Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fao yatahadharisha upungufu wa chakula nchini

New Content Item (1)

Mratibu wa miradi ya kilimo kutoka FAO, Tanzania, Diomedes Kalisa akitoa mada katika mafunzo ya wakaguzi wa viuatilifu, juu ya Sheria, kanuni na taratibu za matumizi na biashara za bidhaa hizo, yanayoendelea mjini Moshi. Picha na Bertha Ismail.

Muktasari:

  •  Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (Fao), limesema kuwa Tanzania iko katika hatari ya upungufu wa chakula siku zijazo kutokana na mwenendo mbaya wa matumizi ya kemikali katika kilimo.

Moshi. Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (Fao), limeitaka Tanzania kuchukua tahadhari juu hatari ya upungufu wa chakula unaoweza kutokea siku zijazo.

Fao imeitaka Tanzania kuhamasisha wakulima kupunguza matumizi makubwa ya kemikali katika kilimo pia Serikali ichukue hatua za haraka za kuhuisha mpango mkakati wa Taifa ulioisha muda wake juu ya urejeshaji wa bioanuai kwenye mazingira yake ili kusaidia shughuli za uchavushaji mimea kwenye mazao kufanyika.

Hayo yameelezwa leo Januari, 9, 2024, mjini Moshi na Mratibu wa miradi ya kilimo kutoka ofisi ya Fao nchini, Diomedes Kalisa kwenye mafunzo ya wakaguzi wa viuatilifu juu ya Sheria, kanuni na taratibu za matumizi na biashara za bidhaa hizo.

Kwa mujibu wa utafiti walioufanya, Kalisa amesema matumizi makubwa ya kemikali katika shughuli za kilimo, yamesababisha kupotea kwa Bioanuai ndani ya udongo, ambayo husaidia kukamilisha kazi yake ya uchakataji na kutoa rutuba inayotakiwa katika ustawi wa mazao.

Kupitia mradi wa kujengea uwezo kuhusiana na utekelezaji wa mikataba ya kimataifa ya kimazingira unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU), Kalisa amesema Fao wameanza kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya wakulima katika mikoa sita nchini, juu ya hatari ya matumizi ya kemikali katika kilimo hasa zile zisizofaa au kuisha mda wake.

Amesema Tanzania ikiwa ni moja ya nchi nne za Afrika wanufaika wa mradi huo, wakulima kutoka mikoa ya Da-es-salaam, Iringa, Mbeya, Morogoro Arusha na Kilimanjaro wamefikiwa.

“Malengo makubwa ya mradi huu ni kuangalia kwa namna gani bioanuai ambazo zimeanza kupotea zinaweza kuhuishwa kwa mustakabali wa mazingira na ustawi wa binadamu kupitia uhakika wa uchavushaji wa mazao,” amesisitiza Kalisa.

Amesema wanahamasisha wakulima kupunguza matumizi ya kemikali katika urutubishaji wa udongo badala yake watumie njia mbadala zinazopatikana katika mazingira yao kwa kuzingatia usalama wa kimazingira na kwa afya ya walaji lakini pia kwa mahitaji ya soko la kimataifa.

“Pia tunawaambia madhara ya kemikali zisizo na ubora ambazo hazijahakikiwa na mamlaka husika za mimea na dawa, na zile salama watumie kwa kiasi kidogo sana pale inapobidi,” ameongeza Kalisa.

Awali akifungua mafunzo hayo, Mkurgenzi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu nchini (TPHPA), Joseph Ndunguru amesema mafunzo hayo kwa wakaguzi 32 wa viuatilifu nchini, yanalenga kuongeza pato la Taifa litokanalo na kilimo kupitia utatuzi wa visumbufu mimea kwa wakulima.

Kupitia matumizi ya viuatilifu sahihi na vyenye ubora, Ndunguru amesema wakulima wataweza kupata tija ya kilimo chao lakini pia kuboreka kwa masoko ya mazao nje ya nchi na kuongeza pato la wananchi na taifa kwa ujumla.

“Mafunzo haya yatawasaidia wataalamu wetu hawa kujua sheria, kanuni na taratibu mpya za viuatilifu na wataweza kuvizibiti kuanzia mipakani visiingie na madukani visiwepo kuwafikia wakulia wetu ambao wamekuwa wakipata hasara kupitia bidhaa hizo,” ameongeza mkurugenzi huyo.

Mmoja wa washiriki katika mafunzo hayo, Kaimu meneja wa TPHPA Kanda ya Kusini, Lilian Muyaga, amesema kuwa kupitia mafunzo hayo, wanatarajia kujua jinsi ya kukagua viuatilifu lakini pia adhabu za sheria mpya za viuatilifu zilizotoka hivi karibuni.

“Mbali na hilo tutapata muda wa kubadilishana uzoefu wa kazi wa mbinu chafu za biashara ya viuatilifu ili tuweke kukabiliana nazo kwa pamoja kwa manufaa ya wakulima na nchi kwa ujumla,” amesema Lilian.