Fao yatoa Sh1.6 bilioni kwa kituo cha utafiti wa mbogamboga Arusha

Katibu wa Usimamizi wa Mikataba ya Kimataifa wa Fao, Uhifadhi wa Vinasaba vya Mbegu, Dk Kent Nnadozie (kushoto) akibadilishana mkataba wa makubaliano na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini ya Kituo cha Utafiti wa Mbogamboga na Matunda cha Kimataifa, Dk Gabriel Rugalema jijini Arusha leo Machi 5, 2024. Picha na Janeth Mushi
Muktasari:
- Lengo la Fao kukabidhi fedha hizo ni kukuza na kuboresha kilimo cha mbogamboga hapa nchini na Afrika.
Arusha. Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (Fao), limesaini makubaliano ya awali na Kituo cha Utafiti wa Mbogamboga na Matunda cha Kimataifa na kukipatia Dola 650,000 za Marekani (Sh1.6 bilioni) kwa ajili ya kuboresha benki ya mbegu iliyopo kituoni hapo.
Hayo yamesemwa leo Machi 5, 2024 jijini Arusha na Katibu wa Usimamizi wa Mikataba ya Kimataifa wa Fao, Uhifadhi wa Vinasaba vya Mbegu, Dk Kent Nnadozie wakati wa utiaji saini makubaliano hayo yaliyofanyika katika ofisi za kituo hicho eneo la Tengeru.
Amesema lengo la Fao kukabidhi fedha hizo kwa kituo hicho ni kukuza na kuboresha kilimo cha mbogamboga hapa nchini na Afrika.
Dk Nnadozie amesema kituo hicho kina wajibu wa kuboresha na kukuza kilimo hicho sambamba na kuongeza idadi ya mbegu katika benki yake iliyopo kituoni hapo ili kuhakikisha uchumi unakua na usalama wa mbegu unakuwepo.
Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini wa kituo hicho, Dk Gabriel Rugalema amesema mkataba huo umesainiwa chini ya mkataba wa kidunia wa kuangalia masuala ya viini lishe na vinasaba duniani.
Amesema wameungana kwa kuwa wote wana malengo yanayofanana ikiwamo kufanya dunia iwe na chakula salama na chenye kuleta afya nzuri, kilimo kipanuke kiweze kuwasaidia watu kuwa na lishe bora na kipato kizuri na ajira za uhakika kwa vijana.
"Tumekubaliana watasaidia benki ya mbegu ambayo miaka miwili imekuwa ikijengwa hapa na imekuwa bora zaidi lakini tunahitaji rasilimali fedha ili kuiendeleza, zitasaidia kwenye tasnia hii ya vipando vya mbogamboga, duniani kuna aina zaidi ya mbegu milioni moja," amesema Dk Rugalema.
"Sisi hapa kwenye benki yetu ya mbegu tunazo aina zaidi ya 7,000 kwa hiyo lazima tuendelee kukusanya,kuchakata na kutunza kwa muda mrefu ili hizo mbegu zitumike kuzalisha mbegu mpya na katika tafiti za kisayansi na kuendeleza kilimo cha mboga katika nchi za Afrika." Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa wanatarajia hadi mwakani kuwa na mbegu 15,000 na hadi kufikia mwaka 2030 watakuwa na mbegu 40,000.
“Watanzania watarajie uchakataji, ukusanyaji na utunzaji wa mbegu ndio msingi wa kilimo cha mboga mboga, hivyo Watanzania wanapaswa kukitumia vema kituo hicho katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa jumla,” amesema Rugalema.