2024 katika fani sita za kipaumbele.
Mwongozo huo umezinduliwa leo ikiwa ni takribani miezi saba baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kueleza kuwa Serikali inaangalia uwezekano wa kutoa mikopo kwa ngazi hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo Jumatano Oktoba 4, 2023, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kiasi cha Sh48 bilioni kwa ajili ya mikopo hiyo.
Fedha hizo zitatolewa kwa wanafunzi 8,000 katika maeneo sita ya vipaumbele yenye uhitaji mkubwa wa wataalamu ambayo ni afya na sayansi shirikishi, ualimu wa hisabati, fizikia na mafunzo ya amali, uhandisi na nishati, madini na sayansi ya ardhi na kilimo na mifugo.
Waziri Mkenda ameeleza kuwa maeneo hayo ya vipaumbele yamechaguliwa baada ya Serikali kufanya tathmini ya uhitaji mkubwa wa watalaamu katika ngazi ya kati.
“Serikali imejenga hospitali, zahanati na vituo vya afya nchini kote ambavyo vinahitaji wataalamu. Serikali pia imejenga na kukarabati shule ambazo zinahitaji walimu wa sayansi pia inatekeleza mageuzi katika sekta za mafuta, gesi, madini na sekta ya kilimo.
“Baada ya kufanya tathmini tumeona tuanze na maeneo haya ili kuwapa fursa vijana wetu kupata ujuzi na kuweza kuajirika baada ya kuhitimu masomo yao,” amesema Profesa Mkenda.
Kutolewa kwa mwongozo huo kutafuatiwa na kufunguliwa kwa dirisha la kupokea maombi kwa njia ya mtandao kwa siku 15 kuanzia Oktoba 7 hadi 22, 2023.
“Niwasisitize waombaji watumie siku nne kusoma mwongozo na kuangalia vigezo ambavyo vimewekwa maana usije ukaona afya ukafikiri kila fani ya afya itatolewa mkopo, kuna maeneo tumeyaangalia.
“Tusingependa kuona watu wanaostahili wanakosa mkopo kwa sababu ya kushindwa kuzingatia vigezo. Kitu kingine muhimu waombaji watambue kuwa baada ya kumaliza masomo wanufaika watarejesha mkopo kwa kiwango cha asilimia 15 kutoka kwenye mishahara yao ya mwezi,” alisema Profesa Mkenda.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Nactvet), Dk Adolf Rugayugwa amesema mikopo hiyo inaenda kuongeza idadi ya watalaamu katika kada za kati.
Amesema wapo ambao licha ya kuwa nia ya kusoma katika ngazi hiyo wameshindwa kutokana na programu kuwa na gharama kubwa hivyo mikopo italeta hamasa kubwa.
“Tumesubiri kwa muda mrefu suala hili, wanafunzi wa stashahada wakipata mikopo itaongeza idadi ya wanafunzi kwenye kada hii ambayo ni muhimu katika kutengeneza wafanyakazi. Kwa sasa ukiangalia takwimu wenye shahada ni wengi kuliko wenye stashahada kitu ambacho si kizuri, utendaji kazi unahitaji mchanganyiko wa kada hizi,” amesema Dk Rutayugwa.
Rais wa Shirikisho la Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso), Maria John amewataka wanafunzi wa stashahada kuchangamkia fursa hiyo ambayo imekuwa ikiombwa kwa muda mrefu.
“Kwa muda mrefu tulihitaji hili, tulimuomba Rais na hatimaye ametusikia linaenda kutekelezwa, wito wangu kwa wanafunzi tuitumie vyema fursa hii.
“Serikali imetupatia mikopo ili tusome basi twende tukasome ili lengo la kutupa mikopo hii litimie, tupate ujuzi na maarifa tulitumikie taifa na tusisahau tunawajibika kuirejesha mikopo hii na wengine wapate,” amesema Maria
Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (HESLB), Profesa Hamis Dihenga amesema ufuatiliaji wa kina utafanyika kuhakikisha mikopo hiyo inatolewa kwa ufanisi na kuwafikia walengwa.